Sungusungu atupwa jela miaka minane kwa kuua bila kukusudia

Muktasari:
- Tukio hilo limetokea Juni 3, 2024, ambapo mshtakiwa akiwa Mtemi wa Sungusungu, kwa kushirikiana na wenzake wawili ambao bado hawajakamatwa, walimpiga na kumjeruhi vibaya Jumanne baada ya kufikishwa kwao kwa tuhuma za kumjeruhi mtu mwingine kwa panga.
Geita. Mahakama Kuu, Masjala Ndogo ya Geita, imemhukumu Majid Badru, Mtemi wa Sungusungu, kifungo cha miaka minane jela baada ya kukiri kumuua bila kukusudia Adil Jumanne, mkazi wa Mtakuja katika Mji Mdogo wa Katoro.
Hukumu hiyo imetolewa leo Ijumaa, Mei 2, 2025, na Jaji Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Calvin Mhina, ambaye amesema Mahakama imezingatia maelezo ya pande zote mbili pamoja na ushahidi wa ripoti ya daktari, ulioonyesha wazi kuwa kifo cha marehemu kilitokana na kipigo.
Katika kesi hiyo, Wakili wa Serikali, Robert Neophitus, ameiambia Mahakama kuwa Juni 3, 2024, mshtakiwa akiwa Mtemi wa Sungusungu wa Mtakuja, kwa kushirikiana na wenzake wawili ambao bado hawajakamatwa, walimpiga na kumjeruhi vibaya Jumanne baada ya kufikishwa kwao kwa tuhuma za kumjeruhi mtu mwingine kwa panga.
Baada ya kipigo hicho, Jumanne alipelekwa katika Kituo cha Polisi cha Katoro na baadaye Hospitali ya Mji Mwema kwa matibabu, ambako alifariki dunia.
Majid Badru amekiri kosa hilo mahakamani na kutiwa hatiani kwa kosa la kuua bila kukusudia, kinyume na Kifungu cha 195(1) na 198 cha Kanuni ya Adhabu, Sura ya 16 iliyofanyiwa marejeo mwaka 2022.
Awali, Wakili wa Serikali ameiomba Mahakama kutoa adhabu kali, akieleza kuwa marehemu alikuwa kijana tegemeo kwa familia yake na pia ni sehemu ya nguvu kazi ya Taifa.
Kwa upande wa utetezi, Wakili Doreen Narzis ameiomba Mahakama kupunguza adhabu kwa mteja wake, akieleza amekiri kosa, hajaisumbua Mahakama. Pia hana rekodi ya makosa ya nyuma na ni baba wa familia mwenye watoto wanaomtegemea.
Ameongeza kuwa tukio hilo lilitokea wakati mshtakiwa akitekeleza majukumu yake kama sungusungu.
Akisoma hukumu, Jaji Mhina amesema mshtakiwa hakupaswa kumpiga marehemu ambaye tayari alikuwa mikononi mwao, bali walipaswa kumfikisha polisi.
Amesema kitendo hicho ni cha kujichukulia sheria mkononi, hata kama hakikuwa na nia ya kuua, hivyo kingeweza kuepukika.
"Kumpiga mtu ambaye tayari yupo chini ya ulinzi ni matumizi mabaya ya madaraka. Hukumu hii iwe fundisho kwa wengine," amesema Jaji.
Ameongeza kuwa mshtakiwa ana haki ya kukata rufaa kama hataridhika na uamuzi huo.