Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Simulizi ya saa tatu za mshikemshike kuzuka moto MCL

Maofisa wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji pamoja na wa Kampuni ya ulinzi ya SGA wakiwa katika harakati za kuudhibiti moto uliozuka kwenye stoo zilizopo jengo la uchapaji wa magazeti MCL.

Dar es Salaam. “Nilipofika nje, nilishangaa kuwaona niliowaacha ndani tayari wako nje.”

Ni maneno ya Kulwa Magwa, msanifu mkuu wa gazeti la Mwanaspoti akielezea saa tatu za mshikemshike wa tukio la ajali ya moto, lililotokea katika ghala la kiwanda cha kuchapisha magazeti cha Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL), Tabata relini jijini Dar es Salaam.

Magwa ni miongoni mwa wafanyakazi kadhaa walioshuhudia tukio hilo wakiwa kazini, lililotokea saa 1 usiku muda ambao aghalabu wengine huwa tayari wameshaondoka.

Tukio hilo lililotokea Agosti 29, mwaka huu katika chumba cha kuhifadhia vifaa mbalimbali vya MCL, kulingana na tathmini iliyofanyika limesababisha hasara ya zaidi ya Sh940 milioni. Hata hivyo, ukaguzi na tathimini zaidi bado inaendelea mpaka sasa.

Mbio za kutoka ndani ya ofisi kukimbilia kusikojulikana, sintofahamu ya kipi kinapaswa kuanza kuokolewa na mayowe ni miongoni mwa yaliyoshuhudiwa na kusikika wakati wa tukio hilo.

Milio ya ving’ora kwa takriban dakika tano, haikutosha kuwastua baadhi ya wafanyakazi juu ya tukio hilo, wengi walidhani vinajaribiwa, lakini uliposhuhudiwa moshi kila mmoja aliusaka mlango.

Chumba cha uzalishaji magazeti shughuli zilikuwa zikiendelea katika hatua za mwishomwisho na kutokana na kuwahi muda, sauti ya ‘kuna moto kiwandani…tokeni ndani hazikusikika vilivyo’ hadi kengele ilipogongwa kuwashtua kuwa kuna tukio la moto.

“Nikiwa ofisini kwangu niliona moshi mzito unapanda juu, nilishtuka na sikujua kitu cha kufanya, baadaye nilipata akili ya kushuka chini kumueleza msimamizi wa uchapaji kuwa kuna moto," anasimulia Aliamini Adam mkuu wa kitengo cha picha katika kiwanda cha uchapishaji magazeti.

Anasema tukio hilo lilitokea wakati akisubiri kianze kipindi cha pili cha mchezo wa mpira wa miguu kati ya Klabu ya Yanga na JKT, aliokuwa anafuatilia kwenye runinga.

Kabla ya mapumziko, anasema vilianza kusikika ving’ora vya tahadhari kwa dakika tano, lakini hawakuhofu wakidhani ni kawaida kwani vimekuwa vikijaribiwa au wakati mwingine vinapiga kelele kwa sababu ya vumbi.

“Lakini nilipoona huu moshi nikasema si wa kawaida, ndipo nilipoamua kushuka chini kuona ni nini kinaendelea nikiwa kwenye ngazi nikaona moshi unatokea stoo ya kuhifadhia vifaa.

"Na laiti ukuta wa hili jengo usingekuwa mgumu nafikiri mimi ningekuwa wa kwanza kufa na hakuna ambaye angejua kama nilikuwa ndani kutokana na moshi mzito uliokuwepo,” anaongeza Adam.

Baada ya kutoa taarifa kwa msimamizi wa uchapaji, Adam anasema vijana waliokuwepo walishirikiana kuvunja mlango kwa kupokezana hadi walipofanikiwa.

“Walijaribu kuvunja kufuri kwa kutumia nyundo na machuma huku wengine wakiwa wameshika mitungi ya kuzimia moto ili mlango utakapofunguka waanze kuuzima,” anasema.

Wakati hayo yanaendelea, tayari taarifa za tukio hilo zilishasambazwa katika makundi ya mtandao wa WhatsApp ya wafanyakazi wa MCL, na juhudi za kuusaka msaada wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji na kampuni binafsi zilianza.

