Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Vituo vya CNG kufikia 12 mwishoni mwa 2025

Muktasari:

  • Hadi sasa, vituo vinane vinafanya kazi na vinne viko hatua za mwisho kukamilika. Serikali pia inapanga kuongeza vituo hadi 20 kufikia Juni 2026.

Dar es Salaam. Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) limesema kuwa ifikapo mwisho wa mwaka huu, vituo 12 vya gesi asilia iliyosindikwa (CNG) vitakuwa vinafanya kazi kwa uwezo kamili.

Hatua hiyo inalenga kukabiliana na ongezeko la mahitaji ya nishati safi, sambamba na kupunguza msongamano wa magari unaosababisha foleni ndefu katika vituo vya mafuta.

Mhandisi Mwandamizi kutoka Kampuni ya Gesi (GASCO), Hassan Temba, amesema kuwa matumizi ya gesi asilia iliyosindikwa (CNG) siyo tu hatua muhimu kuelekea matumizi ya nishati safi, bali pia ni fursa ya mabadiliko makubwa kwa watumiaji na wawekezaji.

Akizungumza na Mwananchi leo, Julai 3, 2025 katika Maonyesho ya 49 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (DITF), maarufu kama Sabasaba, Temba amesema kuwa CNG ni kichocheo kikuu cha ukuaji wa biashara na uwezeshaji wa kiuchumi.

Ameongeza kuwa, kwa kuwa GASCO ni kampuni tanzu ya TPDC, inatazama CNG kama njia ya kufungua fursa kwa wajasiriamali wa ndani kuwekeza katika sekta ya nishati, hivyo kuchangia katika kujenga mustakabali wa kijani wa Taifa.

“Kutokana na dhamira ya TPDC ya kupanua miundombinu ya CNG, vituo vinane tayari vinafanya kazi, huku vinne vingine vikiwa katika hatua za mwisho za kukamilika,” amesema Temba.

Amesema maendeleo hayo yanatarajiwa kupunguza kwa kiasi kikubwa msongamano katika vituo vya mafuta, sambamba na kuharakisha matumizi ya gesi hiyo nchini kote.

Temba amesema vituo vilivyopo maeneo ya Mbezi–Tangi Bovu, IPTL, na Goba tayari vimekamilika kwa asilimia 80, na kinachosubiriwa ni kazi ndogo za miundombinu kabla ya kuanza kuhudumia wateja.

“Sisi kama TPDC tumekamilisha sehemu yetu ya miundombinu kwa vituo hivyo vinne. Kazi iliyobaki sasa ni kwa wawekezaji kumalizia upande wao na muda si mrefu vituo hivyo vitaanza kazi rasmi,” amefafanua Temba.

Tangu kuzinduliwa kwa kituo cha kwanza cha TPDC cha CNG, mwitikio kutoka kwa wananchi umekuwa mkubwa, huku Temba akiamini kuwa ndani ya miaka miwili, foleni ya magari itakuwa historia.

“Kumekuwa na mabadiliko katika tabia za matumizi ya nishati na kadri watu wengi wanavyohamia kwenye CNG, tutaendelea kushuhudia faida kama muda mfupi wa kujaza gesi, kupungua kwa hewa chafu, na usalama mkubwa wa nishati,” amesema.

Hayo yanaelezwa wakati ambapo taarifa ya Wizara ya Nishati inaonyesha kuwa hadi Aprili 2025, jumla ya vituo tisa vya kujazia gesi asilia kwenye magari (CNG) vilikuwa tayari vimekamilika na vinafanya kazi, ikilinganishwa na vituo viwili pekee vilivyokuwepo katika mwaka wa fedha 2020/21.

Kwa mujibu wa Waziri wa Nishati ambaye pia ni Naibu Waziri Mkuu, Dk Doto Biteko, alipowasilisha bajeti ya wizara hiyo bungeni, Serikali imepanga kuongeza idadi ya vituo hivyo hadi kufikia 20 ifikapo Juni 2026, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kukuza matumizi ya nishati mbadala.

Ameeleza kuwa kuimarika kwa matumizi ya gesi hiyo, hususan kwenye magari na bajaji, kumeleta manufaa kwa wananchi, yakiwemo kupunguza gharama za uendeshaji wa vyombo hivyo na kupunguza utegemezi wa fedha za kigeni kwa ajili ya kuagiza mafuta kutoka nje ya nchi.

“Ili kuendelea kuweka urahisi, Serikali kupitia TPDC inaendelea na taratibu za ununuzi wa vituo sita vya CNG vinavyohamishika, ambapo vitatu vitakuwa katika Jiji la Dar es Salaam, kimoja Morogoro na viwili Dodoma,” alisema Dk Biteko.