Shahidi aeleza Mahakama alivyozimia kwenye ajali iliyoua sita

Muktasari:
Mashahidi wawili wamefungua ukrasa wa ushahidi wa upande wa Jamhuri katika kesi ya Trafiki namba 27/2023, inayomkabili dereva, Oswald Binamungu (39) ambaye anadaiwa kuwagonga ‘wanajogging’ na kusababisha vifo vya watu sita na kujeruhi wengine tisa.
Mwanza. Mashahidi wawili wamefungua ukrasa wa ushahidi wa upande wa Jamhuri katika kesi ya Trafiki namba 27/2023, inayomkabili dereva, Oswald Binamungu (39) ambaye anadaiwa kuwagonga ‘wanajogging’ na kusababisha vifo vya watu sita na kujeruhi wengine tisa.
Mashahidi hao ambao ni Hotelia katika hoteli ya Adden Palace iliyopo Pasiansi wilayani Ilemela mkoani hapa, Peter Silikwa na Askari wa Polisi Kitengo cha Usalama barabarani, mwenye namba F.8489 Koplo Chipila (42) wametoa ushahidi wao leo Alhamisi Agosti 24, 2023 mbele ya Mahakama ya Wilaya ya Ilemela.
Oswald akiendesha gari yake aina ya Toyota Double Cabin Julai 22, mwaka huu anadaiwa kuwagonga kwa nyuma wana kikundi wa Adden Palace Jogging Club eneo la Kiseke na kusababisha vifo na madhara kinyume na Kifungu namba 40 (1), 63 (2) (a) na 27 (b) cha Sheria ya Usalama Barabarani namba 168 marejeo ya mwaka 2002.
Akiongozwa na Mwendesha Mashtaka wa Serikali, Anitha Mweli, shahidi wa kwanza wa Jamhuri, Peter Henry Silikwa ambaye ni miongoni mwa majeruhi katika ajali hiyo ameieleza Mahakama kuwa aliburuzwa na gari hiyo hadi akazimia, alipozinduka alishuhudia miili ya wana kikundi wenzake ikiwa pembeni mwa barabara.
Huku akiwa na jeraha kichwani, Silikwa amesema baada ya dakika kadhaa kupita maofisa wa Polisi walifika wakamchukua kwenda kituoni kupatiwa PF3 na kupelekwa katika hospitali ya Wasabato iliyoko Pasiansi kisha Sekou Toure ambako alilazwa siku tatu kisha kuruhusiwa.
Wakati Sikilwa akitoa maelezo hayo, shahidi wa pili ambaye ni askari (Trafiki) mwenye namba F.8489 Koplo Chipila ameieleza Mahakama kuwa baada ya kuchora ramani ya tukio alibaini wanajogging hao walikuwa wakikimbia upande wa kushoto wakati waenda kwa miguu wanatakiwa kupita upande wa kulia wa barabara.
Koplo Chipila alipoulizwa na Wakili wa utetezi, Linus Amri iwapo kikundi hicho kilikuwa kimesajiliwa, Koplo Chipila amesema hakikuwa kimesajiliwa wala wanachama wake hawakuvaa viakisi mwanga (Reflector) ambazo zinaelekezwa kuvaliwa na wafanya mazoezi wanapopita barabarani au kuongozwa na Ofisa wa Polisi (Trafiki).
Hii ni sehemu ya ushahidi huo ikijumuisha maswali ya waendesha mashtaka wa Serikali, Monica Mweli na Mwanahawa Changale, mawakili wa utetezi, Linus Amri na Steven Kitale dhidi ya shahidi ambaye ni Hotelia, Peter Silikwa na F.8489 Koplo Chipila.
Monica Mweli: Tueleze tarehe 22/7/2023. Saa 3 ulikuwa wapi na ukifanya nini?
Shahidi: Kwa kumbukumbu tarehe 22/7/2023 ilikuwa asubuhi mapema tulikuwa tunafaya mazoezi ya Jogging kukimbia barabarani.
