Shahidi kesi ya kina Mbowe asimama ghafla akihojiwa, asema hajisikii vizuri

Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe akiwa anasoma kitabu akisubiri kesi kuanza ndani ya Mahakama Kuu ya Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumi Uchumi Dar es Salaam . Picha zote na Sunday George
Muktasari:
- Mkaguzi wa Polisi, kutoka Ofisi ya Mkuu wa Upelelezi, Mkoa wa Kipolisi Temeke, Tumaini Swila ambaye ni shahidi wa 13 wa upande wa mashtaka katika kesi ya ugaidi inayomkabili Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na wenzake watatu amesimama ghafla na kuieleza Mahakama kuwa hajisikii vizuri wakati akihojiwa na Wakili wa utetezi Peter Kibatala.
Dar es Salaam. Mkaguzi wa Polisi, kutoka Ofisi ya Mkuu wa Upelelezi, Mkoa wa Kipolisi Temeke, Tumaini Swila ambaye ni shahidi wa 13 wa upande wa mashtaka katika kesi ya ugaidi inayomkabili Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na wenzake watatu amesimama ghafla na kuieleza Mahakama kuwa hajisikii vizuri wakati akihojiwa na Wakili wa utetezi, Peter Kibatala.
Shahidi huyo ambaye leo Jumatano Februari 9, 2022 aliendelea kuhojiwa kuhusu ushahidi alioutoa, ikiwa ni siku ya tatu mfululizo upande huo wa utetezi wanamhoji.
Swila alianza kuhojiwa na upande wa utetezi juzi Jumatatu baada ya kumaliza kutoa ushahidi wake katika Mahakama Kuu, Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi.
Leo, wakati akiendelea kuhojiwa na Wakili Kibatala, ghafla shahidi huyo alisimama na kusema kuwa hajisikii vizuri hivyo upande wa mashtaka kuomba Mahakama kuahirisha kesi hiyo mpaka kesho.
Baada ya upande wa mashtaka kuomba ahirisho hilo, upande wa utetezi ukiongoza na Wakili Kibatala ulipinga ahirisho la mpaka kesho huku ukitaka ahirisho la muda mpaka saa tisa jioni.
Hata hivyo, Jaji Joachim Tiganga anayesikiliza kesi hiyo akirejea sababu za maombi ya ahirisho na hoja za utetezi kupinga, amesema kutokana na ombi la upande wa mashtaka kuwa linahusiana na suala la kiafya ambalo ni muhimu, amekubali ombi la kuahirisha kesi hiyo.
Jaji Tiganga ameahirisha kesi hiyo mpaka kesho Alhamisi Februari 10, 2022.
Hapa ni mahojiano kati ya Wakili Kibatala na shahidi wa 13 wa upande wa mashtaka…
Jaji Joachim Tiganga ameshaingia mahakamani na mawakili wa pande zote wamajitambulisha.
Sasa Wakili Kibatala anaendelea kumhoji shahidi
Wakili: Morning Mr Swila
Shahidi: Morning
Wakili: Tulijadili jana kuwa wakati wanakwenda Morogoro (washtakiwa) walikuwa wametoka sehemu mbalimbali za nchi?
Shahidi: Ni sahihi
Wakili: Ni sahihi kwamba aliyewa-summon ni Urio?
Shahidi: Ni sahihi kwa matakwa ya Mbowe
Wakili: Ni sahihi huko walikokuwa walikuwa wanafanya shughuli halali na hawakuwahi kujihusisha na uhalifu?
Shahidi: Ni sahihi
Wakili: Ni sahihi shahidi kwamba Luteni Urio aliwa-convene Morogoro kwa sababu makazi yake yalikuwa ni Morogoro?
Shahidi: Ni sahihi
Wakili: Ni sahihi kwamba mshtakiwa Freeman Mbowe hakuwahi kuwepo Morogoro before au after? Washtakiwa kukutana Morogoro?
Shahidi: Ni sahihi
Wakili: Uliwahi kufahamu kwamba mshtakiwa wa tatu kabla ya kwenda Morogoro kukutana na Urio ilibidi Urio amuombee ruhusa kwa baba yake?
