Tanzania kutumia roboti utoaji wa huduma za Posta
Naibu Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhandisi Merryprisca Mahundi akifungua mkutano wa 42 wa Baraza la Wataalam wa Umoja wa Posta Afrika (PAPU) jijini Arusha. Picha na Bertha Ismail
Muktasari:
- Hayo yamesemwa leo Jumanne Juni 11 na Naibu Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Merryprisca Mahundi alipofungua mkutano wa 42 wa Baraza la Wataalamu wa Umoja wa Posta Afrika
Arusha. Wakati Umoja wa Posta Afrika (Papu) ukijipanga kuanzisha jukwaa la pamoja la biashara mtandao, Tanzania iko mbioni kuanza kutumia roboti katika utoaji wa huduma za vifurushi.
Hayo yamesemwa leo Jumanne Juni 11 na Naibu Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Merryprisca Mahundi alipofungua mkutano wa 42 wa Baraza la Wataalamu wa Umoja wa Posta Afrika kutoka nchi wanachama 45.
Wadau hao wanakutana Jijini Arusha kujadili changamoto, utatuzi na fursa zilizopo katika uboreshaji wa huduma za posta katika nchi za Afrika.
Mahundi amesema wizara yake iko mbioni kufanikisha matumizi ya roboti katika utoaji wa huduma zake.
Amesema katika kusaidia Shirika la Posta ili iendelee kukua na kutanuka kwa matumizi ya kidigitali, matumizi ya roboti yatakuwa suluhu la kudumu.
"Lakini hatuishii hapo, tutahakikisha wizara inakwenda kujitanua katika ulimwengu wa kidigitali kama kutumia roboti, basi na Posta Afrika tutawashauri waweze kufikia huko" amesema Mahundi.
Postamasta Mkuu wa Tanzania, Maharage Chande amesema kutokana na kukua kwa mawasiliano ya teknolojia, Shirika la Posta lina nafasi kubwa ya kufanya biashara.
Amesema kwa kulitambua hilo, wameanza kutengeneza maabara maalumu itakayokuwa na wataalamu wa kufanya programu za kutengeneza majukwaa kwa ajili ya biashara mtandao kutoka nchi zote wanachama.
"Nchi za Afrika tutashirikiana kutengeneza majukwaa mbalimbali kwa ajili ya biashara ambayo yatasaidia wananchi wa nchi za ukanda huu wa kaskazini kuweka bidhaa zao kwa ajili ya wateja wa nchi za ukanda wa kusini,” amesema Chande.
Amesema pia wanatarajia kupitisha kanuni na miongozo itakayosaidia namna bora ya uboreshaji wa jukwaa hilo la biashara kwa masilahi mapana ya wananchi wa nchi wanachama.
"Katika hili, teknolojia ya akili mnemba haiepukiki ambayo yenyewe itatusaidia kujua taarifa mbalimbali za mahitaji ya bidhaa na maeneo husika kwa ajili ya wananchi wetu kuchangamkia,” amesema Chande.
Mkurugenzi wa Huduma za Sheria kutoka Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Dk Philip Filikunjombe amesema wanaendelea kuweka mazingira wezeshi kwa ajili ya watoa huduma za posta wakilenga kurahisisha usafirishaji wa vifurushi na bidhaa mbalimbali.
"Mazingira wezeshi ndio msaada mkubwa utakaosaidia huduma hizi ziweze kufanikiwa,” amesema Filikunjombe.
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Papu, Dk Sifundo Moyo amesema lengo la mkutano huo ni kujadili fursa na changamoto kwa lengo la kupata majibu chanya yatakayosaidia maboresho.
Amesema katika mkutano huo wanatarajia kuazimia sera moja na utaratibu wa utoaji wa huduma za posta katika nchi wanachama kwa ajili ya hatima ya shirika hilo kwa miaka zaidi ya mitano ijayo.
"Hii itasaidia mbali na kuitangaza Afrika kibiashara katika mataifa ya Ulaya lakini pia itakuza uchumi wa wananchi wa kawaida hasa kupitia jukwaa la pamoja na kibiashara,” amesema.