Nyanda za juu kusini waja na mikakati ya uzalishaji kahawa

Mkuu wa Mkoa wa Songwe Daniel Chongolo akizungumza wakati wa kikao cha wadau wa kahawa mikoa ya nyanda ya juu kusini kilichofanyika wilayani Mbozi Jana Aprili 23,2025 picha na Denis Sinkonde
Muktasari:
- Moja ya mkakati ni kuzalisha tani 300,000 kwa mwaka 2025 pamoja na kukabiliana na changamoto zinazokwamisha uzalishaji wa kahawa zikiwamo uhaba wa mbegu za zao hilo, mabadiliko ya tabia nchi, wadudu na magonjwa.
Songwe. Mikoa ya Nyanda za juu kusini inatarajia kuongeza wigo wa uzalishaji wa zao la kahawa yenye ubora kwenye soko la dunia kwa kufikia tani 300,000 mwaka huu, ikiwa ni ongezeko la kutoka tani 65,235 za sasa.
Imeelezwa kuwa hilo litakuwa ongezeko la kihistoria ambalo halijawahi kutokea.
Hayo yamesemwa leo Aprili 24, 2025 na Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Daniel Chongolo kwenye uzinduzi wa kikao maalumu cha wadau wa kahawa, Kanda ya Nyanda za Juu.
Kikao hicho kinahusisha wadau kutoka mikoa ya Mbeya na Rukwa kikiwajumuisha viongozi wa mikoa, wilaya, wataalamu wa kilimo na wakulima.
Chongolo amesema uzalishaji wa zao la kahawa kwa mikoa ya nyanda za juu kusini huongezeka kila mwaka na mwaka 2023/2024 jumla ya kilo 17 milioni sawa na tani 17,169.8 na msimu wa mwaka 2024/2025 kilo zaidi ya milioni 20 sawa na tani 20,870 za kahawa ghafi, zilizalishwa huku wakulima 344 wakipatiwa mafunzo ya uzalishaji bora wa zao hilo.
Hivyo, Chongolo amesema wamejipanga kuongeza uzalishaji wa kahawa safi kutoka tani 65,235 za sasa na wafikie tani 300,000 ifikapo mwisho wa msimu wa mwaka huu.
Amesema hilo ni ongezeko la kihistoria linalolenga kuipa Tanzania nguvu mpya kwenye soko la dunia la kahawa.
“Mikakati ya kuongeza uzalishaji imejikita katika kuzalisha miche milioni tatu ya aina ya Combat Coffee, inayopandwa kwa kutumia mbegu badala ya vikonyo na ina uwezo wa kustahimili magonjwa hatari kama Coffee Berry Disease (CBD) na Coffee Leaf Rust (CLR),” amesema Chongolo.
Amesema pamoja na mikakati ya kuongeza uzalishaji wa zao hilo, watahakikisha wanakabiliana na changamoto zinazolikwamisha ikiwamo kushambuliwa na wadudu, magonjwa sambamba na mabadiliko ya tabianchi, uhaba wa mbegu bora ya kahawa na kusababisha uzalishaji hafifu.

Katika habari picha ni wadau wa kahawa Kanda ya nyanda za juu kusini wakiwa kwenye kikao Cha kujadili masuala mbalimbali ya uzalishaji wa zao hilo.picha na Denis Sinkonde
Akizungumza kando ya kikao hicho na Mwananchi, mkulima wa zao hilo, Emmanuel Siwale kutoka wilayani Mbozi, amesema licha ya kuweka mikakati ya uzalishaji wa kahawa, ameiomba Serikali kuangalia upya kodi wanazotozwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).
Amesema kama mfumo utafanyiwa marekebisho, utasaidia kuwaondolea wakulima utitiri wa kodi ataweza kuongeza mtaji kwa kuwa mzunguko wa biashara utarahisishwa.
“Hivi karibuni Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe alipiga marufuku wakulima kulipishwa kodi na TRA, namuomba na mkuu wetu wa mkoa wa Songwe, aweke msukumo katika jambo hili,” amesema Siwale.
Naye Hamis Mwasenga mkulima kutoka Mbozi amesema kikao hicho kihakikishe kinajadili namna nzuri ya kumwezesha kila mkulima ashiriki kikamilifu katika mnyororo mzima wa thamani ya kahawa.
“Nasema hivi kwa sababu mwelekeo wa pamoja wa kuibua fursa mpya, kuongeza ubora na thamani ya zao hilo muhimu kiuchumi unapaswa kumfikia kila mkulima,” amesema Mwasenga.