Shahidi: Sikuwahi kufahamu
Wakili: Nikikwambia kuwa pia mzee Ling'wenya ilibidi aitishe kikao akiwemo mjomba wake ili uamuzi uwe ni wa pamoja?
Shahidi: Sikufahamu?
Wakil: Hukuwahi kufahamu kuwa wazazi wake walimwachia mtoto wao kwenda kwenye mikono salama ya Urio na Mbowe ambao walikuwa wanafahamika?
Shahidi: Sikuwahi fahamu
Wakili: Uliwahi kufahamu wakati washtakiwa wanakaa Morogoro katika makundi mawili Mbowe hakuwahi kutia neno kwa yaliyokuwa yanajadiliwa pale?
Shahidi: Wakati gani? Hebu fafanua
Wakili: Ok, Iko hivi, umefanya upelelezi ukaandika taarifa, swali langu ni kwamba Urio alikaa nao washtakiwa kwa makundi mawili. Kwanza Halfan na Lujenge kisha Adamoo na Ling'wenya, swali langu ni kwamba Mbowe alitia neno katika hilo?
Shahidi: Sifahamu
Wakili: Aliyewamba Bwire na Lujenge na Adamoo na Ling'wenya mahitaji ya kuwepo kwa hiyo kazi ni Urio, ni sahihi?
Shahidi: Ni sahihi, baada ya kuwasiliana na Mbowe
Wakili: Waliwasiliana kwa njia gani?
Shahidi: Ni pale alipomwambia LutenI Denis Urio amtafutie hao. Pia walikuwa wanawasiliana kwa simu kwa telegram.
Wakili: Kwa kuwa wewe hukuwepo wala Kingai na DCI ambaye ndiye mlalamikaji utakubaliana na mimi kuwa yote mliyoambiwa na Urio ni hearsay?
Shahidi: Siyo hearsay
Wakili: Utakubaliana na mimi kwamba kwa kuwa sote hatukuwepo ni lazima kwanza tumuamini kwanza Urio na tulinganishe neno la Urio na la Mbowe?
Shahidi: Siyo lazima
Wakili: Kwa nini siyo lazima?
Shahidi: Maneno na aliyoyasema Urio bila hata kumtumia mshtakiwa wa nne yalifanyiwa kazi na ukweli ukajulikana
Wakili: Mlirekodi mazungumzo ya Mbowe na Urio?
Shahidi: Hapana
Wakili: Urio alitaja kuwa alikutana na Mbowe kwamba walikutana Casa Hotel, uliwahi kwenda kwenye hiyo hoteli?
Shahidi: Sikwenda maana hapakuwa na umuhimu
Wakili: Pia Urio alitaja kuwa walikutana na Mbowe kwenye mghahawa fulani, uliwahi kumchukua akupeleke kwenye huo mghahawa?
Shahidi: Hapana, hapakuwa na umuhimu?
Wakili: Sijakuuliza umuhimu
Shahidi: Wewe unaniuliza swali nami najibu sasa usichague majibu yangu mimi nakujibu ninavyofahamu na si unavyotaka wewe?
Wakili: Mtu anapoleta taarifa wewe kama mpelelezi unaichunguza kwanza au unafungua tu file?
Shahidi: Inategemea na taatifa yenyewe
Wakili: Hii ya Urio mliichunguza?
Shahidi: Ndio
Wakili: Uliwahi kwenda 92KJ kujiridhisha kuwa tarehe 14/7/2020 alikuwepo kazini?
Shahidi: Sikwenda
Wakili: Ulichunguza kwamba baada ya taarifa kuwa Urio ndio aliwapeleka kina Adamoo kwa Mbowe naye alikamatwa?
Shahidi: Ndio nilichunguza
Wakili: Uliongea na nani?
Shahidi: Kupitia jalada la uchunguzi
Wakili: Sitaki jalada la uchunguzi
Shahidi: Sasa unanichagulia jibu? Mimi nimeshakujibu
Wakili: Unamjua mkuu wa kikosi cha 92KJ ni nani?
