Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Sekta ya kubahatisha inavyozidi kukua

Muktasari:

  • Kwa mwaka wa fedha uliopita sekta hiyo ilikuwa kwa asilimia 22,matarajio yaliyopo ni ukuaji zaidi kwa mwaka 2025 hadi kufikia asilimia 25 au zaidi.

Dar es Salaam. Sekta ya michezo ya kubahatisha inatarajiwa kuendelea kukua kwa zaidi ya asilimia 20 katika kipindi cha miaka ijayo huku ikivutia zaidi uwekezaji ambao unaliingizia taifa mabilioni ya Shilingi.

Hayo yamebainishwa leo Januari 21, 2024 wakati wa kumtambulisha mwendeshaji mpya wa bahati nasibu ya Taifa ambayo sasa itaendeshwa na kampuni ya Ithuba Tanzania ambayo ni ubia kati ya wazawa na wawekezaji wa kigeni.

Akizungumza katika uzinduzi huo Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Michezo ya kubahatisha Tanzania (GBT), James Mbalwe amesema kwa uwekezaji tu wa Ithuba sekta ya michezo ya kubahatisha imeongeza ukubwa wake kwa Dola za Marekani 20 milioni (zaidi ya Sh50 bilioni).

“Kwa mwaka wa fedha uliopita sekta yetu ilikuwa kwa asilimia 22, tunatarajia mwaka huu itakuwa kuanzia hapo au hadi asilimia 25 na zaidi, Mwaka jana mapato ya Serikali kutokana na shughuli za kubahatisha yalikuwa zaidi ya sh200 milioni tunatarajia makubwa zaidi,” amesema.

Mbalwe amesema katika utafiti walioufanya walibaini kuwa wacheza wakubwa wa michezo ya kubahatisha ni vijana hususani waendesha bodaboda wakati wakiwa wametulia kusubiri wateja wanaburudika.

Katika hafla hiyo Naibu Waziri wa fedha Hammad Chande amesema kuwa Ithuba sio mwenye bahati nasibu ya Taifa yeye ni mwendeshaji tu na Serikali itaendelea kuwa mwenye mchezo huo huku akisisitiza kuwa usimamizi wa karibu utafanyika.

“Serikali haitafumba macho pale taratibu, sheria, kanuni na maadili vitakiukwa eti kisa biashara. Imani yangu ni kuwa, imani italindwa kama mlivyoaminiwa, tayari mnafanya vyema katika mataifa ya Afrika kusini na Uganda bila shaka mtafanya hivyo na hapa,” amesema Chande.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Ithuba Tanzania Kelvin Koka amesema Sh50 bilioni zinazotajwa za uwekezaji zitawekezwa mwaka huu na wanatarajia kutoa ajira zaidi ya 2000 katika kipindi chao cha mkataba wa miaka nane.

“Ithuba ni kampuni iliyosajiliwa Tanzania na ina umiliki wa wazawa kwa asilimia zaidi ya 40. Tunataka kila Mtanzania aweze kushiriki katika fursa chanya zitakazoibuliwa na uwekezaji wetu,” amesema Koka.

Aidha katika mkakati wao wa kudhibiti uraibu na athari hasi kwa jamii Koka amesema wameweka tokeni ya Sh100 na wanaamini kuwa mtu hawezi kufilisika kwa kiasi hicho kidogo cha fedha.