Wanawake 100 kupelekwa China kujifunza ujasiriamali, uzalishaji

Meneja Masoko wa Yas Tanzania, Joshua Swayi (kulia) akimkabidhi tuzo, malkia wa nguvu (sekta ya uvuvi) Elelhah James. Kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya Misungwi, Johari Samizi. Picha na Mpiga Picha Wetu.
Muktasari:
- Safari za kuwapeleka wanawake hao nchini China zitaanza kuratibiwa kati ya Agosti na Septemba mwaka huu.
Mwanza. Wanawake 100 nchini wanatarajiwa kupelekwa China kwenda kujifunza teknolojia ya uzalishaji, ujasiriamali, masoko, namna ya kutangaza bidhaa na kuinua mitaji ya biashara zao.
Kauli hiyo imetolewa na Mwenyekiti wa Jukwaa la Malkia wa Nguvu, Lilian Masuka wakati wa hafla ya utoaji wa Tuzo za Malkia wa Nguvu, mkoani Mwanza usiku wa kuamkia leo Jumapili Aprili 27, 2025.
Masuka amesema baada ya kufanya hafla za utoaji wa tuzo zinazotambua mchango wa wanawake katika ujasiriamali, biashara, uzalishaji na utoaji wa huduma kwa umma, wamebaini kuna mkwamo miongoni mwao hususan kukosa uzoefu wa namna ya kuendesha shughuli zao.
“Jukwaa la Malkia wa Nguvu tumezunguka kanda ya ziwa kwenye wilaya tofauti tofauti tukizungumza na malkia wa nguvu, ni rasmi 2025 (mwaka) tutawapeleka wanawake 100 nchini China kujifunza teknolojia, wenzetu unakuta ana kiwanda hapa mpaka hapa (kidogo) lakini uzalishaji wake ni mkubwa,” amesema Lilian.
Amesema safari za kuwapeleka wanawake hao China zitaanza kuratibiwa kati ya Agosti na Septemba mwaka huu, huku wanawake wanaojishughulisha na ujasiriamali, uzalishaji, biashara na sekta nyingine za uzalishaji wakitakiwa kujisajili kupitia kurasa za jukwaa la malkia wa nguvu 2025.
“Hivyo, tumeona tuwapeleke malkia wa nguvu China mkajifunze teknolojia inafanyaje kazi, masoko, branding (kujitangaza), kufungasha bidhaa, pia tuangalie wenzetu wana mtaji mdogo wanatoboa toboaje?”
Akizungumzia uamuzi huo, mshiriki wa hafla hiyo, Elizabeth Samuel amesema uamuzi huo si tu utabadilisha mtazamo wa wanawake, pia utapandikiza taswira mpya katika akili ya mwanamke wa Kitanzania atakayoweza kuipandikiza kwa wenzake na kuleta mabadiliko chanya nchini.
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Said Mtanda amewataka wanawake kujiamini na kutumia fursa walizonazo kuonesha uwezo wao kama alivyofanya Rais Samia Suluhu Hassan ambaye ameuthibitishia ulimwengu kuwa mwanamke anaweza kufanya chochote ikiwamo kuongoza nchi.
"Taifa letu limebahatika sana kuwa na Malkia wa Nguvu, Samia Suluhu Hassan kama Rais kwa sababu kwa haiba na utashi wake ameweza kusimamia tunu zetu za Taifa ambazo Amani, Upendo na Umoja wa Kitaifa. Hilo linatosha kabisa kutufanya tukubali kwamba Malkia wa Nguvu wana uwezo mkubwa wa kulea, kuongoza na kusimamia,” amesema Mtanda.
Kupitia jukwaa hilo wanawake mbalimbali walitunukiwa tuzo za kuthamini mchango wao katika jamii miongoni mwao ni mjasiriamali, Salma Mipawa aliyetunukiwa tuzo ya Malkia wa Nguvu katika sekta madini, Mganga Mfawidhi Hospitali ya Sekou Toure, Dk Bahati Msaki aliyetwaa tuzo ya Malkia wa Nguvu katika Uongozi na Elelah James (sekta ya uvuvi).
Pia kuna, Veronica Sarakikya (tuzo ya ufunguo wa maisha), Mkurugenzi wa Shamba la Mifugo la Lake Farm na Lake Zone Food Products, Joyce Kabago (aliyetunukiwa tuzo ya sekta ya kilimo na biashara) na Dk Emmanuela Ambrose ambaye Daktari Bingwa wa Saratani kwa Watoto Bugando (sekta ya afya).
Wakati huo huo, Mariam Warioba ametunukiwa tuzo ya Malkia wa Nguvu sekta ya elimu, Alphoncia Barongo ambaye ametunukiwa tuzo mfanyabiashara bora huku tuzo ya ‘Inspirational Icon’ ikienda kwa Rhobi Alphonce ambaye alipambana kutetea haki ya mwanamke mkoani Mara.