Takukuru yabaini mapungufu kwenye miradi ya Sh6.5 bilioni

New Content Item (1)
New Content Item (1)

Muktasari:

Miradi 22 yenye thamani ya zaidi ya Sh6.5 bilioni iliyochunguza na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini Tanzania (Takukuru) mkoani Mwanza imebainika kuwa na mapungufu kadhaa ikiwemo ukiukwaji wa taratibu za manunuzi, kasi ndogo ya utekelezaji na ubora hafifu.

Mwanza. Miradi 22 yenye thamani ya zaidi ya Sh6.5 bilioni iliyochunguza na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini Tanzania (Takukuru) mkoani Mwanza imebainika kuwa na mapungufu kadhaa ikiwemo ukiukwaji wa taratibu za manunuzi, kasi ndogo ya utekelezaji na ubora hafifu.

Kwa mujibu wa Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Mwanza, James Ruge, miradi hiyo ni kati ya miradi ya maendeleo 130 yenye thamani ya zaidi ya Sh30.4 bilioni ambayo utekelezaji wake ulichunguzwa na taasisi hiyo kati ya Oktoba Mosi hadi Desemba 31, 2022.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Mwanza leo Jumatano Machi 22, 2023, Mkuu huyo wa Takukuru amesema miradi iliyochunguzwa ni kutoka sekta za afya, elimu, ujenzi na maji.

Amesema Takukuru imebaini kasi ndogo ya utekelezaji wa miradi ya ujenzi wa vyumba vyumba 92 vya madarasa katika shule 12 za Halmashauri ya Jiji la Mwanza.

"Mkurugenzi wa Jiji la Mwanza ameshauriwa kutoa fedha za kutosha kulingana na makadirio kuwezesha miradi hiyo kukamilika kwa wakati," amesema Ruge.

Mradi mwingine uliobainika kuwa na kasoro ni ujenzi wa Zahanati ya Mihama, Manispaa ya Ilemela uliogharimu zaidi ya Sh 92 milioni ambao msingi wake umebainika kuwa mfupi na umetekelezwa eneo lenye chemichemi.

Kutokana na kasoro hizo, Takukuru imeuagiza uongozi wa Manispaa ya Ilemela kuzingatia kanuni ya ujenzi kwenye maeneo tepetepe ikiwemo kuimarisha na kujenga msingi mrefu.

Miradi mingine iliyobainika kuwa na kasoro na maelekezo ya maboresho kutolewa ni ujenzi wa barabara zinazounganisha vijiji tisa vya Mantare- Mwanekeyi, Maligisu- Mwabasabi, Manawa- Nyamigamba na Mhulula- Chamva ambayo vifusi vilivyotumika vimebainika kutostahili.

Katika mradi wa maji eneo la Sagani Wilaya ya Magu unaotekelezwa kwa gharama ya zaidi ya  Sh 2.5 bilioni nao umebainika kutekelezwa chini ya kiwango kutokana na kina cha mitaro ya mabomba kubainika kuwa fupi.