Prime
Shahidi asimulia mipango mauaji ya Milembe aliyekuwa mfanyakazi wa GGM

Wakili Lebaratus John anayemtetea mshtakiwa wa kwanza, Dayfath Maunga kwenye kesi ya mauaji ya aliyekuwa mfanyakazi wa Mgodi wa Dhahabu wa Geita (GGM), Milembe Selemani, akijadiliana na mteja katika Mahakama Kuu Kanda ya Geita jana Ijumaa Aprili12, 2024. Picha na Rehema Matowo
Muktasari:
- Shahidi aliyeandika maelezo adai mshtakiwa alikiri kukodi wauaji aliowalipa Sh2.6 milioni na maelezo hayo yamepokewa na Mahakama kama ushahidi.
Geita. Shahidi wa 11 wa upande wa Jamhuri katika kesi ya mauaji ya aliyekuwa mfanyakazi wa Kampuni ya uchimbaji Dhahabu Geita (GGM), Milembe Seleman, ameieleza Mahakama kuwa mshtakiwa wa kwanza, Dayfath Maunga, ndiye aliyekodi wauaji kwa malipo ya Sh2.6 milioni.
Shahidi huyo, Koplo Darius, ambaye ni askari polisi kutoka Idara ya Upelelezi Wilaya ya Geita, ametoa madai hayo jana Ijumaa Aprili 12, 2024.
Milembe (43), aliyekuwa mfanyakazi wa kitengo cha ugavi katika kampuni ya GGM aliuawa Aprili 26, 2023 kwa kukatwa na kitu chenye ncha kali sehemu mbalimbali mwilini, ikiwemo kichwani, usoni na mikononi.
Mbali ya Maunga (30), washtakiwa wengine katika kesi hiyo ya mauaji ni Safari Labingo (54), Genja Pastoy, Musa Lubingo (33) na Ceslia Macheni (55).
Kesi hiyo namba 39 ya mwaka 2023 inasikilizwa na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Geita, Kelvin Mhina.
Akiongozwa na Wakili wa Serikali, Merito Ukongoji kutoa ushahidi, Koplo Darius amesema yeye ndiye aliyemhoji Maunga baada ya kukamatwa.
Amesema katika mahojiano mshtakiwa alikiri kutenda kosa hilo, akieleza sababu na namna alivyowapata wauaji.
Koplo Darius pia aliwasilisha mahakamani kielelezo cha maelezo ya onyo, aliyodai ni ya mshtakiwa, aliyoyarekodi alipomhoji kuhusu tuhuma za mauaji hayo. Mahakama imepokea kielelezo hicho namba tisa cha upande wa mashtaka.
Mipango ya mauaji
Kwa mujibu wa maelezo hayo kama yalivyosomwa mahakamani na shahidi, mshtakiwa wa kwanza Dayfath, alikuwa akiishi na Milembe (marehemu kwa sasa) kama mume na mke kuanzia Juni 2020 na walikuwa wakifanya mapenzi ya jinsia moja.
Katika mahusiano hayo, inadaiwa Milembe alikuwa akimsaidia kusomesha mtoto wake na kusaidia ndugu zake.
Licha ya kuishi pamoja, inadaiwa katika maelezo hayo mshtakiwa alieleza siku zilivyoenda Milembe alianza kumnyanyasa, hivyo akataka kuondoka.
Hata hivyo, alidai kuwa alishindwa kutokana na vitisho kutoka kwa Milembe, kwamba alikuwa na picha zake za utupu.
Inadaiwa Februari 2023 (Dayfath) alimtafuta Safari Lubingo aliyekuwa akiuza nyanya wakaanzisha uhusiano wa kimapenzi.
Shahidi akirejea maelezo hayo, alidai Dayfath alimdanganya kuwa anaishi na wifi yake na kwamba, mume wake yuko Afrika Kusini, lakini wifi yake amekuwa akimbana kutumia mali za mume wake.
Inadaiwa Safari alimshauri kutumia waganga wa kienyeji lakini zilishindikana.
Shahidi alidai Machi 2023 Safari alimpigia simu (Dayfath) akitaka abadili njia na alimweleza amepata watu wa kushirikiana naye kutekeleza jambo hilo.
Safari inadaiwa alimweleza kuwa watu hao walidai walipwe Sh1.6 milioni lakini akasema ataongea nao. Baadaye alimpigia simu akidai wamekubali Sh1.2 milioni na akamtaka atume Sh200, 000 ili waanze kazi.
