Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Serikali, Lissu walivyokabana kwa hoja Mahakama Kuu

Muktasari:

  • Tundu Lissu amefungua shauri la maombi ya mapitio, akipinga uamuzi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuahirisha usikilizwaji wa kesi ya jinai inayomkabili uliotolewa Juni 2, 2025.

Dar es Salaam. Mahakama Kuu Masjala Ndogo Dar es Salaam imepanga kutoa uamuzi wa pingamizi la Jamhuri dhidi ya shauri la Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu, Julai 11, 2025.

Lissu amefungua shauri la maombi mahakamani hapo akiiomba Mahakama iitishe mwenendo wa Juni 2, 2025 wa kesi ya jinai inayomkabili katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.

Jamhuri imeweka pingamizi la awali ikiiomba Mahakama ilitupilie mbali shauri hilo bila kulisikiliza, huku ikibainisha sababu tatu.

Pingamizi limesikilizwa leo Ijumaa, Juni 27, 2025 na Jaji Elizabeth Mkwizu, huku mawakili wa pande zote wakivutana kwa hoja za kisheria.

Lissu anakabiliwa na kesi ya kuchapisha taarifa za uongo mtandaoni, katika Mahakama ya Kisutu inayosikilizwa na Hakimu Mkazi Mkuu, Godfrey Mhini.

Kesi hiyo ilipangwa kuanza kusikilizwa ushahidi Juni 2, 2025, lakini Mahakama ya Kisutu iliahirisha usikilizwaji kufuatia maombi ya upande wa mashtaka kwamba iahirishwe kusubiri shauri la maombi madogo ya kuwalinda mashahidi katika kesi hiyo.

Lissu hakuridhika na uamuzi huo, ndipo akafungua shauri la maombi ya mapitio Mahakama Kuu, akiiomba mahakama iitishe jalada la kesi hiyo ya msingi na kupitia mwenendo wa siku hiyo kujiridhisha na usahihi na uhalali wake.

Shauri hilo lilipangwa kusikilizwa leo Juni 27 lakini kutokana na pingamizi hilo la Jamhuri mahakama imelazimika kama ilivyo utaratibu kusikiliza kwanza pingamizi.

Katika pingamizi hilo, Jamhuri imeibua sababu tatu, ya kwanza wanadai maombi hayo yanakiuka kifungu cha 372(1) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA), Marejeo ya Mwaka 2022.

Wakili wa Serikali Mwandamizi, Mosia Kaima amedai shauri hilo linalenga kupinga amri ya Mahakama ya kuahirisha usikilizwaji wa kesi Juni 2, 2025.

Amedai amri ya ahirisho ilikuwa haimalizi kesi ya msingi, hivyo amri hiyo haipaswi kusomewa mapitio kwa mujibu wa kifungu hicho cha sheria.

Sababu ya pili, Wakili Kaima amedai mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza maombi hayo akidai yanalenga kuifanya Mahakama iamue iwapo kifungu namba 188 cha CPA kinakiuka Katiba au la.

Amedai chini ya kifungu cha 372 cha CPA ambacho kimetumika kufungua maombi hayo hakitoi mamlaka kwa Mahakama kuangalia suala la ukatiba wa kifungu cha sheria.

Amedai suala la ukatiba wa kifungu utaratibu wa kufuata umewekwa wazi katika Sheria ya Bradea kupitia kifungu cha tisa.

"Kwa hiyo suala la mwombaji kuleta suala la ukatiba wa kifungu kwa kupitia kifungu cha 372(1) si sahihi, hivyo tunaomba maombi haya yaondolewe, yasikubaliwe," ameomba.

Sababu ya tatu ya pingamizi, Wakili wa Serikali Mwandamizi, Job Mrema amedai maombi hayo ni batili kwa kuwa yamechanganya maombi mengi kwa pamoja kasoro inayojulikana katika taaluma ya sheria kuwa ‘omnibus’.

"Maombi haya ni ‘omnibus’ kwa sababu kuna maombi sita; ambayo la kwanza, la tatu mpaka la sita yana mahitaji tofauti ili yaweze kusikilizwa," amedai.

Amedai hakuna sheria ya moja kwa moja inayozungumzia ‘omnibus’ bali limazingumziwa katika utamaduni wa Mahakama akisema kuna uamuzi wa mashauri mengi ya Mahakama Kuu na Mahakama ya Rufani kuhusu suala hilo.

"Kwenye ombi la kwanza mwombaji anaiomba mahakama kuita jalada na kufanya mapitio ya mwenendo wa Juni 2, 2025 katika shauri namba 8606/2025," amedai na kuongeza:

"Lakini katika ombi la tatu ameiomba mahakama iite na kufanya mapitio ya shauri namba 8606/2025 lililoko Kisutu ili mahakama iamue suala la ukatiba wa kifungu cha 188 CPA.”

Amedai suala la ukatiba wa kifungu cha sheria hufunguliwa chini ya Sheria ya Utekelezaji Wajibu na Haki za Msingi (Bradea), marejeo ya mwaka 2022 na kwamba, kifungu cha 4 cha Bradea kiliweka utaratibu kwa hoja za ukatiba.

