Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Ufanisi mdogo mashirika ya umma tatizo liko hapa

Moshi. Nini kinayakumba mashirika yetu ya umma? Ni swali linalogonga vichwa vya Watanzania, hasa wanaposikia hasara ya mabilioni ya shilingi, lakini Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), ametegua kitendawili hicho.

Katika ripoti kuu ya mwaka ya Ukaguzi wa Mashirika ya Umma kwa mwaka wa Fedha 2023/2024 ya Machi 2025 iliyokabidhiwa bungeni mjini Dodoma Aprili 16, 2025, CAG amebainisha changamoto kuu nne zinazoyatafuna mashirika hayo.

CAG kupitia ukaguzi huo anasema mashirika hayo ya umma bado yanakabiliwa na changamoto kama vile hasara zinazojirudia, ukata wa fedha, upungufu katika utawala bora, na ucheleweshaji katika utekelezaji wa mapendekezo ya ukaguzi.

CAG alikagua mashirika ya umma 217 na kutoa hati za ukaguzi ambapo kati ya hati 217 alizotoa, hati 213 zilikuwa zinaridhisha na 4 zilikuwa ni hati zenye shaka huku asilimia ya hati zinazoridhisha imeendelea kuwa asilimia 98 sawa na mwaka jana.


Hasara mtindo mmoja

Katika ukaguzi huo, CAG alikagua utendaji wa kifedha wa mashirika ya umma 217 na kulinganisha na mwaka wa fedha uliopita 2022/2023 na kubaini mashirika ya umma 12 yalipata hasara ya kifedha kwa miaka mitatu mfululizo. Katika ukaguzi huo, mashirika matano yalipata hasara kwa miaka miwili mfululizo, wakati mashirika mawili yalipata hasara kwa mwaka wa 2023/2024.

Hasara hizi kwa mujibu wa CAG, zinasababishwa na utendaji duni wa uwekezaji na shughuli za biashara, usimamizi usio mzuri wa matumizi ya fedha, pamoja na ukusanyaji mdogo wa mapato kutokana na mikakati isiyofaa ya kibiashara.

“Hali hii inaweza kusababisha kupungua kwa uwezo wa kugharamia shughuli muhimu na uwekezaji, na kutegemea kwa kiasi kikubwa ruzuku za Serikali ili kufidia upungufu wa kifedha,” anasema CAG katika ripoti yake hiyo.

Mathalan, CAG anasema katika ripoti hiyo ya ukaguzi kuwa Shirika la Reli Tanzania (TRC) lilirekodi ongezeko la hasara kwa asilimia 120, ikiongezeka kutoka Sh102 bilioni 102 mwaka 2022/2023 hadi kufikia Sh224 bilioni mwaka 2023/24.

Ongezeko hili kubwa lilichangiwa hasa na kupungua kwa mapato na kupanda kwa gharama za uendeshaji, licha ya kupokea ruzuku ya Serikali ya jumla ya Sh29.01 bilioni kutoka Serikalini kwa ajili ya uendeshaji na maendeleo ya shirika.

Shirika la Ndege Tanzania (ATCL), nalo liliendelea kurekodi hasara za kifedha kwa miaka sita mfululizo, licha ya kupokea ruzuku kutoka serikalini.

CAG anasema mwaka 2023/2024, ATCL ilipokea Sh70 kwa ajili ya mishahara ya wafanyakazi na gharama zingine za wafanyakazi, pamoja na Sh57 bilioni kama ruzuku ya maendeleo kwa miradi ya uwekezaji.

Hata hivyo, CAG amebaini kuwa licha ya msaada huu wa kifedha, hasara halisi ya ATCL iliongezeka kwa asilimia 62, ikipanda kutoka Sh56.6 bilioni mwaka 2022/23 hadi kufikia Sh91.8 bilioni mwaka 2023/24, huku hasara zikifikia Sh534 bilioni.

“Hali mbaya ya kifedha ilichangiwa hasa na gharama kubwa za kodi na matengenezo ya ndege mpya zilizonunuliwa, ambazo ziliongeza gharama kwa Kampuni,” anasema CAG na kufafanua athari za kuharibika kwa ndege.