Monica: Mlikuwa watu wangapi?
Shahidi: Kundi la watu kuanzia 27 hadi 30
Monica: Umesema group la watu 27 mpaka 30, tuambie kikundi chenu kinaitwaje?
Shahidi: Kinaitwa Adden Palace Jogging Club
Monica: Unasema mlikuwa mnakimbia, tueleze mlikuwa mnatoka wapi kwenda wapi?
Shahidi: Tulikutana Saa 12 asubuhi ratiba ilikuwa kukimbia barabara ya Kiseke kuelekea Nsumba
Monica: Utaratibu ukoje sasa kabla ya kuanza kukimbia?
Shahidi: Ratiba ilikuwa imeshapangwa, kwamba tunaingia barabarani kwa kuongozwa na viongozi wawili ambao tunakimbia nao
Monica: Unasema mnaongozwa na viongozi wawili, ni kina nani hao?
Shahidi: Anayekuwa mbele anaitwa, Gregory anayekuwa nyuma anaitwa Mfungo Mathias
Monica: Mkiwa mnaongozwa na viongozi hao nini kiliwatokea?
Shahidi: Baada ya kuanza kukimbia katika barabara ya Kiseke kuelekea Nsumba, tulipofika maeneo ya Kituo kinachoitwa Mzambarauni, ndipo ajali ilipotokea,
Monice: Ni ajali gani iliyotokea?
Shahidi: Ni ajali ya gari, ambapo tuliburuzwa,
Monica: Mliburuzwa vipi?
Shahidi: Baada ya ajali kutokea tulishangaa tukiburuzwa na gari ndipo mimi nilipoanguka na kupasuka kichwa.
Monica: Uliburuzwa vipi?
Shahidi: wakati tunakimbia tulikuwa kwenye mstari wa watu watatu watatu tumejipanga. Alianza Kuburuzwa mwenzangu anayeitwa Shadrack.
Monica: Ieleze Mahakama kitu gani kiliwaburuza?
Shahidi: Niliburuzwa na gari ambalo lilitokea nyuma yetu.
Monica: Wakati mnakimbia mkaburuzwa kwenye barabara mlikuwa upande gani?
Shahidi: Upande wa kushoto
Monica: Unasema mliburuzwa na gari, ulifanikiwa kuiona gari?
Shahidi: Sikufanikiwa kwa sababu baada ya kuburuzwa nilianguka chini na kupoteza fahamu.
Monica: Baada ya kuanguka chini nini kilitokea?
Shahidi: Baada ya kuzinduka ndipo nilipoona damu zikitiririka nyingi sana maeneo ya kichwani
Monica: Ukiwa na hali hiyo, nini ulikifanya?
Shahidi: Baada ya kuzinduka, niliona wenzangu wakiwa wamelala chini, sehemu ya mifupa yao ikiwa imevunjika na kuonekana, wengine wakiwa wamekufa.
Monica: Nini kiliendelea baada ya kuona hali hiyo kwako na wenzio?
Shahidi: Nilipatiwa msaada kutoka kwa mwezangu anayeitwa Mfungo Mathias, kisha nikaona Askari wa Usalama barabarani akifika eneo la tukio.
Monica: Baada ya kuwaona askari nini kingine kilitokea?
Shahidi: Baada ya hapo Mfungo Mathias akanisaidia kupata usafiri wa kunipeleka hospitalini.
Monica: Ni Hospitali gani ulienda kwa ajili ya matibabu?
Shahidi: Ni hospitali ya Wasabato iliyoko Pasiansi.
Monica: Wakati unapatiwa matibabu nini kilitokea?
Shahidi: Daktari aliniambia kwamba nimeumia sehemu za kichwa, hivyo nastahili kushonwa baada ya hapo nikahamishiwa Hospitali ya Sekou Toure kwa matibabu zaidi.
Monica: Wakati unafika Sekou Toure, nini kilifanyika?
