Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Afikishwa mahakamani kwa madai ya kumuua mkewe

Muktasari:

  • Tukio hilo linadaiwa kutokea Machi 11, 2024, katika Kijiji cha Ilolangulu, ambapo washtakiwa kadhaa walihusishwa na mauaji ya mtu mmoja kwa kushirikiana kwa karibu. Kesi hiyo imeibua hisia kutokana na mazingira ya mauaji na namna yalivyotekelezwa, ikielezwa kuwa ni ya kikatili na isiyo ya kawaida.

Geita. Mkazi wa Kijiji cha Ilolangulu, Wilaya ya Mbogwe mkoani Geita, Samwel Lusaja (53) na mwenzake Masumbuko John (47), wamefikishwa katika Mahakama Kuu – Masjala Ndogo ya Geita, wakikabiliwa na tuhuma za mauaji ya Sophia Kaboja (60), ambaye anatajwa kuwa mke wa Samwel Lusaja.

Kesi hiyo namba 8275/2024, imewasilishwa mahakamani kwa ajili ya kusikilizwa kwa hoja za awali.

Washtakiwa wanakabiliwa na tuhuma za kutenda kosa la mauaji, kinyume na Kifungu cha 196 pamoja na Kifungu cha 197 cha Kanuni ya Adhabu, Sura ya 16 iliyofanyiwa marejeo mwaka 2022.

Wakili wa Serikali, Deodatha Doto ameieleza Mahakama kuwa tukio hilo lilitokea Machi 11, 2024, katika Kijiji cha Ilolangulu, ambapo washtakiwa wanadaiwa kushirikiana kumuua Kaboja kwa kumchoma kwa kisu na kumpiga kwa fimbo.

Kwa mujibu wa maelezo ya awali ya upande wa mashtaka, Kaboja alikuwa amelala na wajukuu zake wawili nyumbani kwake wakati Samwel Lusaja alipotokea usiku na kugonga mlango.

Baada ya Kaboja kufungua mlango, alishambuliwa na watuhumiwa kwa kutumia kisu na fimbo, kitendo kilichosababisha kifo chake.

Wakati wa tukio hilo, mjukuu wa marehemu, Silvester, alisikika akilia huku akiwaomba wahusika waache kumpiga bibi yake, lakini waliendelea na shambulio hilo.

Baada ya kushambuliwa, Kaboja aliachwa amelala chini huku hali yake ikiwa mahututi.

Asubuhi yake, mtoto wa marehemu, Rahel Samwel, alifika nyumbani na kuukuta mwili wa mama yake ukiwa umejaa damu.

Alitoa taarifa kwa majirani na kuuarifu uongozi wa kijiji, ambao waliwasiliana na vyombo vya usalama.

Ripoti ya uchunguzi wa mwili wa marehemu imebaini kuwa chanzo cha kifo kilikuwa ni kuvuja damu nyingi kutokana na majeraha aliyopata katika shambulio.

Washtakiwa wote wamekana kutenda kosa hilo, na kesi hiyo imeahirishwa hadi itakapopangiwa tarehe rasmi ya kusikilizwa.

Kwa mujibu wa upande wa Jamhuri, kesi hiyo inatarajiwa kuwasilishwa kwa ushahidi kutoka kwa mashahidi 17 na vielelezo vitano.

Kila mshtakiwa anatarajiwa kuwasilisha shahidi mmoja kwa ajili ya utetezi wao.

Wakati huohuo, Frank Deus, mkazi wa Chato, amefikishwa katika Mahakama Kuu – Masjala Ndogo ya Geita kwa tuhuma za kumuua Makenz Said, ambaye pia ni mkazi wa Chato.

Kesi hiyo, namba 8274 ya mwaka 2025, inamkabili Deus kwa kosa la mauaji ya kukusudia, kinyume na Kifungu cha 196 na 197 cha Kanuni ya Adhabu, Sura ya 16 iliyofanyiwa marejeo mwaka 2022.

Kwa mujibu wa maelezo ya mwendesha mashtaka, Julai 26, 2024, Frank Deus alikwenda kwa mganga wa kienyeji kwa ajili ya matibabu.

Amedai kuwa usiku wa Julai 27, 2024 Deus aliingia katika chumba alicholala Makenz Said na kumtuhumu kuwa ameiba pesa zake.

Inadaiwa kuwa, Makenz Said akiwa na ndugu yake, Emanuel Said, ambaye alikuwa kama mwangalizi wa mgonjwa, walianza kushambuliwa na Deus.

Emanuel alikimbia haraka na kutoka nje, huku akimuacha Makenz akipigwa kwa fimbo.

Wakati watu walipofika eneo la tukio, walimkuta Makenz tayari amefariki dunia.

Tukio hilo liliripotiwa kwa vyombo vya polisi, ambapo mshtakiwa alikiri kutenda kosa hilo wakati wa mahojiano.

Hata hivyo, mshtakiwa amekana kutenda kosa hilo mahakamani, na kesi hiyo imeahirishwa hadi itakapopangiwa tarehe ya kusikilizwa.

Upande wa mashtaka umewasilisha mashahidi saba na vielelezo vitatu, ambavyo ni: ripoti ya uchunguzi, ramani ya eneo la tukio, na maelezo ya onyo ya mshtakiwa.