SH81 bilioni kuwezesha mizani 90 kupima magari kwenye mwendo

Waziri Innocent Bashungwa akizungumza na watendaji baada ya kukagua utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa mizani inayopima magari yakiwa kwenye mwendo eneo la Rubana Wilaya ya Bunda. Picha na Beldina Nyakeke.
Muktasari:
Serikali imepanga kutumia zaidi ya Sh81 bilioni kuboresha mizani 90 ya magari katika maeneo mbalimbali nchini.
Bunda. Serikali imepanga kutumia zaidi ya Sh81 bilioni kuboresha mizani 90 ya magari katika maeneo mbalimbali nchini.
Akizungumza mara baada ya kukagua utekelezaji wa mradi wa mizani ya kupima magari yakiwa kwenye mwendo unaotekelezwa eneo la Rubana Wilaya ya Bunda, Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa amesema maboresho hayo yanatarajiwa kufanyika kuanzia mwaka wa fedha wa 2024/25 hadi 2026/27.
Pamoja na mambo mengine, Waziri Bashungwa amesema maboresho hayo yatausu kufunga mitambo ya kisasa yenye uwezo wa kupima magari yakiwa kwenye mwendo, kipaumbele zaidi ikiwa ni kwenye mizani yenye misongamano ya magari ya mizigo.
"Nimeagiza tathmini ifanyike katika mizani yote na tayari tumeamua kufanyia marekebisho ya mizani 90 kuongeza ufanisi," amesema Bashungwa
Amesema maboresho hayo yataondoa tatizo la msongamano wa magari kwenye mizani ambayo siyo tu ni usumbufu kwa wadau, bali pia huathiri uchumi kwa watu kupoteza muda mrefu kusubiri kupima uzito wa magari badala ya kufanya shughuli za uzalishaji mali.
"Magari kupanga foleni kwa muda mrefu kwenye mizani huchelewesha mzunguko wa biashara; Serikali imepanga kuondoa tatizo hili,’’ amesisitiza
Kuhusu ulinzi wa ubora wa miundombinu ya barabara, Waziri Bashungwa amewataka wadau wa usafirishaji kuzingatia sheria na kununi za usalama barabarani na upakiaji wa mizigo kulingana na uzito stahiki.
Awali, Mkurugenzi wa Miradi wa Wakala wa Barabara Nchini (Tanroads), Boniface Mkumbo alimweleza Waziri Bashungwa kuwa utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa mizani ya Rubana unaogharimu zaidi ya Sh22 bilioni umefikia asilimia 77.
‘’Mkandarasi tayari amelipwa zaidi ya Sh16.2 bilioni na kazi hii inatarajiwa kukamilika ifikapo Desemba, mwaka huu,’’ amesema Mkumbo