Shahidi: Simfahamu
Wakili: Uliwahi kuandika rekodi za mawasiliano ya simu ya Mbowe na uliomba rekodi za mawasiliano?
Shahidi: Ndio nilifanya
Wakili: Kwa barua ya tarehe ngapi?
Shahidi: Barua ya tarehe 23/8/2020
Wakili: Ilikwenda wapi?
Shahidi: Kitengo cha uchunguzi wa Cyber
Wakili: Kule kwa Ndowo?
Shahidi: Ndio
Wakili: Ndowo ndio anatunza rekodi za mawasiliano ya simu?
Shahidi: Ili aombe
Wakili: Kwa hiyo ulimu-instruct Ndowo aombe?
Shahidi: Sikumuelekeza Ndowo niliandika kwa Kitengo
Wakili: Report ya uchunguzi ya Ndowo uliiona?
Shahidi: Ndio niliiona
Wakili: Kuna mahali Ndowo ameonyeaha kuwa uliwahi kuomba voice recorded?
Shahidi: Hakuna
Wakili: Ulimueleza Jaji kwa nini hakuomba?
Shahidi: Sikumwambia
Wakili: Hivi DCI au Kingai wakipokuteua kuwa kwenye hiyo timu ya upelelezi walikuteua kwa ajili ya uwezo au kwa sabau tu uko kwenye hicho kitengo?
Shahidi: Sababu ya uwezo
Wakil: Hivi una elimu gani vile?
Shahidi: Kidato cha sita
Wakili: Baadaye ukaenda Chuo Kikuu?
Shahidi: Hapana
Wakili: Ahaa umaenda chuo cha Polisi moja kwa moja?
Shahidi: Ndio
Wakili: Sawa nimeamini uliteuliwa on merit. Unafahamu kuwa hawa vijana walipokwenda Morogoro walitumia nauli zao?
Shahidi: Sijui
Wakili: Unafahamu kwamba Freeman Mbowe alitoa shilingi 669000 / kufadhili ugaidi, unafahamu kwamba kama mpelelezi unatakiwa ku-trace kila sent ilitumikaje?
.
Shahidi: Sio lazima, cha msingi ni mtumaji kuwa na uelewa wa malengo
Wakill: Unafahamu kwamba mahakama inataka ipate uelewa kuwa aliituma na ilitumikaje?
Shahidi: Nafahamu
Wakil: Sawa tumeshafahamu Urio hakukueleza kuwa washtakiwa watatu na mwingine ambaye yuko at Large walitumia nauli zao mpaka Morogoro? Alikwambia nani aliwa-refund?
Shahidi: Luteni Urio
Wakil: Unafahamu kwamba mpaka wanakwenda Morogoro walikuwa hawajui kuwa wanakwenda kuambiwa nini?
Shahidi: Ndio
Wakili: Unakumbuka kiasi cha pesa iliyokuwa exchanged kati ya Urio na Lujenge?
Shahidi: Sikumbuki
Wakili: Hivi waliokueleza kuja kutoa ushahidi kwenye hii kesi walikuwa serious au walikwambia mradi tu?
Shahidi: Serious
Wakili: Hii kesi ni nzito au nyepesi?
Shahidi: Nzito
Wakili: Nani yuko accountable for kwa hili, tumuulize nani?
Shahidi: Sijui
Wakili: Hela iliyobadilishwa kati ya Urio na Adamu Kasekwa, Adamoo ni shilingi ngapi?
Shahidi: Sikumbuki
Wakili: Unafahamu Lujenge alipewa nauli shilingi ngapi kwa ajili ya kwenda Moshi au Dar?
Shahidi: Sikumbuki, siwezi kukumbuka kila kitu mimi nilifanya upelelezi na kujua hiyo hela ilitumikaje
Wakili: Huo mgawanyo ndo tunataka kufahamu. Unafahamu Ling'wenya alipewa nauli kiasi ni kwenda Dar kama anavyosema au Moshi kama Urio anavosema?