Shahidi: Nilifanyiwa uchunguzi wa kichwa kwenye eneo niliposhonwa na nikalazwa kwa siku tatu.
Monica: Wakati unaenda hospitali ulienda na kitu gani?
Shahidi: Nilikuwa na Fomu namba Tatu (PF3) niliyopewa Polisi kwa ajili ya kwenda kupatiwa matibabu.
Monica: Baada ya hizo siku tatu nini kilitokea?
Shahidi: Baada ya kupatiwa huduma kwa siku tatu, Daktari aliniruhusu kutoka hospitalini.
Wakili wa Utetezi, Linus Amri akamuuliza maswali shahidi;
Linus: Shahidi nakuuliza maswali machache ujibu Ni Kweli au Si Kweli
Shahidi: Ni kweli hujaeleza ilikuwa asubuhi saa ngapi?
Shahidi: Sikumbuki
Linus: Ni kweli hujaeleza gari iliyokugonga ilikuwa inafananaje na ilikuwa na mtu gani?
Shahidi: Sijaeleza
Linus: Ni kweli Hujaeleza Adden Palace Jogging inawanachama wangapi?
Shahidi: Nimeeleza wanachama 25-30
Linus: Nikweli hujatoa kielelezo chochote kinachoonyesha kwamba Adden Palace ina wanachama wangapi?
Shahidi: Sijatoa.
Linus: Ni kweli hujaeleza mahakamani, kipindi unakimbia ulikuwa upande gani wa barabara na gari?
Shahidi: Nimeeleza nilikuwa upande wa kushoto
Linus: Umeeleza kuwa umeburuzwa, ilikuburuza ukiwa kushoto au kulia?
Shahidi: Nilikuwa kushoto wakati gari inaniburuza
Linus: Ni kweli upande wako wa kushoto ulipokuwa kulikuwa na mistari mingine ya wakimbiaji?
Shahidi: Mistari hiyo ilikuwa miwili upande wa kulia
Linus: Ni kwei hukuona gari inakuja wala hukuona gari inaondoka?
Shahidi: Ni kweli
Linus: Ni kweli barabara mliyokuwa mnakimbilia, ina sehemu ya watembea kwa miguu na sehemu ya magari?
Shahidi: Sikumbuki
Linus: Ni kweli mlipokuwa mnakimbilia ilikuwa ni sehemu ya barabarani kwa wingi wenu? Mlikuwa mnakimbia katikati ya barabara?
Shahidi: Si kweli, ilikuwa pembeni ya barabara katikati ni kwenye eneo la mstari
Linus: Barabara ya Kiseke ina mstari?
Shahidi: Ndiyo
Linus: Ni kweli barabara ya Kiseke ina kingo ndefu za barabarani?
Shahidi: Sikumbuki
Linus: Una ugonjwa wa kusahau au kuona shahidi?
Shahidi: Sina
Linus: Kwa hiyo ni kweli hukuona kingo za Barabara ukiwa unakimbia?
Shahidi: Sikumbuki
Linus: Ni kweli majeruhi yako unaposema ulivuja damu, gari haikukugonga wala kukugusa?
Shahidi: Gari haikunigusa moja kwa moja
Linus: Kwa hiyo gari haikukugonga wewe moja kwa moja?
Shahidi: Iliniburuza, haikunigonga.
Linus: Unajua maana ya kuburuza?
Shahidi: Ndiyo ni kupitiwa na gari.
Linus: Kwa hiyo gari haikukugonga ilikuburuza?
Shahidi: Ndiyo
Linus: Adden Palace jogging ina kibali cha Jogging?
Shahidi: Hapana
Linus: Ni kweli kipindi mnakimbia mkitoka Adden Palace Hoteli, hamkukutana na Trafiki barabarani?
Shahidi: Ni kweli
Linus: Na ilikuwa wazi panaonekana?
Shahidi: Ni kweli
Linus: Na mlivyokuwa mnapita kwenda kiseke mlipita barabara ya Sabasaba wala hamkuona Trafiki?