CAG alisema kuharibika kwa ndege za Airbus A220-300 kutokana na kutu na hitilafu za injini zinazohusiana na mtengenezaji, ilisababisha upotevu wa mapato, na gharama zisizorejeshwa za bima, matengenezo, na gharama za wafanyakazi.

CAG ametoa mapendekezo kwa mashirika matatu yaliyoongoza kwa hasara huku akiishauri TRC lijikite katika kuoboresha ufanisi wa utendaji wake na ATCL likitakiwa kushirikiana na Serikali kutafiti njia nzuri ya kuliendesha shirika hilo.

Kwa Shirika la mawasiliano Tanzania, CAG amependekeza liboreshe ufanisi katika utendaji ili kuongeza ukusanyaji wa mapato na kuwasiliana na Serikali ili mapato yatokanayo na Mkongo wa Taifa yabaki katika shirika hilo.


Kuimarisha mashirika kibiashara

Katika tathmini yake, CAG alibaini TRC imeshindwa kufikia asilimia 61 ya mkakati wake wa usafirishaji wa shehena kwa wafanyabiashara wakubwa watano.

Pia Shirika hilo limeshindwa kutoa huduma za usafiri kwa abiria katika Mkoa wa Dar es Salaam kwa asilimia 72 kutokana na upungufu wa treni za kisasa zinazoendana na huduma hiyo.

Kwa upande wa ATCL, CAG alibaini tozo za ukodishaji wa ndege na akiba ya matengenezo kwa miaka sita mfululizo yenye jumla ya Sh369.13 bilioni ambazo hazijalipwa, na matengenezo yasiyo na tija kiasi cha Sh20.63 bilioni.

Matengenezo hayo ni ya Ndege-5H-MWF (Q300) ambayo ilikuwa haifanyi kazi, hadi kufikia Juni 30, 2024 na hii imesababisha ATCL kupata hasara kubwa ya kifedha ya Sh91.80 bilioni na kupunguza utendaji wake.

CAG alibaini miradi minne mikubwa, ambayo inahusisha ukarabati wa meli, ujenzi wa maeneo ya meli, na ujenzi wa gati katika Ziwa Tanganyika na Ziwa Victoria unaosimamiwa na kampuni ya Huduma za Meli Tanzania ulikuwa haujaanza.

Miradi hiyo ilikuwa na thamani ya Sh8.89 bilioni na Dola za Marekani milioni 251.07 ambazo ni karibu Sh652 milioni za Tanzania.


Upotevu wa mapato

Katika mashirika ya umma saba aliyoyakagua, alibaini yalipata hasara ya Sh966.42 milioni itokanayo na mapato yasiyotozwa kwa kiwango sahihi.

CAG pia alibaini utendaji duni wa Shirika la Madini la Taifa katika huduma ya uchimbaji, uliopelekea hasara ya mapato yaliyotarajiwa ya dola za Marekani milioni 15.52, sawa na Sh40.77 bilioni za Tanzania

Kwenye ukusanyaji wa mapato, CAG alibaini mapato yaliyokusanywa nje ya mfumo wa GePG Sh89.73 bilioni katika mashirika ya umma kumi, sawa na asilimia 4 kati ya mashirika ya umma 217 aliyoyafanyia ukaguzi kwa mwaka 2023/2024.

Kwa mujibu wa CAG, hilo ni ongezeko la Sh68.27 bilioni, sawa na asilimia 318 kutoka Sh21.46 bilioni zilizoripotiwa kwa mwaka wa fedha uliopita.

Pamoja na hayo, CAG alibaini mashirika ya umma 106 yana madai makubwa ya zaidi ya mwaka mmoja yanayofikia Sh3.58 trilioni yanayohusiana na huduma zilizotolewa kwa wateja.


Matumizi yasiyo na tija

Katika ukaguzi wa mashirika ya umma, CAG alibaini mashirika ya umma 12 yalifanya matumizi yasiyokuwa na tija ya jumla ya Sh371.42 bilioni.

Hilo kwa mujibu wa CAG ni ongezeko la asilimia 413 ikilinganishwa na Sh72.36 bilioni 72.36 katika mashirika ya umma 17 mwaka uliopita.

