Prime
Sintofahamu kuadimika vipimo vya VVU

Unguja. Wakati vijana wakihamasika kupima Virusi vya Ukimwi, baadhi ya vituo vya afya vya Serikali havina vifaa vya kupimia maambukizi hayo hali inayorudisha nyuma jitihada za kupambana na ugonjwa huo.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti katika ziara iliyofanywa na Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania, Zanzibar (Tamwa-ZNZ), watoa huduma za afya katika vituo mbalimbali vya Wilaya ya Magharibi B na Wilaya ya Kati Unguja, walisema waathirika wa upungufu huo ni vijana ambao wameonyesha mwitikio kujua afya zao.
Wataalamu hao kutoka Kituo cha Afya Fuoni, Tunguu, Suza, Mwera, Magirisi walieleza wananchi hasa vijana wamehamasika kupima VVU na hufika kwa wingi kupata huduma hiyo, lakini kutokana na uhaba wa vipimo hivyo huduma hiyo haipatikani kwa sasa.
Daktari Kiongozi wa Kituo cha Afya Fuoni, Sultani Shela alisema tatizo hilo lina zaidi ya miezi miwili sasa, vifaa havipatikani katika vituo vya huduma rafiki kwa vijana na kwenye vituo vya afya, hali inayowalazimu wateja kwenda katika hospitali binafsi ambapo huduma hiyo hutolewa kwa malipo.
Alisema kwa sasa huduma hiyo inapatikana kwa wajawazito pekee kituoni hapo kwa sababu vifaa walivyonavyo ni vichache.
Alisema wajawazito hulazimika kujua afya zao ili kuwakinga wao na watoto dhidi ya maambukizi ya VVU.
“Kwenye vituo vyote vya Serikali huduma ya upimaji wa VVU ni bure na ndiyo maana wananchi hufika kwa wingi kwa ajili ya kujua afya zao,” alisema Khadija Ali Khamis wa kituo cha huduma rafiki kwa vijana Mwera.
Akizungumzia kadhia hiyo, Waziri wa Afya Zanzibar, Nassor Ahmed Mazrui, alikiri uwepo wa uhaba wa vifaa hivyo na kwamba tatizo hilo limetokana na kuchelewa kufika kontena lenye vifaa hivyo ambavyo hutoka nje ya nchi.
Hata hivyo, alisema tayari kontena hilo imeshafika na vitaanza kusambazwa katika vituo vyote vya afya vya Serikali kuanzia Septemba 4 ili kuendelea kutoa huduma hiyo.
Alisema Serikali inapata msaada wa vifaa hivyo kutoka Global Fund na vifaa vilivyofika vitakidhi mahitaji kwa muda wa mwaka mmoja.
Waziri Mazrui aliwataka wananchi kuendelea kuvitumia vituo vya afya na vituo vya huduma rafiki kwa vijana kupata huduma mbalimbali za kiafya, ikiwemo uchunguzi wa VVU, ambao maambukizi yake kwa sasa yapo katika makundi maalumu hasa vijana wanaotumia dawa za kulevya na wanaofanya biashara ya ngono.
Ziara hiyo ya waandishi wa habari imeandaliwa na (Tamwa-ZNZ) kupitia mradi wa kuendeleza utetezi wa afya ya uzazi kwa wanawake na wasichana mjini na vijijini kwa ufadhili wa Wellspring Philanthropic Fund (WPF) kutoka Marekani.