Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Wakulima Rombo waomba Serikali kudhibiti pembejeo duni

Baadhi ya wakulima wa kahawa,  Wilaya ya Rombo wakiwa kwenye mkutano mkuu wa chama cha msingi cha Ushirika cha Tarakea, Wilaya ya Rombo. Picha na Janeth Joseph

Muktasari:

  • Wameiomba Serikali kudhibiti uuzwaji wa pembejeo duni, hasa viuatilifu visivyofaa kukabili kutu ya majani inayoshusha mavuno.

Rombo. Wakulima wa kahawa katika Wilaya ya Rombo, mkoani Kilimanjaro, wameiomba Serikali kuchukua hatua madhubuti kudhibiti uuzwaji wa pembejeo duni, wakisema hali hiyo imekuwa kikwazo kwa juhudi zao za kukabiliana na magonjwa ya mimea, hususan kutu ya majani.

Wamesema magonjwa hayo yanapunguza uzalishaji kwa kiasi kikubwa na kuwaathiri kiuchumi, kwani kahawa ni zao tegemeo kwa wengi wao.

Wakulima hao wametoa kilio hicho jana, Mei 2, 2025, wakati wa mkutano mkuu wa Chama cha Msingi cha Ushirika cha Tarakea, uliofanyika katika ukumbi wa chama hicho, ambapo walikutana na wataalamu wa kilimo pamoja na viongozi wa Serikali kutoka wilayani humo.

Wamesema baadhi ya maduka ya pembejeo huuza bidhaa zisizo na ubora, hususan viuatilifu vinavyoshindwa kuzuia au kutibu magonjwa ya kahawa, hali inayochangia kudorora kwa mavuno na kusababisha hasara kwa wakulima.

“Changamoto kubwa ni viuatilifu visivyo na ubora. Unanunua dawa ya kutu ya majani lakini haifanyi kazi. Majani huanza kupukutika na mmea hukauka kabisa. Hii inarudisha nyuma juhudi za mkulima na kusababisha hasara,” amesema Beda Tesha, mmoja wa wakulima hao.

Kwa upande wake, Edwina Tarimo ambaye ni mkulima, ameiomba Serikali kuingilia kati kwa kutoa suluhisho la haraka dhidi ya ugonjwa wa kutu ya majani.

“Tunaomba mwarobaini wa tatizo hili. Tumehangaika sana, hatuzalishi kwa tija. Tunahitaji dawa bora ili kilimo hiki kiwe na faida,” amesema.

Kwa upande wake, Anastazia John amesisitiza kuwa kahawa ni zao linalowakomboa wakazi wengi wa Rombo kiuchumi, hivyo ni muhimu kwa Serikali kuhakikisha pembejeo zinazopatikana sokoni zinakuwa na ubora unaotakiwa.


Serikali yatoa wito kwa wakulima

Akijibu hoja hizo, Ofisa Tarafa wa Tarakea, Ally Malekela, aliyemwakilisha Mkuu wa Wilaya ya Rombo, amewataka wakulima kuepuka kununua pembejeo kutoka kwa wauzaji holela.

“Maduka mengi yasiyo rasmi huuza bidhaa zisizokaguliwa. Ili kupata pembejeo bora, ni vyema wakulima wanunue kupitia vyama vya ushirika ambavyo vinasimamiwa na Serikali,” amesema Malekela.

Mkutano huo ulilenga kujadili changamoto za kilimo cha kahawa na kutoa mapendekezo ya maboresho ili kuongeza uzalishaji na mapato kwa wakulima.