Tahadhari upepo mkali, mawimbi kukumba kanda za Pwani, ziwa Nyasa, Victoria

Muktasari:
- Mamlaka ya Hali ya Hewa nchini (TMA), imetoa angalizo la upepo mkali na mawimbi maeneo ya mikoa ya ukanda wa pwani ya bahari ya Hindi pamoja na ukanda wa Ziwa Victoria na Ziwa Nyasa kwa siku tano.
Dar es Salaam. Tahadhari ya uwepo wa upepo mkali unaofikia kilomita 40 kwa saa na mawimbi makubwa yanayofikia mita mbili itakayodumu kwa siku tano kuanzia kesho Alhamisi, imetolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa (TMA), leo Julai 26, 2023.
Kupitia taarifa yake TMA, imetaja baadhi ya maeneo ya ukanda wa pwani ya bahari ya Hindi, mikoa ya Lindi, Mtwara, Tanga, Dar es Salaam na Pwani, ikijumuisha visiwa vya Mafia pamoja na visiwa vya Unguja na Pemba.
Pia tahadhari hiyo imetolewa kwa baadhi ya maeneo ya ukanda wa Ziwa Victoria (mikoa ya Kagera, Geita, Mwanza, Simiyu na Mara) pamoja na ukanda wa Ziwa Nyasa, mikoa ya Mbeya, Njombe na Ruvuma.
TMA imezitaja athari zinazoweza kujitokeza ambazo ni kuathirika kwa baadhi ya shughuli za uvuvi na usafirishaji baharini.
Mamlaka hiyo imekuwa ikitoa tahadhari za mara kwa mara katika siku za usoni ambapo mara ya mwisho ilitoa taarifa ya uwepo wa hali mbaya ya hewa mnamo Julai 13.