Serikali yaonya wanaotumia jina la Dk Nchimbi kutapeli
Makamu wa Rais Tanzania, Dk Emamanuel Nchimbi.
Muktasari:
- Onyo hilo limetolewa na Ofisi ya Makamu wa Rais kutokana na uwepo wa utapeli unaofanyika mtandaoni kupitia jina la Dk Nchimbi.
Dar es Salaam. Ofisi ya Makamu wa Rais imetoa tahadhari kwa umma kufuatia kuibuka kwa ukurasa wa Facebook unaojitambulisha kwa jina la Shirika la Give Direct Foundation, ambao unadaiwa kutumia jina na picha ya Makamu wa Rais, Dk Emmanuel Nchimbi katika kutapeli wananchi kwa kuwaahidi ugawaji wa fedha mtandaoni.
Kwa mujibu wa taarifa kwa umma iliyotolewa leo Mei 15, 2026 na Ofisi ya Makamu wa Rais, ukurasa huo bandia unawaelekeza wananchi kuchangua kiasi cha fedha wanachotaka kupokea, kisha kuwataka kulipa ada ya usajili ili waweze kupata fedha hizo jambo ambalo Serikali imelitaja kuwa ni udanganyifu unaolenga kuwahadaa wananchi.
Ofisi hiyo imeeleza haina uhusiano wowote na ukurasa huo kwa maudhui wala matangazo yanayosambazwa kupitia jina la Dk Nchimbi.
"Makamu wa Rais hajahusika kwa namna yoyote na shughuli hizo za utoaji fedha zinazoenezwa mtandaoni,"imeeleza taarifa hiyo.
Pia, wananchi wametakiwa kuwa makini na mitandao ya kijamii inayotumika kusambaza taarifa zisizo rasmi, hususani zile zinazohusisha ahadi za fedha na kuwataka kufanya malipo ya awali.
Ofisi hiyo imeelekeza hatua tatu muhimu kwa wananchi kuepuka matapeli wa mitandaoni ikiwamo kutojibu wala kufanya malipo yoyote kwa udanganyifu wa aina hiyo.
Hatua nyingine ni kuripoti ukurasa huo moja kwa moja kupitia mfumo wa Facebook kwa kuchagua “Report Ad na kuwasiliana na Jeshi la Polisi Tanzania au Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) iwapo tayari wameathirika.