Somalia kuwa mwanachama wa nane kujiunga na EAC

Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika ya Mashariki (EAC), Dk Peter Mathuki Akizungumza na waandishi wa habari leo Januari 25, 2023.

Muktasari:

  • Maombi ya Taifa la Somalia kujiunga na Jumuiya ya Afrika ya Mashariki (EAC) yameanza kufanyiwa kazi baada ya Sekretarieti ya EAC kutuma  timu yake ya wataalamu kwenda nchini humo kukutana na maofisa wa Serikali ya nchi hiyo.

Arusha. Maombi ya Taifa la Somalia kujiunga na Jumuiya ya Afrika ya Mashariki (EAC) yameanza kufanyiwa kazi baada ya Sekretarieti ya EAC kutuma  timu yake ya wataalamu kwenda nchini humo kukutana na maofisa wa Serikali ya nchi hiyo.

Watalaam hao wa EAC wanatarajiwa kuanza kufanya uhakiki wa utayari wa  maombi ya Somalia kujiunga na Jumuiya ya Afrika ya Mashariki.
Kama Somalia ikikamilisha taratibu za kisheria kujiunga na EAC, itakuwa ni nchi ya nane kuwa mwanachama wa EAC nchi nyingine wanachama ni Tanzania, Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi, Sudani Kusini na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Januari  25, 2023  makao makuu ya EAC jijini Arusha, Katibu Mkuu wa Jumuiya hiyo, Dk Peter Mathuki amesema  timu hiyo ya wataalamu tayari imefika  Somalia na imeanza kazi.
"Baada ya kukutana pamoja wataandaa  ripoti na kuipeleka Baraza la Mawaziri wa  EAC wanaotarajia kukutana Februari 23 mwaka huu na kisha kupelekwa ripoti hiyo kwenye mkutano wa wakuu wa nchi utakaofanyika Februari 25 kwa ajili ya hatua zinazofuata," amesema.
Somalia kwa muda mrefu imekuwa ikiomba kujiunga na Jumuiya ya Afrika ya Mashariki na katika kikao cha mwisho cha wakuu wa nchi kilichofanyika jijini Arusha, Rais wa nchi hiyo Hassan Sheikh Mohamud alishiriki kama mgeni mwalikwa.