Dayfath inadaiwa aliwatumia watu hao picha ya Milembe na kuwaeleza akiwa Geita hulala nyumba ya wageni ya Ze Kisesa.
Shahidi amedai watu hao walienda kuchukua chumba katika nyumba hiyo, lakini walishindwa kutekeleza azma yao kutokana na mazingira.
Aprili 2023 inadaiwa Safari alimpigia simu Dayfath akitaka wakutane Sengerema.
Inadaiwa Dayfath alienda na akatambulishwa kwa watu wengine ambao ni Masumbuko, Genja na Musa na walimhakikishia watakamilisha kazi, hivyo akawapa tena Sh200,000.
Shahidi alidai kwa mujibu wa maelezo ya mshtakiwa, mwishoni mwa wiki Milembe alikuwa akirudi nyumbani Usagara, hivyo Dayfath alimpigia simu Genja (mshtakiwa wa tatu) akimtaka aende Mwanza na kwamba Jumatatu atamsindikiza Milembe hadi stendi ili akiwa anashuka, Genja asogee kwenye gari aombe lifti ya kurudi Geita.
Mpango huo inadaiwa ulifanikiwa na baada ya kupewa lifti, Genja alimpigia simu Dayfath na kumwambia ameshindwa kumuua Milembe kutokana na mazingira.
Hata hivyo, inadaiwa alimweleza wamebadilishana namba za simu na kumweleza Milembe amehama Ze Kisesa kwenda nyumba nyingine ya wageni, California iliyopo mjini Geita.
Aprili 24, 2023, inadaiwa Milembe alimpigia simu Dayfath akimweleza amepata mganga atakayemfanyia zindiko kwenye nyumba anazojenga na kwamba, amempa masharti ya kumtaka aende na chupa tupu za soda saba na maziwa freshi.
Inadaiwa walienda eneo la nyumba alizokuwa akijenga Mwatulole Maduka Matatu.
Aprili 25, 2023 Milembe alimpigia tena simu akimweleza mganga atamtengeneza mwili, kisha waende ‘saiti’.
Saa tano usiku wa siku hiyo, inadaiwa Dayfath alipigiwa simu na Safari Lubingo (mshtakiwa wa pili) akimweleza kuwa kazi yake imeisha na akamtaka amtumie Sh200,000, naye akazituma.
Asubuhi ya Aprili 26, 2023 inadaiwa Dayfath alimpigia simu Milembe akawa hapatikani, hivyo akaamini kazi imeisha.
Baada ya hapo alimtumia Safari Sh810,000 zilizokuwa zimesalia na kufanya jumla ya fedha alizompa kwa kazi ya kumuua Milembe kuwa Sh2.6 milioni.
Sababu za mauaji
Shahidi alidai mshtakiwa wa kwanza alitaja sababu za kufanya mauaji hayo ni kutokana na Milembe kumnyanyasa na kumpiga mara kwa mara.
Anadai pia alikuwa akimfungia chumbani alipokuwa akitoka bila kumuaga, hivyo alikuwa akitaka uhuru wake.
Pingamizi la kielelezo
Kabla ya kupokewa maelezo hayo kuwa kielelezo cha upande wa mashtaka, upande wa utetezi uliweka pingamiizi ukiiomba Mahakama isiyapokee.
Wakili wa utetezi, Liberatus John alidai mteja wake hakuandika maelezo hayo wala kuhojiwa Polisi Nyamagana, hakukiri kosa, na saini iliyotumika si yake.
Kutokana na pingamizi hilo, Mahakama iliendesha kesi ndogo ndani ya ile ya msingi, ili kujiridhisha na uhalali wa maelezo hayo. Pande zote ziliita mashahidi.
Baada ya Mahakama kusikiliza pande zote katika uamuzi wake Jaji ilitupilia mbali pingamizi la upande wa utetezi na kuamua kuyapokea maelezo hayo kuwa kielelezo cha tisa cha upande wa mashtaka.
Uamuzi ulifikiwa baada ya Jaji kusema amejiridhisha kuwa mshtakiwa alitoa maelezo hayo kwa hiyari.
Jaji Mhina ameahirisha kesi hiyo hadi kikao kingine kwa tarehe itakayopangwa na msajili baada ya muda uliokuwa umepangwa kumalizika.
Kesi hiyo ilikuwa imepangwa kusikilizwa kwa wiki moja mfululizo.
“Kwa kuwa bado upande wa Jamhuri haujamaliza kutoa ushahidi, kesi hii inaahirishwa hadi kikao kingine kitakachokaa mwishoni mwa Mei au mwanzoni mwa Juni mwaka huu,” amesema Jaji.