Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

TaCRI yapata aina tatu mpya za Arabika zitakazokabiliana na ukame

Muktasari:

  • Taasisi ya utafiti wa Kahawa nchini (TaCRI) imegundua aina mpya Tatu za Kahawa aina ya Arabika yenye uwezo wa kuvumilia hali ya ukame, ikiwa ni moja ya mikakati ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na kuongeza uzalishaji wa zao hilo.

Moshi. Taasisi ya utafiti wa Kahawa nchini (TaCRI) imegundua aina mpya tatu za kahawa aina ya Arabika yenye uwezo wa kuvumilia hali ya ukame, ikiwa ni moja ya mikakati ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na kuongeza uzalishaji wa zao hilo.

Hayo yamebainishwa leo, Mei 3, 2025 na Mtafiti mwandamizi wa afya ya udongo katika taasisi hiyo, Dk Godsteven Maro wakati akizungumza kuhusiana na mikakati iliyopo katika kuboresha zao la kahawa nchini.

Dk Maro ambaye pia ni msimamizi wa programu ya kilimo bora, amesema kwa sasa wameanza kuzalisha kwa wingi aina hizo za kahawa zinazovumilia ukame na kuzisambaza maeneo yenye changamoto hiyo hatua ambayo itawezesha kuzalishwa kahawa maeneo ambayo yana ukame.

"Kama tunavyofahamu kumekuwepo na changamoto ya mabadiliko ya Tabianchi,tulianza mchakato wa kutambua aina za kahawa ambazo zinahimili ukame ambapo tumefanya majaribio mtawanyiko karibu nchi nzima katika maeneo yenye ukame"amesema Dk Maro na kuongeza kuwa,

"Tumeweza kuthibitisha aina tatu za kahawa aina ya Arabika ambazo zinavumilia hali ya ukame, tunaendelea kuzizalisha kwa wingi ili kuzisambaza katika maeneo ambayo tunafahamu yana shida ya ukame ili kuwezesha wakulima kuendelea kuzalisha kahawa kwa wingi."

Aidha amesema bado wanaendelea na majaribio ili kuweza kupata kahawa aina ya Robusta ambayo itavumilia ukame ili kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi katika uzalishaji wa zao hilo.

"Kwa sasa zipo aina 19 za kahawa ya Arabika na nne za Robusta ambazo zinazaa kwa wingi na zina uhimilivu dhidi ya magonjwa sugu ya kutu ya majani, chulebuni na mnyauko funzari. Sasa tumepata aina tatu za arabika zinazohimili ukame. Ni mafanikio makubwa" amesema Dk Maro.

Aidha Dk Maro ametumia nafasi hiyo kuwataka wakulima kujenga utamaduni wa kufahamu afya ya udongo kabla ya kufanya maamuzi yoyote katika shamba ili kuongeza ubora wa kahawa inayozalishwa nchini.

Akizungumza mtafiti wa usambazaji wa teknolojia TaCRI, Shelta Mseja amesema wamejipanga kuzalisha miche milioni tisa ya kahawa msimu wa 2024/2025, kwa lengo la kuisambaza ili kuongeza uzalishaji wa zao hilo hapa nchini.

"Bado mahitaji ya miche ya kahawa ni makubwa kuliko uzalishaji tunaofanya, hivyo bado tuna kazi kubwa ya kufanya ili kuhakikisha wakulima wanapata miche hiyo", amesema.

Amesema miche hiyo inazalishwa katika vituo vitano vya taasisi hiyo ambavyo viko Lyamungo (Kilimanjaro), Sirari (Mara), Mwayaya (Kigoma), Mbinga (Ruvuma)   na Maruku (Kagera).

Naye afisa ubora wa kahawa TaCRI, Herieth Oswald, amesema taasisi hiyo inaendelea kutoa elimu kwa wakulima wa kahawa kuhusiana na uongezaji wa thamani ya zao hilo hatua ambayo itawawezesha kujiongezea kipato.

“Pamoja na elimu tunayowapa wakulima ya kuzalishaji kahawa bora, pia tunaendelea kuwapa elimu ya jinsi ya kuongeza thamani ya kahawa wanayozalisha ili waweze kujiongezea kipato”, amesema Oswald.