Kweleakwelea wazua vilio kwa wakulima Mbarali, watalaamu waingilia kati

Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki Mbeya na Mjumbe wa Baraza la kutokomeza malaria nchini (EMCT), Gervas Nyaisonga akipuliza dawa katika moja ya dimbwi lenye vizalia vya mbu katika tarafa ya Kipembawe wilayani Chunya mkoani Mbeya.
Muktasari:
- Ndege hao wanatajwa kuishi katika maeneo ambayo ni vigumu kufikika na binadamu, hususan kandokando ya mito na kwenye miti yenye miiba, na huonekana kuvamia mashamba ya mpunga hasa kipindi cha kuelekea mavuno.
Mbeya. Wakati wakulima wa zao la mpunga wilayani Mbarali, mkoani Mbeya, wakijiandaa kwa msimu wa mavuno, taharuki imetanda kufuatia mashamba kuvamiwa na ndege aina ya kweleakwelea, hali inayowaweka wakulima katika mashaka na kuwafanya waombe msaada wa haraka kutoka serikalini ili kunusuru mazao yao.
Ndege hao wanadaiwa kuanza kuvamia mashamba hasa katika kipindi cha kuelekea mavuno, mpunga unapofikia hatua ya ukomavu, na kusababisha uharibifu mkubwa.
Baadhi ya wakulima wamelazimika kukesha mashambani kulinda mazao yao, huku wengine wakiajiri vibarua kwa ajili ya kuwasukuma ndege hao.
Wakizungumza na Mwananchi, baadhi ya wakulima wameeleza kuwa hali imezidi kuwa mbaya, kutokana na ongezeko la idadi ya ndege hao na kiwango kikubwa cha uharibifu kinachosababisha hasara kubwa kwao.

Mkulima David Mkeya (kulia) akionesha aina ya mpunga unaoharibiwa na ndege aina ya kwelea kwelea wakati wa operesheni ya Shirika la kudhibiti nzige wa Jangwani (DLCO). Pembeni wa kwanza ni Meneja wa Shirika hilo, Didas Moshi (aliyevaa kofia) walipotembelea shamba la mpunga la Kapunga wilayani Mbarali mkoani Mbeya.
Mkulima David Mkeya amesema licha ya uwekezaji mkubwa alioufanya katika shamba lake, kwa sasa anaona dalili za kutopata mavuno kutokana na uvamizi wa ndege hao ambao wameharibu sehemu kubwa ya mazao ya mpunga.
Ameeleza kuwa kwa sasa wanafarijika na msaada wanaoupata kutoka Shirika la Kudhibiti Nzige wa Jangwani (DLCO-EA) pamoja na Mamlaka ya Afya ya Mimea Tanzania (TPHPA), ambao wameweka kambi katika mashamba ya mpunga ya Kapunga kwa ajili ya kudhibiti hali hiyo.
"Hawa ndege hatujui wanatoka wapi, zaidi utawakuta shambani haswa kipindi hiki mpunga ukitengeneza maziwa (kukomaa), hali hii inatupa hofu katika mavuno kuweza kupungua licha ya gharama kubwa tulizoweka.
"Lakini, tuishukuru na kuipongeza Serikali kupitia Wizara ya Kilimo ambapo tumeona Shirika la DLCO EA na TPHPA wamefika haraka kuweka kambi kupambana na ndege hao, hii inatupa matumaini," amesema Mkeya.
Naye Shukuru Nzunda amesema kuwa ndege hao wamekuwa wakisababisha uharibifu mkubwa wa mazao, hali iliyowalazimu wakulima kuanza kukesha mashambani ili kulinda mazao yao dhidi ya mashambulizi.
Amesema licha ya changamoto hiyo, wamefarijika na hatua ya haraka iliyochukuliwa na Serikali kuwafikia kwa msaada, akieleza kuwa kipindi cha mavuno huwa na changamoto nyingi, zikiwemo za uvamizi wa ndege hao pamoja na wadudu wengine kama nzige, ambao husababisha hasara kubwa kwa wakulima.
"Tulilazimika kuajiri vibarua ili walinde maeneo yote ya mashamba, na mara nyingine tunakesha mashambani kwa kuwa ndege hao huvamia hasa nyakati za asubuhi na jioni. Tunamshukuru Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe, kwa hatua za haraka alizochukua," amesema Nzunda.

Kwa upande wake, Meneja wa Shirika la Kudhibiti Nzige wa Jangwani (DLCO-EA), Didas Moshi amesema changamoto hiyo ipo wazi, na baada ya kupokea taarifa kutoka kwa wakulima, waliamua kuweka kambi katika mashamba ya Kapunga na Madibira kwa lengo la kuwadhibiti ndege hao waharibifu.
Ameeleza kuwa changamoto kubwa inayosababisha ugumu katika udhibiti wa ndege hao ni uwezo wao wa kuruka kutoka nchi moja hadi nyingine.
Hata hivyo, amesema shirika hilo kwa kushirikiana na Mamlaka ya Afya ya Mimea Tanzania (TPHPA), limejipanga kikamilifu kukabiliana na wanyonyaji hao wa mazao.
"Tayari ndege yetu ya kudhibiti ndege hao ipo hapa Mbeya, ambapo tumeanza na Madibila na kisha tutaelekea Kapunga. Tunapambana na wadudu wahamao wanaovuka mipaka (Transboundary outbreak pests)," amesema Mushi.
"Ndege hawa aina ya kwelea kwelea wanaathiri zaidi mikoa 18 kati ya 26 zilizopo Tanzania, lakini shirika tayari limetengeneza mpango wa kukabiliana nao, na baada ya Mbeya tutakuwa mkoani Singida kutekeleza operesheni hiyo, amesema."
Mushi amefafanua kuwa shirika hilo linahusika na udhibiti wa ndege wahamao kwa kuvuka mipaka, ikiwa ni pamoja na Nzige, Kwelea kwelea, Viua Vijeshi, na Mbung'u, ambao hupatikana katika nchi tisa: Ethiopia, Sudan Kusini, Sudan, Uganda, Djibouti, Kenya, Somalia, na Tanzania.
Meneja wa Mamlaka ya Afya ya Mimea Kanda ya Nyanda za Juu Kusini (TPHPA), Pius Kawala amesema baada ya kufanya uchunguzi wa kina na kubaini mazalia na maeneo wanayoishi ndege hao, wameanza kutumia sumu maalumu iitwayo Kwelea Tox ili kuwadhibiti.
Amesema kuwa kwa sasa, serikali inaendelea kutafuta ndege za Tanzania kwa ajili ya kudhibiti ndege hao, ili kurahisisha operesheni hiyo, badala ya kutegemea ndege za kukodi kutoka Ethiopia.
"Kwa maana hiyo, wakulima na wananchi kwa ujumla waendelee kuiamini serikali. Tutashirikiana nao kwa karibu ili kuhakikisha wanafanya kazi zao kwa ubora na kuongeza mavuno," amesema Kawala.
Naye, rubani wa ndege kutoka Shirika la Kudhibiti Nzige wa Jangwani (DLCO EA), Eutychos Ruigu, amesema changamoto kubwa katika zoezi la kudhibiti ndege hao ni hali ya anga, akieleza kuwa kazi inayofanywa inategemea mwelekeo unaotolewa na TPHPA.
"Kazi inaendelea vizuri, tatizo kubwa ni hali ya anga. Hata hivyo, tunashukuru kwa maendeleo mazuri. Tunaanza kuwavamia maeneo wanayokaa, hasa asubuhi na jioni wakati wanapolala," amesema Ruigu.