TaCRI yaja na mkakati kudhibiti konokono wasumbufu wa kahawa

Baadhi ya miche bora ya kahawa iliyozalishwa kwa ajili ya msimu huu wa kilimo
Muktasari:
- Hatua hiyo imekuja kufuatia uwepo wa athari kubwa katika uzalishaji wa mazao mengine ya kimkakati hususani, kahawa nyanya, mahindi, maharage katika mikoa ya Mbeya na Songwe.
Songwe. Licha ya kuwepo kwa mikakati kabambe ya kuzalisha miche milioni 5 ya zao la kahawa yenye uwezo wa kukabiliana na magonjwa, wadudu aina ya konokono ambao wametajwa kuathiri kwa kiwango kikubwa uzalishaji.
Hatua hiyo imesababisha watafiti wa Taasisi ya Utafiti wa Zao la Kahawa (TaCRI), Kituo cha Mbimba Wilaya ya Mbozi Mkoa wa Songwe kujifungia kufanya tafiti za kina kusaka mwarobaini wa kuwadhibiti.
Akizungumza na Mwananchi Digital leo Jumanne Juni 3, 2025, Meneja wa Programu za Utafiti wa Zao la Kahawa Mikoa ya Mbeya na Songwe, Dismass Pangarasi amesema wadudu aina ya konokono licha ya kuathiri zao hilo pia wameshambulia mazao mengine yakiwepo maharage na mahindi.
Pangarasi amesema kufuatia hali hiyo watafiti watajifungia kufanya tafiti za kina ili kupata mwarobaini wa kuwadhibiti ili kunusuru uzalishaji sambamba na kuzalisha miche bora aina ya 'compact' yenye uwezo wa kukabiliana na magonjwa aina ya chulebuni na kutu ya majani ya kahawa.
"Aina hii ya magonjwa yamekuwa yakisababisha kwa kiasi kikubwa kupunguza uzalishaji, lakini pia ukiangalia gharama za kuzuia inaweza kuchangia asilimia 60 za uzalishaji wa shamba jipya la kahawa kuanzia hatua za awali mpaka kuvuna," amesema.
Amesema katika msimu huu wa kilimo Taasisi ya TaCRI, wameweka mikakati ya kuzalisha vitalu vya miche bora ya kahawa milioni 5 yenye uwezo wa kukinzani wa magonjwa, huku kitaifa ni kufikia uzalishaji wa miche milioni 20 mpaka miche milioni 30.

Baadhi ya miche bora ya kahawa iliyozalishwa kwa ajili ya msimu huu wa kilimo
Pangarasi amesema lengo la kuweka mikakati hiyo ni kutekeleza takwa la kitaifa kuzalisha tani 300,000 za zao la kahawa kwa msimu huu.
"Lengo ni kuongeza tija ya kufikia mikakati ya serikali kuongeza uzalishaji wa zao la kahawa iliyo bora yenye uwezo wa kuleta ushindani soko la ndani na nje ya nchi," amesema.
Changamoto na mikakati
Pangarasi amesema mahitaji yamekuwa makubwa kuliko uwezo wa kuzalisha miche ya mbegu bora, lakini pia upatikanaji wa rasirimali fedha ili kuwafikia wakulima wengi.
"Kuna nguvu kazi ya wananchi kuhitaji kuwekeza kwenye kilimo cha zao la kahawa, lakini changamoto ukosefu wa rasilimali fedha kwa ajili ya kuzalisha mbegu bora sambamba ukosefu wataalamu ili kukidhi mahitaji ya sasa ,"amesema.
Changamoto nyingine ni kuibuka magonjwa na wadudu waharibifu ambao miaka ya nyuma hawakuwepo hususani konokono ambao wameleta athari kubwa kwa wakulima wa mikoa ya Kanda ya Nyanda za Juu Kusini.
"Athari hiyo imeleta msukumo kwa watafiti kuingia kazini kufanya tafiti za kina za athari ya konokono katika mazao ya kimkakati hususani kahawa ili kuifanya kuwa endelevu ,"amesema.
Hali ya uzalishaji
Pangarasi mesema kwa miaka 10 iliyopita kwa Wilaya ya Mbozi Mkoa wa Songwe uzalishaji wa kahawa ulikuwa tani 10,000, huku msimu wa mwaka 2025 uzalishaji umeongezeka na kufikia tani 12,000, lakini mikakati katika msimu huu wa kilimo ni kufikia tani 15,000.
Kauli za wakulima
Mkulima wa Kata ya Nyimbili Wilaya ya Mbozi, Anania Simbeye amesema katika misimu miwili ya kilimo kilio kikubwa ni magonjwa ya majani na konokono kushambulia kahawa jambo ambalo limefifisha uzalishaji.
"Tuombe Serikali kuwezesha vituo vinavyofanya tafiti za zao la kahawa kuwasaidia wakulima kukabiliana na wadudu waharibifu na namna ya kuwadhibiti,"amesema.
Mkulima Tinson Nzunda na Diwani Kata ya Nyimbili, amesema mbali na changamoto hizo elimu kwa wakulima yahitajika ili kufukia malengo ya uzalishaji wenye tija kubwa na kujikwamua kiuchumi.
Ametaja changamoto nyingine inayoathiri sekta ya kilimo ni mabadiliko ya tabianchi jambo ambalo linasababisha mkulima kutumia gharama kubwa za uzalishaji tofauti na anachovuna.