Dk Nchimbi asema serikali itaendelea kuimarisha mazingira ya elimu
Makamu wa Rais Tanzania, Dk Emamanuel Nchimbi.
Muktasari:
- Majengo yanayojengwa yataleta manufaa kwa nchi ikiwa ni pamoja na kutengeneza fursa za ajira, kuongeza uelewa katika sayansi na teknolojia na kushajihisha uchumi wa buluu na kuongeza tija katika kilimo.
Unguja. Makamu wa Rais Tanzania, Dk Emamanuel Nchimbi amesema Serikali zote mbili zishirikiana katika kuimarisha amani na kustawisha maendeleo ya kiuchumi katika jamii kwa pande mbili za Muungano.
Dk Nchimbi ameyasema hayo leo Ijumaa Aprili 24, 2026 Mkoa wa Kusini Unguja, katika hafla ya uwekaji wa jiwe la msingi jengo la maabara za sayansi na shule ya kilimo kupitia mradi wa elimu ya juu mageuzi ya kiuchumi katika chuo kikuu cha Taifa cha Zanzibar Kampasi ya Tunguu.
Amesema, mradi huo ni mfano hai wa faida za Muungano wa Tanzania kwani unagusa maisha ya wananchi wote bara na visiwani kwani eneo hilo linatarajiwa kuwa kitovu cha elimu ya sayansi, teknolojia na kilimo kwa Zanzibar na Tanzania kwa ujumla.
Amesema, tukio hilo la uwekaji wa jiwe la msingi linathibitisha dhamira ya serikali ya awamu ya sita chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu wa kuleta mageuzi makubwa ya kiuchumi kupitia elimu ya juu nchini.
"Ujenzi wa majengo hayo unatarajiwa kusaidia katika kuimarisha utafiti, kukuza ubunifu na kutoa fursa mbalimbali za kitaalamu kwa wanafunzi, wakufunzi na wahitimu," amesema
Dk Nchimbi ameeleza kuwa, mradi huo utaleta manufaa kwa nchi ikiwa ni pamoja na kutengeneza fursa za ajira, kuongeza uelewa katika sayansi na teknolojia na kushajihisha uchumi wa buluu na kuongeza tija katika kilimo.
Naye Waziri Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira, Hamad Yussuf Masauni amesema miundombinu ambayo inajengwa na serikali imechangia kuimarisha sekta ya elimu hata ufaulu wa wanafunzi umeimarika kwa kiasi kikubwa kutokana na mazingira ya kusomea kuwa mazuri.
Naye Kaimu Makamu Mkuu wa Chuo cha Taifa Zanzibar (Suza), Profesa Abditalib Abdallah amesema, majengo hayo mawili makubwa yatakapokamilika yatahudumia zaidi ya wanafunzi 2,600 kwa wakati mmoja.
Amesema, majengo hayo yamejengwa kwa viwango vya kisasa na yatakuwa na maabara za kemia, fizikia, baiolojia, kilimo na maabara mbalimbali za Tehama pamoja na vyumba vya kufundishia, maktaba, ofisi na maeneo maalum kwa ajili ya mahitaji ya kijinsia na watu wenye mahitaji maalumu.