Sh3 bilioni kuchoronga visima vya nishati joto ardhi ziwa Ngosi

Mkurugenzi wa Maendeleo na Biashara wa Kampuni ya Uendeleza wa Joto Ardhi( TGDC) Mhandisi. Idrissa Kajugas akionyesha baadhi ya shehena ya vifaa vilivyopokelewa kwa ajili ya kuanza uchorongaji wa visima vya mradi wa ziwa ngosi. Picha na Hawa Mathias
Muktasari:
- Mradi huo unatarajiwa kuanza kutekelezwa mapema Februari hadi Machi mwaka huu, uchorongaji huo utaanza baada ya kupokewa kwa shehena ya vifaa na mtambo wa kisasa.
Mbeya. Serikali imenunua vifaa vya kisasa vyenye thamani ya Sh3 bilioni kwa ajili ya kuanza uchorongaji wa visima vya kuzalisha umeme wa nishati jadidifu ya jotoardhi katika eneo la Ziwa Ngosi, wilayani Rungwe, Mkoa wa Mbeya.
Mkurugenzi wa Maendeleo ya Biashara wa Shirika la Maendeleo ya Nishati ya Jotoardhi (TGDC), Mhandisi Idrissa Kajugus ameyasema hayo leo Jumatano, Januari 15, 2025 jijini Mbeya.
Amesema vifaa hivyo vimewasili na kupokewa katika karakana ya Shirika la Umeme (Tanesco) iliyopo Iyunga, jijini Mbeya.
Mhandisi Kajugus amesema hatua ya sasa ni kupokea vifaa hivyo na kufanya ukaguzi wa ubora kabla ya kuvisafirisha kwenda eneo la mradi.
"Tunatarajia shughuli za uchorongaji wa visima zitaanza mapema mwezi Februari hadi Machi mwaka huu," amesema Kajugus.
Amesema mradi huo unafadhiliwa na serikali kupitia bajeti kuu, wabia wa maendeleo, pamoja na Tanesco ambayo ni kampuni mama ya TGDC inayotekeleza mradi huo.
Aidha, mkurugenzi huyo amesema serikali ilitoa fedha kwa ajili ya ununuzi wa mtambo wa kisasa wa uchorongaji wa visima na kufanikisha taratibu za mikataba na wataalamu, ikiwemo mhandisi mshauri wa mradi huo.
“Mradi wa Ziwa Ngosi ni miongoni mwa miradi ya kipaumbele ambayo serikali imewekeza kwa lengo la kuhakikisha upatikanaji wa umeme wa uhakika kupitia nishati jadidifu ya jotoardhi unakuwepo,” amesema.
Kajugus amesema visima hivyo vitakuwa na urefu wa kati ya kilomita 1.2 na 1.5 na ujenzi wake utazingatia viwango vya ubora unaohitajika. “Saruji yenye viwango vya kimataifa imetayarishwa kwa ajili ya ujenzi huo,” amesema mhandisi huyo.
Amesema mradi huo pia utaboresha huduma za jamii, ikiwa ni pamoja na upatikanaji wa maji safi na kuboresha miundombinu ya barabara katika eneo husika.
“Tunamshukuru Rais Samia Suluhu Hassan (Serikali) kwa kuipatia TGDC fedha za ununuzi wa mtambo wa uchorongaji wa visima, jambo linaloimarisha utekelezaji wa mradi huu,” amesema.
Fundi Mchundo wa TGDC, Safina Yunde amesema kupitia mradi huo, fursa za ajira zimezalishwa kwa wananchi wa eneo hilo ili kuinua kipato chao.
“Tunahakikisha tunawashirikisha wananchi ili wajione kuwa sehemu ya kulinda na kutunza mradi huu muhimu,” amesema.
Mhandisi wa ujenzi na Kaimu Meneja wa Mradi wa Ziwa Ngosi, Hoja John kwa upande wake ametoa wito kwa wananchi kuhakikisha rasilimali zilizowekezwa katika mradi huu zinalindwa kwa manufaa ya jamii nzima. “Serikali imewekeza kwa kiwango kikubwa kwenye mradi huu wa nishati ya jotoardhi. Ni jukumu letu sote kuhakikisha tunalinda rasilimali hii ili kufanikisha maendeleo ya taifa letu,” amesema.