Shahidi: Ni kweli
Linus: Ni kweli kwa kuwa hamjasajiliwa, hamjui taratibu za kufuata kabla ya kuanza kukimbia?
Shahidi: Tulifundishwa na viongozi
Linus: Hao viongozi wamesajiliwa?
Shahidi: Sikumbuki
Linus: Ni kweli kama Klabu haijasajiliwa hata ruti ya Kiseke ilikuwa haijsajiliwa?
Shahidi: sikumbuki
Linus: Ni kweli umesema umeburuzwa na gari, hujaieleza mahakama gari ilikuwa na mwendo wa aina gani?
Shahidi: Sikuweza kuona mwendo wa gari
Linus: Idadi ya wanawake waliokuwa wanakimbia unaijua? na wanaume?
Shahudi: Sikumbuki.
Wakili Steven Kitale anaingia kumuuliza Shahidi maswali;
Kitale: Shahidi pole kwanza kwa ajali
Shahidi: Asante
Kitale: Shahidi unaweza kutueleza elimu yako?
Shahidi: Elimu yangu ni kidato cha nne
Kitale: Shahidi umeeleza kuwa mlikuwa mnakimbia mistari mitatu, ila hujaeleza ulikuwa mstari wa ngapi?
Shahidi: Ni kweli
Kitale: Ni kweli hujaeleza mahakamani hiyo mistari ilikuwa mingapi?
Shahidi: Ni kweli
Kitale: Ni kweli kwamba hujaieleza mahakama kama uliona wenzako walipokuwa wanagongwa?
Shahidi: Sikumbuki
Kitale: Shahidi tusaidie, hii jogging klabu yenu inamilikiwa na nani?
Shahidi: Kikundi cha wanamichezo, haina mmiliki
Kitale: Unaweza kutuelezea kiongozi wa hicho kikundi ni nani?
Shahidi: Anaitwa Selestine jina la pili sikumbuki.
Kitale: Anafanya kazi gani?
Shahidi: Alikuwa mfanyakazi wa Adden Palac Hotel alifariki katika ajali hiyo
Kitale: Ni kweli umeeleza kuwa wakati unaenda hospitai ulipewa PF3 ila hujaeleza ilikufikiaje?
Shahidi: Ni kweli
Kitale: Sina swali lingine mheshimiwa Hakimu (Amani Sumari).
Hakimu: Shahidi asante, unaweza kuondoka, mwendesha mashtaka mlete shahidi wa pili.
Shahidi wa Pili: F.8489 Koplo Chipila (42) anawasili mahakamani na kupanda kizimbani kutoa ushahidi wake akiongozwa na Mwendesha Mashtaka wa Serikali, Mwanahawa Changale;
Changale: Shahidi tueleze unafanya kazi gani?
Shahidi: Ni Askari polisi wa kitengo cha Usalama barabarani kwa miaka saba sasa.
Changale: Kazi yako ni nini?
Shahidi: Kusimamia sheria za usalama barabarani, ikiwemo kuvusha watoto na watu wasiyojiweza.
Changale: Julai 22, 2023 Saa 12 asubuhi ulikiuwa wapi?
Shahidi: Nilikuwa kituo cha Polisi Kirumba.
Changale: Nini kiliendelea?
Shahidi: Nilipofika maeneo ya Sabasaba, nilipigiwa simu na Afande wangu akiniambia niende maeneo ya Kiseke kuna ajali.
Changale: Saa ngapi ulifika Sabasaba na kwa nini ulikuwa sabasaba?
Shahidi: Ilikuwa Saa 12:30 ni eneo la kazi nililopangiwa.
Changale: Unasema ukiwa pale nini kilitokea?
Shahidi: Nilienda eneo la tukio barabara ya Kiseke
Changale: Barabara ya Kiseke eneo gani?
Shahidi: Kiseke 'A'
Changale: Baada ya kufika ulikuta nini?