Shahidi: Sikumbuki
Wakili: Wakati wanakwenda Moshi walikuwa wanajua wanakwenda kufanya nini?
Shahidi: Sifahamu
Wakili: Sheria ya ugaidi unaifahamu umewahi kuisoma kidogo?
Shahidi: Nimeisoma kidogo
Shahidi: Unafahamu vipengele vinavyohusu kufadhili ugaidi?
Shahidi: Ndio
Wakili: Cha kwanza?
Shahidi: Lazima awe ametuma hela lazima awe anajua hiyo hela anatuma kwa lengo la ugaidi
Wakili: Cha pili?
Shahidi: Sio lazima awe eneo ambalo utatokea ugaidi
Wakili: Cha tatu?
Shahidi: Sio lazima ajue hizo hela zinatumikaje
Wakili: Nikiwa nataka mtu afanye ugaidi Mtwara, zikaenda kutumika kwa kilimo cha mpunga nakuwa nimefadhili ugaidi?
Shahidi: Inategemea
Wakili: Na nini?
Shahidi: Kama kweli imetumika kwa kilimo
Wakili: Ndio ushahidi upo amelima mpunga, japo bado ugaidi unasimama?
Shahidi: Ndio
Wakili: Una uhakika kuwa hiyo 669,000 yote ilitumika baada ya kuwa wameshafika Moshi au iliishia kwenye refund ya nauli?
Shahidi: Hilo sifahamu ila ilitumwa kwa malengo hayo
Wakili: Ndio nataka uidadavue
Shahidi: Hilo nimeshajibu si lazima ajue imetumikaje
Wakili: Urio anasema tarehe 20/7/2020 alitumiwa shilingi laki tano?
Shahidi: Sahihi
Wakili: Hiyo laki tano Mbowe aliituma kwa lengo gani?
Shahidi: Kufadhilli vitendo vya kigaidi
Wakili: Ambavyo ni vipi?
Shahidi: Kuchoma vituo vya mafuta kulipua masoko na maandamano na kuwadhuru viongozi
Wakili: Katika ushahidi wake anaeleza laki tatu alii-refund kwa Bwire na Lujenge, unafahamu au hufahamu?
Shahidi: Sifahamu
Wakili: Kati yako na Urio nani yuko kwenye nafasi nzuri ya kufahamu jinsi hela ilivyotumika?
Shahidi: Urio
Wakili: Ulisoma statement za Adamu na Ling'wenya jinsi hela ilivyotumika?
Shahidi: Nilisoma lakini sikumbuki hicho kiwango.
Wakili anampatia shahidi maelezo ya washtakiwa hao wawili ya Adamu Kasekwa na Ling'wenya
Wakili: Tuanze na ya Adamu Kasekwa, tafuta sehemu ambapo anasema tarehe 24/7/2020 nilikutana na Mohamed Ling'wenya. Soma kwa sauti na shahidi anasoma.
Wakili: Ni shilingi ngapi hapo ametaja?
Shahidi: 87,000 kwa nauli ya Moshi
Wakili: Ulilinganisha kiwango cha nauli kwa maelezo ya Kasekwa na ya Urio?
Shahidi: Ndio
Wakili: Urio alisema aliwapa shilingi ngapi?
Shahidi: Sikumbuki
Wakili: Sasa nakukumbusha maelezo ya Urio ambayo ni kielelezo cha utetezi cha 4 (exh D4)
Wakili Kidango anapinga kuwa kielelezo hicho kilitolewa kwa shahidi wa 12 kama kielelezo cha utetezi, tunaona si sahihi kumhoji shahidi aliyeko mahakamani kwa kielelezo hicho badala ya shahidi aliyepita.
