Prime
Mafanikio huwa neema, nakama kwa wanandoa

Wanandoa wawili walioana wakiwa maskini walijaliwa kupata utajiri baada ya kusota kwa muda. Walisimama kidete na kujikunja hadi wakachuma na kuukata.
Walifanya kazi kwa bidii kama wadudu. Kila kitu kiliwekwa pembeni wakati wa mchakato huu wenye kila changamoto hata kukatishwa tamaa mbali na kuhujumiwa.
Baada ya kupata, tabia za baba zilianza kubadilika. Alianza kutumia muda mwingi na matajiri wenzake na wapambe. Ilifikia akakosa hata muda kidogo wa kukaa na mkewe. Hili lilimchanganya na kumuudhi mkewe ambaye muda wote wa kutafuta walikuwa pamoja. Alijiuliza.
Iweje sasa tumeneemeka, mume anaanza kukosa muda nami? Swali hili hakuweza kulipatia jibu. Hata alipomuuliza mumewe, alimjibu kuwa alikuwa kwenye vikao na mipango ya fedha. Maskini alisahau kuwa fedha, wakati mwingine, ni fedheha na neema yaweza kuwa nakama.
Baya zaidi, mume alizoea kulalamika kwa wapambe wake kuwa mkewe anataka kumcontrol jambo ambalo liliwaudhi na kumpa ushauri mbaya kiasi cha kuanza kuharibu ndoa yake mwenyewe tokana na mafanikio aliyopata na mwenzie.
Jamaa alisahau kitu kimoja ambacho watu wengi wa namna hii hufanya.
Alisahau kuwa wakati akiwa hana kitu, hawa jamaa hawakuwapo ingawa walikuwa wanaishi sehemu moja.
Maskini hakujua kuwa wakati wa kupanda ndege walaji huwa hawaonekani shambani hadi mazao yaive waje kula na yakiisha watoweke! Hakujua kuwa angetokea kufilisika, ni mkewe peke yake angekuwapo kama alivyokuwapo wakati wa kutafuta.
Kitu kingine ambacho mwanaume alisahau ni kwamba, je kama mkewe naye angepata mashoga walaji na kukosa muda naye angefanya nini? Haya mambo, ukitaka yasikupe taabu, kila unalofanya, kabla ya kulifanya, jiulize, ningekuwa huyu ninayemtendea angekuwa mimi na mimi nikawa yeye, ningetaka anitendeeje? Hii ndiyo njia rahisi ya kujihukumu na kutumia kupima kila unalofanya.
Mfano, unapotaka kumuona mwenzio hakufai tena katika jambo lolote liwe dogo au kubwa, jiulize, ingekuwa mimi ningependa afanye nini? Je kama hakufai, wewe unamfaa? Je chanzo na matokeo ya tabia kama hizi ni nini? Unajua gharama za lile unalofanya kiasi cha kumkwaza mwenzako? Ulishajiuliza au kuvaa viatu vya mwenzako.
Vivae hata kimawazo lau mara moja, utajua anavyojihisi na changamoto unayomtengenezea.
Tokana na kutawaliwa na kuishi katika mfumo dume unaopendelea wanaume na uumiza wanawake, uzoefu wetu ni kwamba kuna baadhi ya wanaume wanaowachukulia wanawake kama si binadamu wanaoweza kuumia, kuudhika, hata kuudhi kama wao. Watu wa namna hii hawapendi kujilinganisha na wanawake kwa lolote.
Hivyo, hata wanapowaudhi au kuwaumiza wanawake, ni kutokana na kuwachukulia kama viumbe visivyo na hisia wala haki sawa na wao. Wanawake ni binadamu sawa na binadamu yeyote.
Wana ubora na udhaifu wao sawa na wengine.
Kwa kuzingatia usawa wa binadamu kimaumbile, kuna haja ya kufikiri upya namna tunavyowachukulia wanawake.
Japo si wote, wanawake wengi wana vifua vya kuvumilia kwa sababu mbali mbali ziwe za kujitakia au zilizo juu ya uwezo wao. Mfano, inapoyumba au kuvunjia ndoa, mwanamke ana nafasi kubwa ya kuumiza na kuumizwa kuliko mwamaume.
Chukulia wanandoa ambao wako kwenye miaka 50 kwenda juu. Kama mume na mke watakuwa na umri huu, ndoa inapovunjika, uwezekano wa mwanaume kupata mchumba haraka na kuoa hasa akiwa ana mali ni mkubwa kuliko mwanamke.
Hivyo, kwa kujua hili, wanawake wa umri huu wanaweza kulazimika kuvumila baadhi ya mambo ila si yote.
Hufikia mahali wakasema liwalo na liwe.
Je kuna haya ya kufanya hivyo wakati, mwisho wa siku, wote mnapata hasara na kuumia. Hata mkiachana mkaoa au kuolewa upya, bado kuna kipande cha maisha ambacho hakiwezi kusahaulika au pengo linaloweza kuzibika.
Katika kisa hiki, bahati nzuri sana, baba alijirekebisha baada ya kumruhusu mkewe amueleze anavyojisikia na namna ambavyo angependa mambo yawe.
Katika kujadili kadhia hii, mama alitumia neno moja kubwa lililombadilisha mumewe. Alisema “kabla ya kuwaona marafiki na wapambe zako ni wa maana kuliko mimi, jiulize, ungekuwa wewe ndo mimi na mimi ndiyo wewe, ungetaka nikutenze vipi mume wangu?” Neno kama wewe ungekuwa mimi lilidhoofisha mume na kuomba msamaha na kuachana na urafiki na upambe wa mashaka. Zaidi ya hapo, mama alimkumbusha walivyokuwa wapweke wakati wakitafuta utajiri ambao sasa ulikuwa unataka kuwatenganisha.