Shahidi: Nilikuta watu wengi wamejaa Barabarani, upande wa kushoto kuna watu wamelala
Changale: Hao waliokuwa wamelala walikuwa katika hali gani?
Shahidi: Walikuwa wameshafariki
Changale: Walikuwa watu wangapi?
Shahidi: Walikuwa watano
Changale: Nini kingine ulichokikuta?
Shahidi: Nilikuta damu nyingi barabarani na wengine wakiwa wana majeraha, nikamjulisha Afande DTO (Mkuu wa Trafiki Wilaya ya Ilemela), Beatus.
Changale: Nini kiliendelea?
Shahidi: Afande aliniambia nikague eneo na kutafuta shuhuda mmoja, kisha nikachora mchoro wa eneo la ajali.
Changale: Huyo shuhuda anaitwa nani? Na alikueleza nini?
Shahidi: Anaitwa Mfungo, nilimkuta eneo la tukio, akanielekeza jinsi ya kuchora ramani ya ajali ilivyotokea.
Changale: Unaposema alikuwa anakuelekeza unamaanisha nini?
Shahidi: Alinionyesha.
Changale: Umesema ulikuta miili ya watu waliokufa, ilikuwa eneo gani?
Shahidi: Niliikuta miili yote mitano ikiwa nje ya barabara, yaani nje ya vitofali vilivyowekwa kando ya barabara.
Changale: Pembeni ya barabara upande gani?
Shahidi: Upande wa kushoto
Changale: Baada ya kuchora ramani, ulibaini ajali imesababishwa na nini?
Shahidi: Shuhuda aliniambia gari ilisababishwa na gari
Changale: Wakati unachora ramani, tuambie kuhusu gari?
Shahidi: Shuhuda mmoja alisema gari hiyo imeegeshwa kwenye kituo cha mafuta eneo la Nsumba.
Changale: Baada ya kuchora ramani, uliipeleka wapi na utaitambuaje?
Shahidi: Niliipeleka kwa DTO, na ina mwandiko wangu, sahihi yangu na sahihi ya shuhuda na mtuhumiwa.
Changale: Ieleze Mahakama kuna umbali gani kutoka ajali ilipoanzia hadi ulipowakuta waathiriwa?
Shahidi: kwenye ramani inaonekana, kutoka ajali ilipoanzia hadi watu walipoangukia ni futi 30 na kutoka ajali ilipotokea mpaka mtu wa mwisho alipoangukia ni futi 240
Changale: Nini unaiomba Mahakama kuhusu ramani hiyo?
Shahidi: Naomba ipokelewe kama kielelezo mbele ya Mahakama katika kesi hii.
Changale: Kwa kuuona huo umbali wewe unapata nini, inakusaidia nini?
Shahidi: Unaweza kueleza kuwa dereva alikuwa spidi au hakuwa spidi
Changale: Tueleze alikuwa spidi au hakuwa spidi
Shahidi: Dereva alikuwa spidi
Changale: Kwa mujibu wa hiyo ramani hao watu waliogongwa walikuwa upande upi wa barabara?
Shahidi: Upande wa kushoto.
Changale: Kwenye ramani nani alisaini?
Shahidi: Saini yangu na askari aliyenisaidia, shuhuda na saini ya dereva wa gari ambaye mimi sikumsainisha kwa sababu hakuwepo eneo la tukio.
Changale: Unaweza kutueleza nini kuhusu saini ya dereva katika ramani hiyo?
Shahidi: Mimi kusema ukweli sikumsainisha, hivyo sielewi kilichotokea
Upande wa Utetezi ukiongozwa na Wakili, Linus Amri na Steven Kitale wanaanza kumuuliza shahidi wa pili (Koplo Chipila) maswali.
Linus Amri: Watembea kwa miguu wanaongozwa na sheria gani?
Shahidi: Sijui
Linus: Na wakimbia kwa miguu wanaongozwa na sheria gani?
Shahidi: Sijui
Linus: Ni kweli hujaeleza umesaini OB Kituoni saa ngapi?
