Sh5 bilioni zalipa fidia wananchi kupisha ujenzi bomba la mafuta

Muktasari:
Katibu Mkuu Wizara ya Nishati, Felchesmi Mramba amesema jumla ya Sh5 bilioni zimetolewa kwa ajili ya kuwalipa fidia kwa wananchi waliopisha ujenzi wa bomba la kusafirisha mafuta ghafi kutoka Hoima-Uganda hadi rasi ya Chongoleani nchini Tanzania
Tanga. Jumla ya Sh5 bilioni zimetolewa kuwalipa fidia wananchi wanaopisha ujenzi wa bomba la kusafirisha mafuta ghafi kutoka Hoima-Uganda hadi rasi ya Chongoleani nchini Tanzania.
Hayo yamesemwa leo Jumamosi, Julai 23, 2022 na Katibu Mkuu Wizara ya Nishati, Felchesmi Mramba wakati wa ziara iliyofanywa na ujumbe kutoka Uganda ulioongozwa na Waziri wa Madini wa nchi hiyo, Peter Lokeris.
Ujumbe huo ulitembelea Chongoleani eneo litakapojengwa bomba hilo mkoani Tanga.
Katibu Mkuu huyo amesema zaidi ya wananchi 600 ambao mradi utapita katika maeneo yao na ambapo kazi maalumu zitafanyika wameshalipwa ikiwemo kujengewa nyumba huku wananchi 8800 maeneo yao yamefanyiwa tathimin na wanasainishwa mikataba kwaajili ya kulipwa.
"Kazi za fidia zimeanza kufanyika kwa maeneo yote yanayopitiwa na bomba ambapo watu 300 katika sehemu zinapofanyika kazi maalum mfano pale Sojo tayari wameshalipwa fidia zao na kujengewa nyumba zao na kuhamishwa na wananchi wengine 300 wameshalipwa hivyo fedha karibia bilion tano zimeshalipwa" amesema Mramba
Mramba amesema kazi zenyewe hazijaanza kwasasa wako kwenye kazi za maandalizi hasa kwenye kuweka bomba na kwamba kazi zilizoanza ni za kujenga kiwanda cha kupaka rangi na kuweka plastiki kwenye mabomba katika eneo la Sojo.
Pia, amesema mradi huo ni wa miaka mitatu na kwamba wameshaanza kuagiza mabomba hivyo kuanzia mwezi wa nane au ifikapo mwezi wa 12 yatakuwa yameshaingia mabomba hayo.
Mwenyekiti wa Kamati ya kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, Dastan Kitandula amesema timu hiyo kutoka Uganda wamekwisha tembelea eneo la kuzalisha umeme kwa kutumia gesi lakini wakaona ni muhimu wafikie Tanga kujionea eneo lilipo na kwamba Tanga ndio kutakuwa na kazi kubwa kwani mafuta yale yatapitia hapo.
Hata hivyo, Waziri wa Madini kutoka Uganda, Lokeris amesema wamefurahi kufika Tanga kujionea mradi wa bomba utakapopita.