Asilimia 3.4 ya watu wenye VVU hawajafikiwa Mtwara

Mtwara. Watu 3,890 wanaoishi na Virusi vya Ukimwi mkoani Mtwara wanatajwa kuacha matumizi ya dawa za kufubaza Virusi vya Ukimwi.
Akizungumza katika kikao kazi cha viongozi wa mkoa, viongozi wakuu wa dini na wadau kutoka shirika la USAID Afya Yangu Kanda ya Kusini, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Hamad Nyembea alisema kuwa zaidi ya watu 43,038 wanakadiriwa kuwa na maambukizi mkoani humo.
Hata hivyo amekiri kuwa hadi sasa, asilimia 3.4 ya watu wenye maambukizi hawajafikiwa na kwamba pia hawajatambua hali zao, huku wengi wakiwa ni wanaume, vijana na watoto wenye umri (15-24).
“Tuna mkakati wa Tisini na tano (asilimia 95) tatu, ili hadi kufikia mwaka 2025, kuwe na asilimia 95 ya watu wanaoishi na VVU wenye kujua hali zao za maambukizi, sambamba na waliopima kwa asilimia 95, huku wale wenye kugundulika kuwa wanaishi na VVU, wawe wanatumia dawa za ARV kwa asilimia 95," amesema na kuongeza;
"Lakini pia tunaendelea kushirikisha mashirika ya kidini kusaidia kuhusu utoaji elimu juu ya VVU na Ukimwi katika kushughulikia imani potofu juu ya upimaji wa VVU, kuanza ARV mapema, huduma za TB, kupunguza unyanyapaa na kuzuia unyanyasaji wa kijinsia," alisema Dr Nyembea.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Kanal Ahmed Abbas amesema kuwa wadau hao wamekutana ili kuweka mikakati bora itakayo ongeza hamasa ya kutolewa elimu katika masuala ya Ukimwi na Kifua Kikuu (TB) mkoani Mtwara.
"Yaani ni kama vile tumesahau uwepo wa magonjwa ya Ukimwi na TB, tumekuwa hatutoi kipaumbele kwa magonjwa hayo na kuna magonjwa yamekuja katikati tunaona ndio yenye athari kubwa. Kuwa walioambukizwa tumesahau kuwapatia huduma na tumesahau kuwafatilia,” amesema.
"Tumekaa na kuona kuna umuhimu wa kuendeleza mapambano na mikakati mbalimbali tukishirikiana na wadau wakiwemo mashirika yasiyokuwa ya kiserikali na mashirika ya dini ili kwa pamoja kama mkoa tuweze kufikia malengo ya 95-95-95" katika mwitikio wa Ukimwi amesema Kanali Abbas
Kwa upande wake Meneja wa Mkoa wa mradi wa USAID Afya Yangu Kanda ya Kusini Itros Sanga amesema kuwa vijana kuanzia miaka 15-24 wako kwenye hatari zaidi na ndio makundi yanaoongoza kwa nchini kupata maambukizi.
"Unajua ugonjwa wa Ukimwi na TB yana ukaribu kwakuwa ukiwa na TB kinga inashuka na kusabisha kuwa na uwezekano mdogo wa kuzuia maambukizi ya VVU,” amesema na kuongeza;
"Tunataka kuhakikisha kuwa vituo vinatoa huduma bora na kuhakikisha kuwa jamii pia inaunganishwa na kupata huduma hizi bora ambapo tunaamini kuwa yeyote anaeishi na VVU anatambua hali yake anaetambua aweze kutumia dawa na anaetumia aweze kuwa na VVU vilivyofubaa ili aishi na virusi ambavyo hatoweza kumuambukiza mtu" alisema Sanga.