Shahidi: Ni kweli
Linus: Hujaeleza kituo cha kazi ulifika saa ngapi?
Shahidi: Nimeeleza Saa 12
Linus: Kutoka Sabasaba kwenda Kiseke kuna umbali gani?
Shahidi: Sijui
Linus: Ulishawahi kupita barabara ya Kiseke? Ina mistari katikati?
Shahidi: Ndiyo nilishawahi, barabara ina mistari
Linus: Kwenye ramani yako umeweka Mistari?
Shahidi: Ndiyo
Linus: Kwa uelewa wako, watu wanaruhusiwa kukimbia barabarani?
Shahidi: Ndiyo
Linus: Ili watu wakimbie barabarani wanatakiwa wawe na vitu gani?
Shahidi: Wanatakiwa wapite sehemu ya watembea kwa miguu
Linus: Watembea kwa miguu wanatakiwa wapitie upande gani wa barabara?
Shahidi: Watembea kwa miguu wapite kulia na vyombo vya moto vipitie kushoto
Linus: Ni kweli ambapo miili ilikutwa haikuwa sehemu sahihi ambapo watembea kwa miguu wanatakiwa kupita?
Shahidi: Ni kweli
Linus: Zile kingo za barabarani ni kubwa kiasi cha mtu akiwa anakimbia anaweza kujikwaa?
Shahidi: Ni kweli
Linus: Ni kweli kwa wingi wa wale watu waliokuwa wanakimbia, zile kingo zinaweza kuwaumiza?
Shahidi: Si kweli
Linus: Ni kweli kwamba zile kingo zinaweza kumuumiza mtu akijikwaa?
Shahidi: Ni kweli
Linus: Ni kweli watembea kwa miguu hawaruhusiwi kupita sehemu ya watembea kwa miguu na pale kulikuwa na Zebra?
Shahidi: Wakati mwingine wanaruhusiwa, lakini kama hamna Zebra wanaweza kuruhusiwa na askari
Linus: Ni kweli futi haipimi spidi (Kasi) ya gari?
Shahidi: Futi inapima urefu wa ajali siyo spidi
Linus: Shahidi ni kweli kivuli kinatokana na kitu?
Shahidi: Ni kweli
Linus: Ni kweli ulipata kivuli pasipokuwepo gari?
Shahidi: Ni kweli
Linus: Ni kweli kwamba kwenye kielelezo P1 (ramani) hakikuwa na saini ya mshtakiwa ila umeiona hapa mahakamani?
Shahidi: Ni kweli
Linus: Ni kweli saini hii imejazwa na mtu mwingine bila kuwepo mchora ramani?
Shahidi: Ni kweli
Linus: Ni kweli kwa kuwa hii saini hukuwepo kuna uhalisia wa maandishi kubadilika kwenye kielelezo ambacho hukuwa nacho?
Shahidi: Ni kweli
Linus; Ni kweli hujaieleza mahakama kuwa kielelezo hiki kilikuwa kimetunzwa na nani na ulimkabidhi nani?
Shahidi: Ni kweli
Linus: Ni kweli hujawahi kuitwa kusaini maelezo ya nyongeza katika kielelezo hiki wala hakuna jina la dereva?
Shahidi: Ni kweli
Linus: Ni kweli hujaeleza ulipokuwa hakuna magari mengine yaliyopita?
Linus: Ulifanikiwa kuiona miili ya watu wale ila hujaelez ilikuwa na hali gani?
Shahidi: Daktari ndiyo anayeweza kueleza
Linus: Ni kweli gari lilikuwa bovu?
Shahidi: Ni kweli
Linus: Ni kweli gari lilikuwa haliwezi kutembea lenyewe?
Shahidi: Ni kweli
Linus: Kwa kuwa lilikuwa haliwezi kutembea, basi lilikuwa bovu?
Shahidi: Si kweli
Linus: Ulilikagua?
Shahidi: Sikulikagua
Linus: Ni kweli gari ilikuwa mbovu kwa muonekano?