Licha ya gari la zimamoto la kampuni ya SGA kufika eneo la tukio saa 2:07 usiku, ilikuwa vigumu kuingia ndani kwa kuwa, askari wake hawakuwa na vifaa vya kuzuia moshi.

Dakika kumi baadaye gari la Jeshi la zimamoto na uokoaji lilifika katika eneo hilo na juhudi za kuzima zilianza kwa kushirikiana na wafanyakazi.

Hali ilivyokuwa

Ni tamu kusimuliwa, lakini chungu ikikutokea, ndivyo unavyoweza kusema kuakisi hali ya baadhi ya wafanyakazi waliokuwepo katika eneo la tukio, hasa wale waliokuwa na magari mawili katika eneo la maegesho.

“Nilipotoka nilimpa Rama funguo anisaidie kutoa gari moja, sasa sijui ilikuwa ni kuchanganyikiwa badala ya kwenda mbele akawa anarudi nyuma, ikabidi nimtoe nitafute mtu mwingine anayeweza kunisaidia,” anasema Joseph Damas, Mhariri Mtendaji wa gazeti la Mwananchi.

Katika siku hiyo, hakuna aliyejali hadhi ya mavazi aliyovaa, hata wenye tai walikimbia mithiri ya wanariadha na balaa zaidi lilishuhudiwa kwa wale wenye vitambi.

“Mimi niliposikia kengele nilidhani kikao cha wahariri, kumbe moto, muda huo nilikuwa nawaza mpira, tulikuwa tunasubiri kipindi cha pili cha mechi ya Yanga na JKT,” anasema Charles Abel mwandishi wa gazeti la Mwananchi na Mwanaspoti.

Kwa Salome Gregory anayeandikia gazeti la The Citizen, hakufikiria milango ya kawaida kujinusuru, tukio hilo lilimkumbusha kuisaka milango ya dharura ambayo hata hivyo alishindwa kuitumia kwa kutojua funguo zilipo.

“Naujua mlango mmoja wa dharura lakini niliwaza funguo yake inakaa wapi ili nitoke nikakosa jibu,” anasema.

Ilikuwa vigumu kuamini kwa Mhariri wa habari msaidizi wa gazeti la Mwananchi, Ibrahimu Yamola alipopigiwa simu na Samuel Kamndaya, Mhariri wa Habari wa gazeti la The Citizen.

“Kaka…tokeni nje kuna moto unawaka huku kiwandani,” anasimulia Yamola vile alivyopokea maelezo na kuamua kutoka ndani kwenda kujionea

“Nilipofungua tu mlango, niliona moshi mwingi kutokea kiwandani, nikarejea ndani kuwaambia wezangu kuna moto, walidhani ni masihara, nikaamua kugonga kengele ambayo huwa tunaitumia kuitana kukiwa na jambo au kikao, kila mmoja akataka kufahamu kuna nini nikawajuza kuhusu moto unaowaka kiwandani, hapo purukushani sasa zikaanza za kila mmoja kutafuta pa kutokea,” anasema Yamola


Taarifa zilivyofika

Kwa kuwa ni wafanyakazi wachache ndiyo waliokuwepo ofisini, baada ya taarifa hizo walilazimika kurudi kama anavyoeleza Meneja wa Kitengo cha uzalishaji, Vespery Michael “Nikiwa njiani nilidhani ni stoo ndogo nikawa najaribu kuwapigia Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) wakate umeme lakini sikufanikiwa. Nilipofika nilijaribu kutaka kuzima umeme, lakini moshi ulishatanda na hivyo nilishindwa,” anasema.

Wingi wa moshi, anasema ulisababisha hata askari wa zimamoto kumwaga maji katika eneo lisilo sahihi.

Kuungua kwa chumba hicho, kumeacha simanzi zaidi kwa Mtunza ghala wa MCL, Stella Joseph anayesema anajiona hana kazi ya kufanya kwa sasa kwa kuwa ofisi yake imeungua.

