Serikali yatoa Sh40 bilioni kuboresha huduma za afya Lindi

Mkuu wa mkoa waLindi Zainabu Telack ,akiwajulia hali wagonjwa waliolazwa kwenye Hosptali ya Sokoine Mkoa wa Lindi, alipofanya ziara ya kuwatembelea wagonjwa waliolazwa hosptalini hapo ikiwa sehemu mojawapo ya kusheherekea miaka 62 ya uhuru. Picha na Bahati Mwatesa
Muktasari:
- Serikali imetoa zaidi ya Sh40 bilioni kwa ajili ya kuboresha miundombinu ya sekta ya afya mkoani Lindi ambazo zimetumika kukarabati vituo vya afya 30, zahanati 262 na hospitali 11.
Lindi. Serikali imetoa zaidi ya Sh40 bilioni kwa ajili ya kuboresha miundombinu ya sekta ya afya kwa mkoani hapa ikiwamo kukarabati vituo vya afya 30, zahanati 262 na hospitali 11.
Hayo yameelezwa leo Ijumaa Desemba 8, 2023 na Mkuu wa mkoa huo, Zainab Telack, mara baada ya kutembelea wagonjwa katika Hospitali ya Rufaa ya Sokoine ikiwa ni kuelekea katika sherehe za miaka 62 ya uhuru.
Amesema kuwa kuanzia mwaka 2021/2022 vituo vya kutolea huduma za afya mkoani Lindi vilikuwa jumla 272 lakini kufikia 2022/2023 vimeongezeka na kufikia 303.
Ameongeza kuwa, kuna fedha nyingine zilizoletwa kwa ajili ya ujenzi wa hospitali ya rufaa ya mkoa itakayokuwa na vifaa vyote ikigharimu zaidi ya Sh13 bilioni," amesema.
Akiwa hospitalini hapo, Telack amekabidhi misaada mbalimbali iliyotolewa na wadau ikiwamo sukari, sabuni na maji.
Kwa upande wake Mganga mfawidhi wa hospitali ya Rufaa ya Sokoine, Alexander Makalla amesema kuwa kipindi cha nyuma hospitali ya mkoa ilikuwa haina jengo la watoto, hivyo watoto walikuwa wakichanganywa na wakubwa na kufanya hali kuwa ngumu kuwahudumia.
"Kwa kweli sisi wafanyakazi wa hosptali ya Sokoine tunamshukuru sana Mama Samia (Rais Samia Suluhu Hassan) kwa kutuwezesha kupata jengo la mama na mtoto," amesema Makalla.
Amesema pia, sasa hivi hospitali hiyo ina madaktari bingwa sita, mashine ya ya CT- scan inayowarahisishia wagonjwa kutokwenda hosptali ya Taifa ya Muhimbili Dar es Salaam.
Akizungumza na Mwananchi, Mariam Sefu, aliyelazwa hospitalini hapo amesema kuwa huduma zote za vipimo zinapatikana, kwani awali walikuwa wanapata shida.
Naye Mkurugenzi wa Manispaa ya Lindi, Juma Mnwele amesema kuwa wanamshukuru Rais Samia kwa kuwaongezea vituo vya kutolea huduma ya afya katika Manispaa yake, kwani mwanzoni kulikuwa na vituo vichache.
"Popote utakapo kwenda kituo cha kutolea huduma za afya unapata, sio hadi uende hospitali kubwa, kama ugonjwa wa kawaida unatibiwa hapohapo kwenye zahanati au kituo cha afya kilicho karibu,” amesema Mnwele.