Shahidi: Ndiyo
Linus: Ni kweli wakati unakabidhi gari kituoni, uliondoka nayo eneo la tukio ikiwa mbovu?
Shahidi: Ni kweli
Linus: Ulimkabidhi gari nani?
Shahidi: DTO
Linus: Ulimkabidhi gari bovu au zima?
Shahidi: Gari lilikuwa bovu.
Wakili wa utetezi, Kitale anaingia kumuuliza Shahidi (Trafiki)
Kitale: Unaweza kueleza elimu yako na ulipata ufaulu gani?
Shahidi: Kidato cha nne na nilipata Dsaraja la tatu.
Kitale: Hii ramani uliichora saa ngapi na kumaliza Saa ngapi?
Shahidi: Nilianza Saa 12:35 na kumaliza Saa 1 kamili asubuhi
Kitale: Ajali ilitokea Saa ngapi?
Shahidi: Ajali ilitokea Saa 1: 40 asubuhi
Kitale: Uchunguzi wa gari ulifanyika kabla au baada ya kuitoa eneo la ajali?
Shahidi: Baada
Kitale: Hujaeleza kama uliona mtu yoyote alikuwa amevaa kiakisi mwanga (reflector)?
Shahidi: Sijaeleza
Kitale: Ni kweli hujaeleza kuwa hizo namba za gari ulizitoa wapi kisha ukazijaza kwenye ramani?
Shahidi: Ni kweli
Kitale: Tueleze shahidi ulizitoa wapi hizo namba za gari?
Shahidi: Koplo Ombeni ndiyo alienda ilipokuwa gari, akanijulisha nikajaza.
Kitale: Ni kweli kwenye ramani yako kwamba hujamweka Koplo Ombeni kwamba alikusaidia?
Shahidi: Si kweli, nilimweka askari, D.8833 Koplo Ombeni
Kitale: Ni kweli klabu za jogging lazima ziwe na vibali zinapotaka kufanya mazeoezi barabarani?
Shahidi: Sifahamu
Kitale: Ni kweli hufahamu kwamba wafanya mazoezi wanatakiwa kuwa na ramani za route wanapotaka kuifanya hivyo ili wapewe ulinzi?
Shahidi: Ni kweli
Kitale: Ni kweli hujaieleza mahakama kama mlichukua ushahidi wa video au kulikuwa na Camera eneo la tukio?
Shahidi: Ni kweli
Ni kweli hujaeleza mahakamani iwapo uliona mtu mwenye kibendera au kulikuwa na kibendera eneo la tukio?
Shahidi: Ni kweli
Kitale: Ni kweli Kwenye ramani yako haionyeshi kama gari iliburuza?
Shahidi: Ni kweli
Kitale: Ni kweli hufahamu kwamba marehemu walikuwa wamehamishwa eneo walilopatiwa ajali na kuwekwa pembeni?
Shahidi: Sifahamu
Kitale: Na kwenye ramani yako hujaonyesha kama kulikuwa na damu au kitu kinachofanana na damu?
Shahidi: Ni kweli
Kitale: Ni kweli hujaeleza hiyo gari ilikuwa na kasi gani?
Shahidi: Ni kweli
Kitale: Ramani yako inaonesha majeruhi ni wangapi?
Shahidi: Haioneshi
Kitale: Ni sahihi kusema kwamba hakukuwa na majeruhi?
Shahidi: Si sahihi
Kitale: Uliwaona?
Shahidi: Niliwaona wakiwa ndani ya gari wanaondoka
Kitale: Walikuwa wangapi?
Shahidi: Niliyemuona ni mmoja tu.
Kitale: Mheshimiwa sina swali jingine.
Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Wilaya ya Ilemela, Amani Sumari ameahirisha shauri hilo hadi Septemba 5, mwaka huu saa 4:30, itakapoitwa kwa ajili ya kuendelea na shahidi wa tatu wa jamhuri huku mshtakiwa akiwa nje kwa dhamana.