Sintofahamu kuondolewa Katibu Mkuu EAC, ateuliwa kuwa Balozi

Muktasari:
- Taarifa kutoka Nairobi zinasema Serikali ya Kenya imependekeza Caroline Mwende Mueke kuchukua nafasi ya Dk Mathuki kwa miaka miwili iliyobaki ya utumishi katika sekretarieti ya EAC.
Arusha. Hali ya sintofahamu imetanda katika makao makuu ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), kutokana na ripoti kwamba Katibu Mkuu wake ameondolewa kwenye nafasi hiyo hivi karibuni.
Dkt Peter Mathuki (raia wa Kenya), kwa mujibu wa vyombo vya habari vya Kenya, ameteuliwa kuwa Balozi wa Kenya nchini Russia na Rais William Ruto.
Iwapo uteuzi wake utathibitishwa, atakuwa Katibu Mkuu wa kwanza wa EAC kuondoka katika wadhifa huo kabla ya kumaliza muda wake wa miaka mitano.
Dk Mathuki aliteuliwa kuwa Katibu Mkuu wa EAC Februari 27, 2021 wakati wa mkutano wa kwanza wa wakuu wa nchi uliofanyika kwa njia ya mtandao kwa sababu ya mlipuko wa Uviko-19.
Katibu Mkuu si tu kiongozi wa sekretarieti ya EAC, chombo cha utendaji cha Jumuiya, lakini pia ni ofisa mkuu wa hesabu wa chombo hicho cha kikanda.
Pia, ni katibu wa mkutano wa wakuu wa nchi na mjumbe wa zamani wa Bunge la Afrika Mashariki (Eala).
Kwa mujibu wa mkataba wa EAC, katibu mkuu anateuliwa na wakuu wa nchi na atahudumu kwa muda wa miaka mitano ambayo hauwezi kuongezwa.
Vuguvugu la kuondolewa kwa Dk Mathuki kabla ya uteuzi mpya kutangazwa na Ikulu ya Rais wa Kenya, William Ruto, lilianzia kwenye kikao cha Bunge la Afrika Mashariki (Eala) kinachoendelea jijini Nairobi.
Bunge hilo lilikuwa linajadili matumizi ya Dola milioni sita za Marekani ambazo zinadaiwa kutumika bila kupitia utaratibu wa kawaida wa kuidhinishwa na Bunge hilo.
Dk Mathuki amefanya kazi katika taasisi mbalimbali za Afrika Mashariki kabla ya kuteuliwa kuwa bosi wa EAC na baadaye kupitishwa wakati wa utawala wa Rais Uhuru Kenyatta.
Alichaguliwa kuwa bosi wa EAC alipokuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Baraza la Biashara la Afrika Mashariki (EABC), jukwaa la biashara la kanda lenye hadhi ya uangalizi katika EAC.
Lakini ilikuwa katika kipindi chake cha miaka mitano (2012-2017) kama mbunge wa Eala, ambapo Dk Mathuki alijulikana zaidi katika masuala ya kikanda.
Wakati fulani, alikuwa mwenyekiti wa kamati ya Eala yenye nguvu ya Sheria, kanuni na haki iliyoongoza kuondolewa kwa Spika wa Eala wakati huo, Margaret Ssentongo Zziwa (2012-2014).
Kabla ya kuwa mbunge wa jumuiya hiyo, alifanya kazi kwa muda mfupi katika mradi ulio chini ya Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Afrika Mashariki (EATUC) lenye makao yake makuu jijini Arusha.
Uteuzi wake wa kuwa balozi unakuja takriban miaka mitatu baada ya kushika hatamu za uongozi katika sekretarieti ya EAC akichukua nafasi ya Liberat Mfumukeko wa Burundi.
Kwa mujibu wa itifaki ya EAC, mkuu wa nchi anayestahili, anamteua mtu wa kujaza nafasi hiyo ambaye anapitishwa na mkutano wa wakuu wa nchi.
Wadhifa huo kwa kawaida huwa wa mzunguko miongoni mwa nchi wanachama na wanaoteuliwa huhudumu kwa miaka mitano.
Taarifa kutoka Nairobi zinasema Serikali ya Kenya imependekeza Caroline Mwende Mueke kuchukua nafasi ya Dk Mathuki kwa miaka miwili iliyosalia ya utumishi katika sekretarieti ya EAC.
Mtaalamu huyo wa sera za umma amefanya kazi katika mashirika na misheni mbalimbali ya Umoja wa Mataifa, ikiwa ni pamoja na Unesco, Mpango wa Maendeleo wa Umoja wa Mataifa (UNDP) na Misheni ya Kulinda Amani ya Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini.
Uteuzi wake utalazimika kuidhinishwa na wakuu wa nchi katika mkutano mkuu. Dk Mathuki ni Mkenya wa pili kukalia kiti cha Katibu Mkuu wa EAC baada ya Francis Muthaura (1996 – 2001).
Kuteuliwa kwa Dk Mathuki kuwa Balozi wa Kenya nchini Russia kuliwashtua wafanyakazi wengi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, kwani hii ilikuwa ni mara ya kwanza kwa bosi huyo wa jumuiya hiyo kung’atuka kabla ya kufika mwisho wa muda wake.
Makatibu wakuu waliotangulia walikuwa Francis Muthaura (1996-2001), Nuwe Amanya Mushega (2001-2006), Juma Mwapachu (2006-2011), Richard Sezibera (2011-2016) na Liberat Mfumukeko (2016-2021).
Uteuzi wa Dk Mathuki kuwa balozi umekuja wakati ambao kuna uwezekano wa kushtakiwa kwa tuhuma za ubadhirifu wa fedha katika sekretarieti hiyo.
Kisa hicho kilizuka wakati wa mjadala kuhusu hotuba ya Rais Ruto, aliyoitoa Jumatano ya wiki iliyopita wakati wa kikao cha uzinduzi wa Eala, jijini Nairobi.
Ripoti zilizonukuliwa kwenye tovuti ya The East African zilitaja wasiwasi kuhusu matumizi ya zaidi ya Dola milioni sita za Marekani bila idhini ya Bunge.
Suala hilo liliibuliwa na Dennis Namara, mbunge wa Eala kutoka Uganda na mwenyekiti wa kamati ndogo ya fedha.
Alisema kushindwa kupata kibali cha Bunge kuhusu matumizi hayo ni ukiukwaji wa wazi wa sheria za fedha zinazosimamia mkataba wa kuanzishwa kwa EAC.
Taarifa kwenye tovuti ya The East African zilisema zaidi kwamba Dk Mathuki, alikuwepo kwenye Bunge hilo, lakini hakuzungumzia tuhuma zinazomkabili.