Wakili Kibatala: Mheshimiwa Jaji upande wa mashtaka hauna hoja. Document hii iko on record aliiandika shahidi na defense exhibit. Naomba niruhusiwe kuendelea
Wakili wa Serikali Abdallah Chavula: Mheshimiwa Jaji waliomba statement hii kupitia kifungu cha 164 na 154 cha Sheria ya Ushahidi Sura ya Sita. Kifungu hiki kiko wazi na purpose ni kum-contradict shahidi, na ni shahidi aliyepita sio kweli kwamba hawana ukomo
Wakili Kibatala anasimama akitaka kumjibu hoja za Chavula kisha wakili wa Serikali Pius Hilla anasimama na kuanza kuzungumzia huku Kibatala naye akiwa bado amesimama.
Wakili Hilla anamtaka Wakili Kibatala akae lakini Wakili Kibatala naye anamtaka Wakili Hilla akae huku akimwambia Hilla kuwa anafanya fujo mahakamani.
Jaji anaingilia kati anamtaka Kibatala akae na kwamba yeye ndiye atakayeamua kama ni fujo au si fujo.
Wakili Kibatala anakaa chini na wakili Hilla anaendelea kisha wakili Chavula anasimama tena na kusisitiza hoja zake kuwa kwa namna walivyoingiza maelezo hayo, wanna ukomo wa kuyatumia.
Wakili Chavula anasoma kifungu Cha 154 ambacho anasisitiza kuwa kinalenga kum-contradict maker wa hiyo statement na kwamba kwa kuwa mahakama imeamini kuwa maker ni PW12 ( shahidi wa 12 upande wa mashtaka), basi hana nafasi tena kuitumia kwa shahidi huyu.
Wakili Kibatala: Kwanza sect 154 yametoka kwa bar si kwenye sheria. Shahidi huyu tumekubaliana kuwa ndiye aliyeandika statement hiyo.
Kifungu 154 ni cha kuruhusu statement kuingia.Tumeweka foundation kumuuliza huyu not from air bali amesema working tool zake kama mpelelezi zilikuwa ni pamoja na statement hii.
Lakini pia tayari nilisham-cross kabla. Ukikataza Mheshimiwa Jaji itakuwaje kuhusu majibu ambayo tayari nilisham-cross kabla? Kwa hiyo tunaomba turuhusiwe kuendelea
Jaji: Hoja iliyojitokeza kutoka kwa Wakili Kidando kuwa upande wa utetezi hauna haki ya kuitumia kielelezo kilicholetwa na upande wa utetezi na kama Chavula alivyosema kililetwa kwa ajili ya shahidi wa 12 tu hivyo kina ukomo..
Hoja hiyo imepingwa na Kibatala akisema kuwa vifungu hivyo vinaruhusu pia mtu aliyeiandaa statement hiyo.
Mahakama kwa kuzingatia hoja zote imetafakari kwa kina na imeongozwa na kanuni inayoongoza kuuliza maswali kuwa lengo ni kutengeneza msingi.
Shahidi huyo ni mpelelezi wa shauri hili. Katika ushahidi wake wa msingi alisema kama mpelelezi akitumia nyaraka zote na akafikia hitimisho anashauri kufungua mashtaka.
Katika ushahidi wake wa msingi alisema ndiye aliyeandika statement hii hivyo ana uelewa wa kile anachoulizwa na kwa kuzingatia alishaulizwa maswali huko nyuma japo hakuwa amepewa statement hii lakini kwa mazingira haya hakuna uvunjifu wa haki. Hivyo ninaruhusu aendeleee kuulizwa na pale ambapo atashindwa tutaona ni sababu zipi ameshindwa.
Kibatala: Kwa sababu nimekupeleka katika eneo specific la hela? Sasa nenda katika maelezo ya Urio, halafu soma.
Shahidi amepewa maelezo ya Urio, yaliyoandikwa na Mkaguzi Tumaini Swila.
Kibatala: Kwa hiyo tunakubalia hapo Julai 22, 2020 Urio alitumiwa fedha kiasi Sh 199,000 na Mbowe kupitia wakala kwa ajili ya kuwapa Adam Kasekwa na Mohamed Ling'wenya kwenda Dar
Shahidi: Ndio.
Kibatala: Je? Fedha hizo zinaendana na zile ulizosoma awali, ambazo Bwire na Moses Lujenge ambazo walitumia Sh87,000.