Amedai suala la ukatiba kwanza, Mahakama inakuwa kama Kamati ya Kikatiba na shauri linasikilizwa na majaji watatu, kwa mujibu wa kifungu cha 10 cha Bradea.

"Kwa hiyo, maombi haya hayawezi kusikilizwa na kuamuliwa kulingana na ubovu wake," amedai.

Wakili Katuga kwa upande wake amedai kilichoruhusiwa kwenye kifungu cha 372(2) kufanyiwa mapitio ni kama kuna ukiukwaji wa utaratibu wa mwenendo.

"Kwa kuangalia katika maombi haya hakuna malalamiko dhidi ya ukiukwaji utaratibu wa mwenendo bali wanalalamikia uamuzi wa Mahakama,” amedai.

Wakijibu hoja za pingamizi hilo kwa nyakati tofauti, mawakili wa utetezi, Fednarnd Makore, Paul Kisabo, Jeremiah Mtobesya, Hekima Mwasipu na Peter Kibatala wamedai pingamizi la Jamhuri halina msingi.

Makore amedai Mahakama hiyo ina mamlaka kisheria kuita na kuangalia mwenendo wowote wa Mahakama ya chini kuhusu uhalali na usahihi wake. Vilevile, mwenendo wa shauri ni pamoja na amri na uamuzi wa Mahakama.

Amedai kifungu cha 372(1) na (2) kimeshajadiliwa mara nyingi na Mahakama ya Rufani katika rufaa mbalimnali, ikiwamo ya Wakili Peter Madeleka ambayo amesema mahakama ilisema kifungu cha 372(2) hakiwezi kuinyima Mahakama mamlaka ya kufanya mapitio ya amri ambayo ina kasoro.

"Kwa hiyo tunaomba mahakama hii iendelee na msimamo wake kuwa ina mamlaka ya kuita na kufanya mapitio ya mashauri yoyote.

Hakuna kesi hata moja ilitolewa na upande wa Jamhuri kujadili kifungu cha 372(1) na (2)," amedai.

Wakili Kisabo amedai maombi hayo hayakinzani na kifungu cha 372(2) cha CPA kwa sababu msingi wa maombi yao ni kurejea mwenendo wa kesi namba 8606/2025 wa Juni 2, 2025 ili kujiridhisha na uhalali na usahihi wake.

"Kwa hiyo, tunaomba mahakama hii kupitia mwenendo mzima na si amri maalumu," ameomba.

Wakili Mtobesya amedai kilichoongelewa Juni 2, 2025 ni kwamba, hapakuwa na msingi wa maombi ya ahirisho la usikilizwaji kesi ya msingi.

Amedai walisema kama kuna umuhimu wa kuahirisha chini ya kifungu cha 188 cha CPA, basi Mahakama ya Kisutu ipeleke shauri hilo Mahakama Kuu maana kulikuwa na kuathiri haki ya kikatiba ya mshtakiwa ya usikilizwaji sawa.

Wakili Mwasipu amedai sababu ya tatu ya pingamizi kwamba kuna maombi mchanganyiko haina mashiko, akieleza maombi yote sita yanaenda pamoja, wala hayatofautiani.

Wakili Kibatala amedai maombi hayo yako sawa kwa kuwa hayalengi kuifanya Mahakama iamuru kama kifungu cha 188 kinakiuka Katiba au la kwa hiyo, hoja ya tatu ya pingamizi haina mashiko.

Wakijibu hoja hizo, mawakili wa Serikali wamesisitiza hoja zao za awali, wakieleza bado sababu zao za pingamizi zina mashiko kiasi cha kuifanya Mahakama itupiliwe mbali shauri hilo.

Jaji Mkwizu baada ya kusikiliza hoja za pande zote ameahirisha shauri hilo hadi Julai 11, 2025 atakapotoa uamuzi.


Kesi ya msingi

Katika kesi ya msingi Lissu anakabiliwa na mashtaka matatu ya kuchapisha taarifa za uongo katika mtandao wa Youtube kinyume cha Sheria ya Makosa ya Kimtandao namba 14 ya mwaka 2015, kifungu cha 16.

Katika mashtaka hayo Lissu anadaiwa kumhusisha Rais wa Jamhuri ya Muungamo wa Tanzania na kutenguliwa kwa wagombea wa Chadema katika maeneo mbalimbali wakati wa Uchaguzi wa Serikali za Mitaa wa mwaka  2024.

Pia anadaiwa kuwatuhumu askari Polisi kuhusika katika wizi wa kura kupitia vibegi na majaji kutokutenda haki kwa madai ya kutaka wapate uteuzi wa Rais kuwa majaji wa Mahakama ya Rufani.

Anadaiwa kutenda makosa hayo Aprili 3, 2025 jijini Dar es Salaam, kwa nia ya kulaghai umma.

Kesi hiyo imeshaanza kusikilizwa ushahidi na imepangwa kuendelea Julai 2, 2025.