Sh800 milioni kujenga kiwanda cha cocoa Kyela
Muktasari:
- Kwa sasa wakulima wanapaswa kujipanga kuzalisha cocoa kwa tija na ubora ili kuweka ushindani wa soko ndani na nje ya nchi
Mbeya. Wakati Chama Kikuu cha Ushirika (Kyela) kikitarajia kutumia zaidi ya Sh800 milioni kwenye ujenzi wa kiwanda cha kuchakata cocoa, wakulima wilayani humo wamesema hatua hiyo itafungua fursa za kiuchumi na uhakika wa bei.
Pia, wamepongeza sera ya mgombea urais wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Samia Suluhu Hassan aliyeahidi Serikali kuongeza nguvu katika ujenzi wa kiwanda hicho iwapo atabaki madarakani.
Septemba 4 mwaka huu, akiwa Viwanja vya Old Airport jijini humo kwenye ziara yake ya kampeni, Samia alisema Mbeya itakuwa wanufaika kwenye kongani za viwanda, akiahidi Serikali kuunga juhudi za Kyecu kujenga kiwanda hicho.
“Baada ya kuhamasisha kilimo kwa kiasi kikubwa na kuleta umeme, kifuatacho ni kuweka kongani za viwanda ili kuongeza thamani ya mazao, hivyo Serikali itaunga juhudi za Kyecu katika kuongeza nguvu kujenga kiwanda,” amesema Samia.
Akizungumza leo Septemba 9 na Mwananchi Digital, Kaimu Meneja wa Chama Kikuu cha Ushirika Kyela (Kyecu), Nabii Mwankyenda amesema hadi sasa wamekusanya Sh196 milioni katika tozo ya Sh50 kwa kila kilo wanayouza ya cocoa.
Amesema matarajio yao hadi mwisho wa msimu wa zao hilo, Machi mwakani ni kukusanya takribani Sh500 milioni, akieleza kuwa gharama za kujenga kiwanda hicho ni zaidi ya Sh800 milioni.
“Hadi Juni tulikusanya zaidi ya Sh 300 milioni ambazo tumeshanunua vifaa vya kidijitali ikiwa ni vipima unyevu, mizani mizuri na ya kisasa ya kupima zao kubaini ubora, hizi ni hatua ambazo zinatupeleka kwenye utekelezaji,” amesema Mwakyenda.
Ameongeza kuwa, tayari wameshapata kiwanja kwa ajili ya eneo la uwekezaji huo wa kiwanda kupitia kwa mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya hiyo na kwamba, wanaendelea kuwasiliana na wadau ili kukamilisha ujenzi huo.
“Tumefurahishwa na kauli ya mgombea urais CCM, kuhusu kutuunga mkono, Kyecu itashirikiana na mgombea huyo na kumpa kura za ndiyo ili tuendelee kunufaika naye kwenye uongozi wake,” amesema meneja huyo.
Mwenyekiti wa Bodi ya Kyecu, Leah Mwakapala amesema kwa sasa wakulima wanapaswa kujipanga kuzalisha zao hilo kwa tija na ubora ili kuweka ushindani wa soko ndani na nje.
“Uwapo wa kiwanda hiki utaleta mataifa mengine kuchakata zao lao hapa Kyecu, hivyo wakulima wetu wajipange kuzalisha kwa wingi, tija na ubora ili kulinda soko letu” amesema Leah.
Mkulima Ayoub Mkumbwa amesema uwepo wa kiwanda hicho utachochea fursa za kiuchumi kwa mkulima mmoja mmoja, huku akitoa pongezi na shukrani kwa mgombea urais wa CCM.
“Ni kilio cha muda mrefu kwa kuwa mara kadhaa tumekosa bei halisi ya zao la cocoa, kwa maana hiyo tukipata kiwanda chetu tutaondokana na changamoto hii na uchumi wetu utabadilika,” amesema Mkumbwa.
Batali Ndile, amesema kiwanda hicho kinaenda kumaliza kero na changamoto ya bei ya zao hilo, akieleza kuwa, wakulima watakuwa pamoja na mgombea urais wa CCM ili kukidhi hitaji lao.
“Amegusa maisha yetu sisi wakulima wa cocoa, tunahitaji soko la uhakika na kuongeza thamani wa zao, kwa maana hiyo, sisi tunaungana naye Samia ili aweze kutusaidia hitaji letu,” amesema Batali.