Takwimu VVU: Kwa nini wasichana ni vinara kwa maambukizi

Dodoma. Wakati Shirika la Afya Duniani (WHO) likitoa takwimu za wanaoishi na virusi vya Ukimwi (VVU) kufikia milioni 38.4 mwaka 2021 kutoka watu milioni 30.8 mwaka 2010, waathirika zaidi wa VVU wameendelea kuwa wanawake, hasa wasichana.
Kwa mujibu wa ripoti ya Programu ya Umoja wa Mataifa ya Ukimwi (Unaid) ya mwaka 2021, kila baada ya dakika mbili duniani, msichana mmoja anapata maambukizi ya VVU.
Ripoti hiyo inaonyesha kila siku watu 4,000 wanapata maambukizi na kati yao 1,100 ni kundi la vijana.
Inaelezwa katika ripoti hiyo endapo mwenendo wa maambukizi mapya ukiendelea kama ulivyo, huenda hadi kufikia mwaka 2025 watu wengi zaidi wakawa na maambukizi mapya.
“Kama mwenendo ukiwa hivi, maambukizi mapya yanatarajia kuwa milioni 1.2 mwaka 2025 badala ya 370,000 kama ilivyotabiriwa awali,” sehemu ya ripoti hiyo inasema.
Takwimu za Tanzania kwa vijana
Kwa Tanzania, kwa mujibu wa ripoti ya ‘Utafiti wa matokeo ya Ukimwi Tanzania 2016-2017’ maambukizi ya VVU yanapungua kadiri ya ngazi ya elimu ya vijana ilivyo (kutoka shule ya msingi hadi sekondari). Takwimu zinaonyesha kuwa Tanzania ina waathirika wa VVU takribani milioni 1.4
Pia, ripoti hiyo inawataja wasichana kuwa na maambukizi ya VVU kwa kiwango kikubwa ikilinganishwa na wavulana.
“Maambukizi ya Ukimwi kwa vijana wasio na elimu ni asilimia 6.1, huku wenye elimu wakiwa na asilimia 0.5.
Mchanganuo wake ni wasio na elimu kabisa (asilimia 6.1), wenye elimu ya msingi (asilimia 5.5) na waliosoma hadi kidato cha nne (asilimia 2.7), Kaimu Mkurugenzi Idara ya Mwitikio wa Kitaifa wa Tume ya Taifa ya Ukimwi (Tacaids), Audrey Njelekela anasema na kuongeza:
“Wasichana wasio na elimu kiwango cha maambukizi ni asilimia 6.7, wenye elimu ya msingi (asilimia 7.2) na waliomaliza kidato cha nne (asilimia 3.6)., huku kwa upande wa wavulana ni asilimia tano, asilimia 3.7 na asilimia mbili mtawalia.”
Mkakati wa kuwafikia vijana
Njelekela anasema kutokana na takwimu kubainisha kuwa waathirika zaidi wa Ukimwi kwa kundi la vijana nchini ni wasichana, mikakati mbalimbali inatekelezwa kwa ajili ya kupunguza maambukizi hayo.
“Kwa kuwa maambukzi mapya yapo kwa kiasi kikubwa kwa vijana wa miaka 10 hadi 24 na zaidi wa miaka 15 hadi 25 na hususani kwa vijana wa kike, mpaka sasa tuna mradi wa kuwafikia unaoitwa ‘Timiza malengo’ kwa ajili ya kulifikia kundi hili,” anasema.
Mradi huo unaotimizwa katika mikoa mitano ya Dodoma, Morogoro, Singida, Geita, Tanga pamoja na halmashauri 18 zenye maambukizi makubwa kwa kundi rika hilo, umefanikiwa kuzifikia shule zote za msingi na sekondari za binafisi na umma.
“Kupitia mradi huu tunawapa mabinti elimu ya afya ya uzazi, kutumia kondomu kwa usahihi kwa sababu hawatapata mimba wala magonjwa na lengo kuu la mradi huu ni kuwafanya mabinti waweze kubaki shuleni na kutimiza malengo yao,” anasema Njelekela.
Hamida (sio jina lake halisi), mwanafunzi wa kidato cha tatu katika shule moja jijini Dodoma anakiri kuwa wapo wasichana waliopo shule wapo hatarini kupata maambukizi ya VVU kutokana na vishawishi na kutokuwa na fedha.
“Sisi tunaosoma mazingira ya mjini tunakutana na vishawishi vingi kwa wauza chipsi na dereva bodaboda, ukiwa na tamaa utajikuta unaingia kwenye matatizo ya maambukizi hayo,” anasema.
Njelekela anasema mradi huo wenye lengo la kutimiza afua hizo kitabibu, kitabia na kimuundo kwa awamu ya kwanza ya utekelezaji wake wasichana wasiokuwa shuleni walipewa Sh400,000 kwa mwezi na walio shule Sh25,000 kwa mwezi ili kujikimu kiuchumi.
Katika awamu ya pili wameamua kujikita zaidi kwenye elimu na kutoa taulo za kike badala ya fedha. “Pia tuna mradi unaitwa ‘Dream’ unadhaminiwa na Pepfar (Mpango wa Dharura wa Rais wa Marekani wa Kukabiliana na Ukimwi) na wenyewe unawafikia walengwa walio ndani ya shule na nje ya shule katika afua hizo jumuishi nilizozitaja, mradi huu unapatikana katika mikoa ya Songwe, Iringa, Shinyanga, Mwanza na Kagera,” anasema.
Imeandikwa kwa udhamini wa Bill & Melinda Gates Foundation