Prime
Hizi ndizo sifa wanazotaka wanaume kwa wanawake

Muktasari:
- Ingawa kila mwanaume ana vigezo vyake, kuna tabia za kimsingi ambazo kwa ujumla huongeza mvuto wa mwanamke na kuimarisha uhusiano wake na mpenzi wake.
Katika uhusiano wa mapenzi, kuna sifa zinazomfanya mwanamke awe wa kipekee na kuvutia mwanaume.
Ingawa kila mwanaume ana vigezo vyake, kuna tabia za kimsingi ambazo kwa ujumla huongeza mvuto wa mwanamke na kuimarisha uhusiano wake na mpenzi wake. Tuone baadhi ya sifa hizo.
Hana mambo mengi
Mwanaume huvutiwa na mwanamke anayetoa mazingira ya utulivu na amani. Mwanamke asiye na drama, asiye na ugomvi wa mara kwa mara, na anayejua faraja ni hazina.
Wanaume wanapenda mahali wanapopata utulivu wa moyo na akili, hivyo mwanamke mpole na mtulivu ana fursa kubwa ya kumvutia mpenzi.
Kujiamini
Kujiamini ni moja ya sifa zinazovutia sana. Mwanamke anayejua thamani yake, anayejitunza, anayezungumza kwa ujasiri, na anayejiheshimu huwa na mvuto wa kipekee.
Kujiamini si kiburi, bali ni ufahamu wa thamani yako na kutoogopa kuionyesha. Mwanaume huvutiwa na mwanamke anayejiamini kwa sababu huwa na uwezo wa kujitegemea na kujiheshimu.
Mahusiano yoyote yanahitaji mawasiliano bora. Mwanamke anayejua jinsi ya kuzungumza kwa heshima, kutoa hisia zake bila kupayuka au kukasirika ovyo, huwa rahisi kuelewana naye.
Uwezo wa kuwa mchangamfu, mcheshi, na mwenye busara katika mazungumzo humfanya mwanaume kumkumbuka hata wanapokuwa mbali.
Anashikilia uamuzi bila kutetereka
Mwanamke ambaye ana msimamo thabiti na si rahisi kuyumbishwa na presha za marafiki, mitandao ya kijamii, au tamaa za muda mfupi huwa kivutio.
“Mwanamke kama huyu anajua anachotaka maishani na anaendelea kusimamia misingi yake bila kutetereka. Mwanaume anapenda mwanamke anayejiamini katika maamuzi yake na si mwepesi wa kushawishika bila sababu,” asema Lily Kiprono, mwanasaikolojia na mtaalamu wa uhusiano.
Anasema mwanamke mwenye roho ya malezi, anayejali wengine, na anayesaidia watu kukua kimawazo na kimaendeleo huvutia sana.
“Hii haimaanishi tu kuwa mwanadada mzuri bali pia kuwa na uwezo wa kusimamia mambo kwa hekima, kusaidia mpenzi wake kufanikisha malengo yake, na kuwa mtu wa kuongeza thamani katika uhusiano,” asema Lily.
Kulingana na mwanasaikolojia Beku Naseku, mwanamke anayejipenda na kujiheshimu anavutia zaidi.
“Huyu ni mwanamke anayefurahia maisha yake bila kuwa na wivu wa kupindukia au hofu ya kushindana na wanawake wengine, kwa sababu anajua thamani yake. Kujipenda kunamfanya awe na furaha ya kweli, na mwanaume anavutiwa na mwanamke mwenye furaha na utulivu wa moyo,” aeleza.
Mwanamke wa bidii, anayejituma
Beku anasema hakuna kitu kinachovutia mwanaume kama mwanamke anayejituma na mwenye malengo maishani.
Mwanamke mwenye maono na anayechapa kazi ili kuyatimiza ana thamani zaidi.
Mwanaume anapenda mwanamke anayejitahidi kufanikisha mambo yake mwenyewe, badala ya kumtegemea kwa kila kitu.
Mwanamke anayeshiriki kikamilifu katika mahusiano yake huvutia mwanamume ikawa vigumu kumuacha.
“Huyu ni tofauti na anayeacha kila kitu kifanywe na mwanaume huku yeye akilalamika. Badala yake, yeye ni msaidizi wa kweli, anayetoa mawazo, kusaidia kupanga mambo, na kushiriki katika maamuzi muhimu. Mahusiano bora hujengwa kwa ushirikiano,” aeleza Beku na kuongeza kuwa uvumilivu wa mwanamke ni dafina kwake.
“Mwanamke mvumilivu huthamini hatua ndogo za maendeleo katika uhusiano. Hana presha ya kupata kila kitu mara moja, bali hujua mambo mazuri huchukua muda. Mwanaume anapenda mwanamke anayeweza kuvumilia changamoto na kusherehekea maendeleo hata kama ni madogo,” afafanua.
Kulingana na mwanasaikolojia Lily, wanaume, hasa wa kisasa, huvutiwa na mwanamke anayejua kujieleza kwa hekima na mwenye mawazo ya kina.
Mwanamke anayetoa ushauri mzuri, anayemchochea mwanaume kufikiria kwa kina, na anayejali zaidi utu kuliko vitu vya anasa ana mvuto wa pekee. Sifa hizi zinamfanya mwanamke kuwa wa kipekee na kuvutia mwanaume.
Ingawa sura na mwonekano vinaweza kuvutia kwa muda, ni tabia na hulka za ndani zinazomfanya mwanamke kudumu katika moyo wa mwanaume.
Mwanamke anayejiheshimu, anayependa amani, mwenye malengo, mwenye hekima, na anayeshiriki kikamilifu katika mahusiano yake ana nafasi kubwa ya kuwa mpenzi wa kweli na mwenzi wa maisha.
Heshima na akili
Mwanasaikolijia, Veronica Masanja amesema kisaikolojia wanaume wanapenda wanawake wasafi, wenye heshima, uwezo mkubwa kiakili, huku urembo na uzuri vikiwa sifa za ziada.
“Attraction (kuvutiwa) inaazia mbali, wanaume wengi wanapenda wanawake wenye utulivu kwa maana ya kutokuwa na visirani, ucheshi, ujasiri, unyenyekevu, unadhifu, upendo, utii na heshima,”anasema Masanja.
Uzuri wa umbo
kwa ujumla wanaume wengi huvutiwa kwanza na maumbile (jinsi mwanamke alivyoumbika) ikiwemo sura.
“Wapo wanaume wanavutiwa na wanawake wenye maumbo makubwa, hasa makalio, lakini pia wapo wanaume wanaovutiwa na wanawake wenye maumbile ya wastani na hata wembamba,”anasema Rehema Mansoor mkazi wa Butimba jijini Mwanza.
Anaongeza lipo pia kundi la wanaume wanaovutiwa na rangi ya mwanamke iwe weupe au weusi na wakati mwingine, wapo wanaume wanaovutiwa na kitu kimoja kimoja kwa mwanamke kama vile miguu iliyojaa, macho ya mviringo, macho ya kurembua, macho makubwa na wakati mwingine macho madogo.