“Sikuwa naelewa kitu cha kufanya, kuna vitu vingi sana vya thamani vya kiwandani vyote vimeungua na sielewi chanzo chake. Siku moja kabla ya moto kulikuwa na mzigo mpya umeingia na haukuwa umefunguliwa kwa muda huo ukitarajiwa kuanza kutumika siku inayofuata kabla ya tukio kutokea,” anasema Stella.


Moto ulivyoathiri shughuli

Vichwa vya wahariri watendaji wa magazeti ya Mwananchi, Mwanaspoti na The Citizen siku hiyo, viliwaza namna watakavyofikisha bidhaa sokoni katika mazingira hayo.

Hiyo ilitokana na ukweli kwamba, moto ulitokea katika chumba kilichopo karibu na kiwanda cha uchapaji wa magazeti hayo wanayoyasimamia.

Katika mazingira hayo, uamuzi wa haraka wa kuwasiliana na kampuni za nje za uchapishaji ikiwemo Jamana Printers Ltd zilifanyika na kufanikiwa.

Pamoja na mafanikio hayo, kulikuwa na athari katika muda wa kufikisha bidhaa hiyo sokoni, kwani yalichapwa kwa kuchelewa kutokana na dharura hiyo.

Kwa mujibu wa Damas, hadi moto unatokea tayari asilimia 95 ya gazeti lilishachapwa, zilibakia kurasa za michezo na ilisubiriwa habari kuhusu mechi ya Yanga na JKT.

“Tunatakiwa tumalize gazeti saa 2:00 usiku lakini siku hiyo Saa 6 usiku ndiyo gazeti zilikwenda kuchapishwa kwenye mtambo wa The Guardian, gari zetu nyingi hazikuwa njiani kwa wakati huo zililazimika kusubiri, kuna baadhi ya mikoa hatukwenda kabisa tulilazimika kupunguza oda na tuliangalia soko la mikoa ya jirani na vituo vikuu. Mikoa ya mbali tuliamua kutokwenda,” anasema Damas.

Kulingana na Damas, magazeti yalikwenda katika mikoa ya Morogoro, Iringa, Dodoma, Arusha na Mbeya, lakini baadhi ya maeneo likiwemo Jiji la Mwanza lilikosa kwa kuwa muda wa kusafirisha kwa ndege ulishapita.

Lakini,uwezo wa kusoma mtandaoni kupitia e-Gazeti anasema uliendelea kuwepo na kesho yake uzalishaji uliendelea kama kawaida.

Mbali na athari katika mauzo, Magwa anasema baadhi ya wafanyakazi walilazimika kurudi ofisini kumalizia kazi, baada ya moto kudhibitiwa.

Hali hiyo iliwaathiri hata wasanifu kurasa ambao ndiyo hufanya mchakato wa mwisho kabla ya gazeti kwenda mtamboni kama anavyosimulia, Himid Nyombwe anayefanya kazi hiyo.

“Saa 9 alfajiri ndiyo niliingia nyumbani kwangu, hii ni baada ya kuhakikisha magazeti yote yamechapishwa, huku wenzangu wakifika majumbani mwao saa 10 alfajiri,” anasema.


Mshtuko kila sehemu

Mhariri Mtendaji Mkuu wa MCL, Victor Mushi anasema ilimchukua muda kuelewa kuhusu tukio hilo, hata baada ya kuelezwa, lakini baadaye alielekeza gari lake litolewe nje kisha kuhakikisha usalama wa wafanyakazi wote.

Baada ya gari lake kuwa nje, anasema alihofu iwapo kwenye chumba cha habari kuna mfanyakazi yeyote aliyebaki.

"Miongoni mwa mafunzo tuliyojifunza ni MCL inahitaji kuwa na njia iliyopangwa zaidi ya kushughulikia dharura hizi, ili sote tujue inapotokea ni kitu gani kitakachotangulia kabla ya kufanya kitu chochote," anasema.

Sebastian Nkoha, Meneja wa Teknolojia ya Habari (Tehama) wa MCL, anasema mpango wa majanga umesaidia kubadilisha mfumo wa uchapaji kwa haraka ingawa sio kwa kiwango kilichozoeleka.

