Miili ya waliofariki kwa kugongwa na gari mazoezini yatambulika

Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Gideon Msuya akionyesha gari iliyowagonga wakimbiaji wa kikundi cha Adden Palace Hotel na kusababisha vifo vya watu sita huku 16 wakijeruhiwa. Picha na Mgongo Kaitira
Muktasari:
Majeruhi saba wa ajali hiyo wanaendelea kupatiwa matibabu katika Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Mwanza Sekou-Toure wakati wengine wanane wakiamishiwa Hospitali ya Rufaa ya Kanda Bugando kwa matibabu zaidi.
Mwanza. Watu sita waliofariki dunia kwa kugongwa na gari wakati wakifanya mazoezi jijini Mwanza wametambulika.
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Gideon Msuya amewataja waliofariki kwenye ajali hiyo iliyotokea Saa 12:30 alfajiri leo Julai 22, 2023 kuwa ni Peter Fredrick, Shadrack Safari, Celestine Daud, Hamisi Waziri, Aman Matinde na Makolongo Manyanda.
Watu sita kati ya 16 waliojeruhiwa katika ajali hiyo iliyohusisha gari ndogo aina ya Toyota Hilux Double cabin iliyowaparamia wakimbiaji wa kikundi cha mazoezi cha Hoteli ya Added Palace ya jijini Mwanza wametambuliwa kuwa ni Magnus Masanja (26), mkazi Wa Isamilo, Godfrey Benard (25-30), Remidius Pontian (24), Grace Dickson (30), mkazi Wa Iloganzala, Husein Hassan (20) na mtoto mwenye umri wa miaka miwili, Baraka Jeremiah.
Ajali hiyo iliyoibua hofu miongoni mwa vikundi vya wakimbiaji jijini Mwanza imetokea katika eneo la Lumala barabara ya Kiseke Wilaya ya Ilemela mkoani Mwanza.
Wanakikundi cha Added Palace hotel Jogging Club hufanya mazoezi ya kukimbia katika barabara kila Jumamosi kwa lengo la kujiweka sawa kimwili na kiafya.
Kikundi hicho cha mazoezi kinaundwa na wafanyakazi wa Adden Palace hotel, wateja na wananchi wanaoishi jirani na hoteli hiyo iliyopo eneo la Iloganzara.
Kwa mujibu wa Kaimu Kamanda Msuya, dereva wa gari iliyohusika katika ajali hiyo alitoroka baada ya kulitelekeza gari katika kituo cha mafuta kilichoko jirani na eneo la tukio na jitihada za kumsaka zinaendelea.
"Jeshi la Polisi linamsaka dereva wa gari hiyo ili achukuliwe hatua za kisheria," amesema Kaimu Kamanda Msuya
Majeruhi saba wa ajali hiyo wanaendelea kupatiwa matibabu katika Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Mwanza Sekou-Toure wakati wengine wanane wakiamishiwa Hospitali ya Rufaa ya Kanda Bugando kwa matibabu zaidi.