Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Serikali yawaonya wanaosafirisha binadamu

Muktasari:

  • Serikali imepiga marufuku usafirishaji wa binadamu wanaokwenda kutumika isivyo halali kwa kuwatumikisha kinyume cha sheria.

Dar es Salaam. Serikali imepiga marufuku usafirishaji wa watoto, wanawake na wenye ulemavu kwa kuwapeleka kutumikishwa nje ya nchi, kwani ni kinyume cha sheria na kuharibu taswira ya nchi.

Kauli hiyo imetolewa leo Januari 5,2023 na Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana, Ajira na Watu Wenye Ulemavu, Patrobas Katambi wakati wa ziara ya kutembelea Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) na Bandari ya Dar es Salaam ili  kufahamu utaratibu wa uingiaji na utokaji ndani na nje ya nchi.

Amesema watu wote wanaojihusisha na biashara hiyo waache mara moja kwa kuwa njia zote za kutoka nje ya nchi zina mifumo ya kuwakamata watu wanaojihusisha na biashara hiyo haramu kwa kisingizio cha mialiko.

"Kuna utaratibu mzuri wa ukaguzi na kuna vifaa vya kisasa vinavyotumika kukagua katika mipaka, hivyo huwezi kusafirisha binadamu kwa njia isiyo halali ni lazima utakamatwa," amesema Katambi.

Amesema yeyote anayetaka kusafiri anatakiwa kufuata utaratibu uliopo na endapo kuna watu watataka kuijaribu Serikali kwa kufanya biashara haramu, hawatarudi uraiani wala kurudi nchi aliyotoka zaidi ya kufikishwa sehemu husika kupitia mamlaka za kisheria.

Pia amesema maeneo ambayo ni vipenyo vya kupitishwa biashara za magendo ikiwepo Ununio na Mbweni, wilayani Kinondoni Mkoa wa Dar es Salaam, wajitafakari kwa kuwa kikosi kazi na vyombo vya usalama vimejipanga kuhakikisha biashara hiyo inakomeshwa.

Kwa upande wake, Wakili wa Serikali Mkuu, Cesilia Shelly ambaye pia ni kiongozi wa kikosi kazi cha ulinzi wa mtoto dhidi ya usafirishaji haramu wa binadamu (AHTCD-TF), amewaomba wananchi kutoa taarifa za usafirishaji wa binadamu na kutumikishwa kazi zisizostahili ndani na nje ya nchi.

"Tuna imani wananchi watashirikiana nasi katika kudhibiti usafirishaji wa binadamu, kutokana na takwimu tulizonazo kwa kiasi kikubwa usafirishaji binadamu umepungua na kuna msukumo wa wananchi kuona si kitu kizuri kufanya biashara hiyo," amesema Cesilia.

Kaimu Meneja wa bandari ndogo ya Dar es Salaam, Yusuph Sunge amesema, "Kama kuna taarifa za usafirishaji wa walemavu na watoto ili wakatumikishwe, hapa hawawezi kupita kwa kuwa tuna utaratibu wa kukata tiketi kwa kutumia vitambulisho na kuna ukaguzi kupitia mamlaka husika ikiwepo jeshi la polisi."

Naye Katibu Mkuu wa Shirikisho la Vyama vya Watu Wenye Ulemavu (Shivyawata), Jonas Lubago amewataka watu wenye tabia ya kusafirisha walemavu kuwapeleka nje ya nchi kwa nia ya kuwatumikisha ili kujiingizia kipato, waache tabia hiyo.

"Tunajua binadamu wana matamanio, hivyo hatuoni kama kuna haja ya kutumia njia ya udhalilishaji wa kuwatumia walemavu katika kujipatia kipato kwa kuwafanya kuwa ombaomba kwa kuwasafirisha nje ya nchi," amesema Lubago.

Awali, Naibu Kamishna wa Uhamiaji (DCI), Juliette Sagamiko amesema wasafiri wote wanapitia utaratibu wa kukaguliwa katika mifumo, hivyo hakuna mtu atakayepitishwa kiholela.

Amesema kwa wale wanaopata fursa za kwenda kufanyakazi nje ya nchi wanakuwa na nyaraka sahihi zikiambatanishwa na kibali cha kwenda kufanyakazi hizo kutoka Kitengo cha Huduma za Ajira Tanzania (Taesa).

"Kuna fursa za ajira zinatokea huko nje ya nchi mabinti wanachukuliwa kwenda kufanyakazi, ni lazima wawe na vibali kutoka Taesa," amesema.