Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Takukuru yataja Tanzania ilivyoingiza maudhui ya rushwa mtalaa wa elimu

Muktasari:

  • Mkutano wa 15 wa Kanda wa Wakuu wa Mashirika ya Kupambana na Rushwa katika Afrika wa Jumuiya ya Madola unafanyia nchini Afrika Kusini ukiwa na lengo la kupata suluhisho la pamoja dhidi ya rushwa.

Dar es Salaam. Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Crispin Chalamila ameshiriki mkutano wa 15 wa Kimataifa wa Wakuu wa Mamlaka za Kupambana na Rushwa kwa Nchi za Jumuiya ya Madola - Kanda ya Afrika unaofanyika Cape Town, Afrika Kusini kwa siku tano.

Mkutano huu unaotarajiwa kuhitimishwa kesho Ijumaa Mei 9, 2025, una lengo la kuimarisha ushiriki wa wadau hususani taasisi za Serikali na zisizo za Serikali, katika kuzuia na kupambana na rushwa Barani Afrika.

Kupitia mkutano huo Mkurugenzi Mkuu Takukuru, Chalamila ameeleza namna ambavyo Tanzania imeingiza maudhui ya kupinga rushwa katika mtaala wa elimu ikiwa ni hatua ya mafanikio katika jitihada za kuzuia na kupambana na rushwa.

Katika mkutano huo, Mkurugenzi Mkuu huyo ameambatana na Mkurugenzi wa Elimu kwa Umma, Joseph Kasongwa  Mwaiswelo na Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Arusha, Zawadi Ngailo.

Mkutano huo unaowakutanisha viongozi kutoka mataifa 21ya Afrika ili kuandaa mikakati ya utekelezaji ukiwa na kaulimbiu “Kuimarisha Ushiriki Jumuishi wa Wadau wa Serikali na Wasio wa Serikali katika Kuzuia na Kupambana na Rushwa.”

Awali, mkutano huo ulifunguliwa na Waziri wa Sheria na Maendeleo ya Katiba wa Afrika Kusini, Mmamoloko Kubayi, Mei 5 Jumatatu.

Waziri Kubayi amesema, “Rushwa inaweza kuharibu taasisi ndani ya nchi kiasi cha kuwagharimu wananchi kupata huduma wanazostahili. Rushwa hupunguza imani ya wawekezaji katika biashara na kuwafukuza na hivyo kuiweka nchi katika hali ya ukuaji mdogo wa uchumi.”

Waziri Kubayi pia amehimiza kuwepo mijadala mbalimbali kuhusu kuzuia rushwa ikiwa ni njia mojawapo ya kuongeza uelewa kwa wananchi.

“Iwapo haitazuiwa na kupigwa vita, rushwa inaweza kuwa njia ya makundi ya uhalifu,” amesema Waziri Kubayi.


Mkuu wa Kitengo Maalumu cha Upelelezi  (SIU) nchini Afrika Kusini, Wakili Andy Mothibi amesema Rais wa zamani wa Afrika Kusini, Thabo Mbeki, amewahi kusema kwamba matatizo ya Afrika yanahitaji suluhisho la Kiafrika, hivyo mkutano huo ni fursa muhimu kwa mataifa ya Afrika kuungana katika mapambano dhidi ya rushwa.

“Mkutano huu unatupa fursa ya kushirikiana rasilimali, kubadilishana uzoefu na kujenga nguvu ya pamoja. Muhimu zaidi, kadri teknolojia inavyoendelea, ndivyo mbinu za kufanikisha mtiririko haramu wa fedha kuvuka mipaka zinavyozidi kubadilika. Tunapaswa kuungana kuzikomesha mapema na kuwazidi ujanja wahalifu,” amesema.

Mkutano huu umeandaliwa chini ya mwamvuli wa Jumuiya ya Wakuu wa Mashirika ya Kupambana na Rushwa katika Afrika ya Jumuiya ya Madola, mtandao wa ushirikiano unaojumuisha taasisi za kupambana na rushwa kutoka nchi 21 za Afrika.

Nchi zinazoshiki mkutano huo ni Botswana, Cameroon, Eswatini, Ghana, Gabon, Kenya, Lesotho, Malawi, Mauritius, Msumbiji, Namibia, Nigeria, Rwanda, Shelisheli, Sierra Leone, Afrika Kusini, Tanzania, Togo, Uganda, na Zambia. Kitengo Maalumu cha Upelelezi (Special Investigating Unit) kinaunda mwenyeji wa Mkutano kwa niaba ya Afrika Kusini.

Mkutano huu utatoa maazimio juu ya vitendo vya rushwa ili kuimarisha juhudi za kupambana na rushwa katika bara la Afrika, ikiwa ni pamoja na Mikakati bunifu, ushirikiano kati ya umma na binafsi, kuimarisha ushirikiano kati ya serikali, jamii ya kiraia, na sekta binafsi ili kuziba mianya katika mifumo ya utawala, ujenzi wa uwezo, ushirikiano wa kikanda.

Rushwa hupunguza kasi ya ukuaji wa uchumi, huongeza umasikini na huharibu imani ya umma.

Mkutano huu utachochea suluhisho la vitendo na jumuishi kulinda mafanikio ya maendeleo na kuhakikisha uadilifu katika taasisi zote.