"Tayari tulishaweka vitu vingi katika mipango ya majanga na ndiyo sababu tulipeleka kwa wachapaji wengine na tukafanikiwa kuchapa magazeti yetu,” anasema.

Kuhusu tukio hilo, anasema alipopata taarifa alidhani ni kiwanda chote kinaungua, hali iliyomsababishia mfadhaiko na hivyo kushindwa kuendesha gari.

Kwa sasa, anasema wanajadiliana kuwa na utaratibu wa kuzima mitambo kisha kuchapa magazeti katika kampuni nyingine mara mbili kwa mwaka, ili kujijengea utayari wa majanga.

“Hili ni eneo la kupata kipato chetu cha kila siku halafu unaona kunaungua ina maana hapo akili inayokuja kwa haraka ni inakuaje kuhusu kipato na ndiyo maana vijana walikuwa wanapambana kuzima moto,” anasema.

Anasema hata vijana kukubali kuingia kwenye hatari yote ni kwa ajili ya kupambania riziki zao.

Tukio hilo, lilimtoa chozi Thadeus Kisaka mbeba vifaa wa stoo za MCL akisema, "Watu wananiuliza kwa nini ulilia siku ya tukio, sababu kubwa niliwaza maisha yangu yatakuaje.

Kipindi hiki kuanza kutafuta kazi sehemu nyingine kwa haraka napata wapi na wakati huo nilitoka hospitali dada yangu kajifungua ndiyo sababu ya kulia na kupambana kuuzima moto."

Lakini wengine, walikuwa mithiri ya waokozi katika tukio hilo, mathalan Esther Mvungi, Mhariri wa Habari wa gazeti la Mwananchi, aliyeamua kumchukua mmoja wa wafanyakazi ambaye ni mjamzito na kumrudisha nyumbani ili kumuepusha na madhara ya moshi.

"Kadiri muda ulivyokuwa unasonga ndivyo hali ya afya za baadhi ya watu zilikuwa mbaya, hivyo niliamua kuondoka na mmoja wa wafanyakazi ambaye ni mjamzito na kumrudisha nyumbani kwake," anasema Mvungi.


Hatua zinazochukuliwa

Meneja Rasilimali watu na Utawala wa MCL, Paul Hamidu anasema wamepokea ushauri tofauti kutoka kwa wadau ikiwemo kuwa na visima vya kuzima moto.

“Tumeambiwa kuna vifaa vya kisasa vyenye uwezo wa kudaka taarifa mapema tunatakiwa kuwa navyo kwa ajili ya kujikinga na majanga ya moto, na hii itasaidia kwenye kupata taarifa,” anasema.

Hata hivyo, anasema wafanyakazi mbalimbali waliokutwa na changamoto kutokana na ajali hiyo wameshapelekwa kufanyiwa uchunguzi wa kitabibu kujua walivyoathirika.


Kauli ya Mkurugenzi Mtendaji

Mkurugenzi Mtendaji wa MCL, Bakari Machumu anasema hofu kubwa baada ya taarifa hiyo ilikuwa kwa wafanyakazi wake.

Anasema alitamani kusikia tukio hilo ni dogo na kwamba limeshadhibitiwa, lakini haikuwa hivyo.

Alipopewa taarifa kutoka kwa Hamidu, Machumu anaeleza alifika ofisini na kushuhudia moshi mzito.

“Nilipofika mita 200 kabla ya MCL nilikutana na moshi, tunachoshukuru jengo la stoo ni imara sana, moto uliwaka zaidi ya saa nne, uharibifu mkubwa uliotokea mle lakini haukutoka nje,” anasema.

Anasema maboresho ya mtambo wa uchapaji yamefanyika usiku kucha kuhakikisha shughuli zinaendelea.

“Tumefanya majaribio na tumethibitisha kwamba kazi inaweza kuendelea, tuliwajulisha wateja wetu wa nje kuwa tupo sawa hivyo tunaweza kuendelea na kazi ya kuchapisha magazeti yao,” anasema.

Hata hivyo, anasema mpango wa mafunzo ya kukabiliana na majanga kwa wafanyakazi wote unatarajia kutolewa.