Shahidi: Zinaendana.
Kibatala: Sasa naomba unijibu swali langu, hizo 87,000 walizopewa Bwire na Moses Lujenge kwa ajili ya kwenda Moshi, zilikuwa ni shilingi ngapi.
Wakati Kibatala akiendelea kumhoji shahidi.
Ghafla shahidi amesimama na kueleza kuwa hajisikii vizuri.
Kibatala: Ingawa sisi sio madaktari lakini tuna wasiwasi na sababu za kuahirishwa kwa kesi hii...kuna sababu nyingine zisizo za kiafya.
Kibatala: Tunaongea haya kwa sababu kuna mashahidi watatu waliomba kuahirisha hii kesi kwa sababu ya kuugua lakini hawakuleta uthibitisho mahakama.
Kidando: Mheshimiwa Jaji nimeongea hapa shahidi ameniambia anaona mwili hauna nguvu na ni suala la afya pia.
Kidando: Kutokana na sababu hizo tunaomba ahirisho la kesi hii.
Jaji: Hili ahirisho ni la masaa au?
Kidando: Shahidi anaomba kwenda hospitali, hivyo tunaomba kesi hii tuahirishe hadi kesho.
Kibatala: Sisi tuna wasiwasi kuhusiana na ahirisho hili...tunapinga ahirisho hili hadi kesho badala yake tunaomba Mahakama itoe ahirisho mpaka saa 9 mchana ili shahidi aje atupe progress ya hali yake.
Kibatala: Na kama ni kesho, basi shahidi aje na uthibitisho kutoka hospitali aliyokwenda kutibiwa.
Kibatala: Nasema hivi kwa sababu ahirisho hili linaathiria mawakili na wateja wetu.
Kibatala: Tumeona SP Jumanne Malangahe hakuleta uthibitisho baada ya kusema anaumwa...hivyo hivyo Inspector Innocent Ndowo naye aliugua na kesi ikaahirishwa na hakuja na udhibitisho wowote siku iliyofuata, hivyo tumeomba izingatia hilo.
Kidando: Mheshimiwa Jaji mwenzetu (Kibatala) ana wasiwasi juu ya hilo, lakini kwanini asiheshimu haki za watu? Asubuhi hapa kabla ya kesi kuanza shahidi aliieleza mahakaka kuwa bado afya yake haiko vizuri.
Uamuzi wa Mahakama:
Jaji Tiganga: Kwanza anarejea sababu za maombi ya ahirisho na hoja za utetezi kupinga
Nimezingatia hoja za pande zote mbili lakini hoja ya shahidi na ukweli kuwa shahidi wakati mahakama inaanza ameieleza mahakamani kuwa jana aliumwa na ataendelea na ushahidi.
Pale inapoombwa kuwa shahidi hajisikii vizuri ni sababu tosha ya kuahirisha kesi na kwa kuzingatia utamadumi huo na kwa kuwa afya ya mtu ni sababu ya msingi. Hivyo tunatoa ahirisho.
Suala ni muda gani suala la afya si busara kupangia muda. Linahitaji attention kubwa lakini pia madaktati ndo wanaweza kusema. Hivyo mahakama haiwezi kumpangia kuwa aende arudi hapa muda gani.
Katika mazingira hayo ni busara kuahirisha mpaka kesho.
Kuhusu ombi la utetezi kuleta ushahidi mahakama inaona ni busara kwamba shahidi aje na uthibitisho sio lazima awe na details za ugonjwa wake lakini kueleza alikuwa anaumwa na alienda hospitalini.
Kwa hiyo shauri hili linaahirishwa mpaka kesho tutakapokuja kuendelea kupokea ushahidi wake
Jaji: Shahidi unaonywa kwamba uko chini ya kiapo na utatakiwa kufika mahakamani hapa kesho kuendelea na ushahidi wako.
Jaji: Pia mahakama inakutaka kuleta uthibitisho sio lazima uwe na details ili kulinda privacy ya afya yako lakini angalau kuonesha kuwa unaumwa na ulikwenda hospitalini