CAG alibaini pia kuwa mashirika 10 yalifanya matumizi yasiyostahili ya jumla ya Sh6.75 bilioni, ikiwa ni ongezeko la asilimia 45 ikilinganishwa na Sh4.64 bilioni katika mashirika ya umma 11 mwaka uliopita.

Pia alibaini kuwa mashirika 66 ya umma yalikuwa na madeni ya jumla ya Sh3.70 trilioni, ambayo yalikuwa hayajalipwa kwa zaidi ya miezi 12.


Utendaji wa benki

Katika ukaguzi huo, CAG alibaini kuwa benki tatu ambazo ni Benki ya Biashara Tanzania, Benki ya TIB Maendeleo na Benki ya Azania hazikusimamia ipasavyo mikopo iliyotolewa ya Sh558.53 bilioni.

Kwa mujibu wa CAG, mikopo hiyo ilijumuisha Sh104.84 bilioni kutoka Benki ya Biashara Tanzania wakati Sh277.07 bilioni ni kutoka benki ya Azania na Sh176.62 bilioni zilikuwa ni za Benki ya TIB Maendeleo.

“Dhamana zilizoahidiwa za mikopo hiyo ama hazikuwa zimekatiwa bima, au zilikuwa bandia au hazikuwepo,” anasema CAG na kuongeza kuwa;-

“Mapungufu katika usimamizi wa dhamana husababisha hatari ya mikopo kwa benki na wakopaji wanaweza kutorejesha mikopo hiyo.”

Halikadhalika CAG alibaini Benki ya Biashara Tanzania haikuweza kuendana na kiwango cha awali kilichowekwa na Benki Kuu ambapo ilikuwa na uwiano wa mtaji wa asilimia 13.41 ambao ni chini ya uwiano unaohitajika wa asilimia 14.5.

Katika ukaguzi huo, CAG alibaini kuwa Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii kwa Sekta Binafsi na Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma ina salio la mikopo isiyolipwa kwa muda mrefu inayofikia Sh3.57 trilioni.

Kati ya fedha hizo, Sh2.28 trilioni ni ya iliyokuwa PSPF zamani na inatarajiwa kulipwa na Serikali na Sh1.29 trilioni ni mkopo uliotolewa kwa Serikali kwa kipindi kinachotofautiana kati ya mwaka mmoja hadi miaka 17.

Mikopo hii isiyolipwa na Serikali imezuia uwezo wa mifuko ya pensheni kufanya uwekezaji zaidi, wakati Serikali hailipi riba ya mikopo na mifuko imesitisha kutoza riba.


Utekelezaji wa mapendekezo ya kaguzi

Katika ripoti hiyo ya mwaka wa Fedha 2023/2024, CAG anasema tathimini yake ya mapendekezo ya kaguzi zilizopita na maagizo ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali inaangazia uhitaji wa kuimarisha juhudi za utekelezaji.

Kati ya mapendekezo 6,749 yaliyotolewa kwa mashirika ya umma 217 katika miaka iliyopita, mapendekezo 2,589, sawa na asilimia 38 yalitekelezwa kikamilifu, huku mapendekezo 2,916, sawa na asilimia 43 yako katika hatua ya utekelezaji.

Kwa mujibu wa Mkaguzi na Mdhibiti mkuu wa Hesabu za Serikali, mapendekezo 1,012, sawa na asilimia 15 hayakutekelezwa, na mapendekezo 232 sawa na asilimia 3 yalipitwa na wakati kwa muktadha wa mabadiliko ya matukio.

Pia alisema kati ya maagizo 209 ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali yaliyotolewa kwa mashirika ya umma 53 katika mwaka wa 2023/24, maagizo 100 ambayo ni sawa na asilimia 48 yalitekelezwa kikamilifu.

Hata hivyo, maagizo 99, sawa na asilimia 47 yalikuwa katika hatua ya utekelezaji, na maagizo 10, sawa na asilimia 5 yalikuwa bado hayajatekelezwa.

CAG katika ripoti hiyo ambayo imewekwa wazi katika Tovuti ya Taifa ya Ukaguzi, anasema kuharakisha utekelezaji wa mapendekezo na maagizo ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ni muhimu katika kushughulikia changamoto zilizopo.