Sekta tisa kuibeba Dira ya Taifa 2050

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Mipango na Uwekezaji), Profesa Kitila Mkumbo akizungumza bungeni alipokuwa akijibu baadhi ya hoja za wabunge waliochangia mjadala wa kupitisha Mpango wa Maendeleo wa Taifa jijini Dodoma. Picha na Edwin Mjwahuzi
Muktasari:
- Sekta zilizobainishwa katika Dira 2050 ni kilimo (uvuvi, mifugo na misitu), utalii, viwanda, ujenzi na mali isiyohamishika, madini, uchumi wa buluu, michezo na ubunifu, huduma za fedha na sekta ya huduma.
Dar es Salaam. Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 (Dira 2050) imebainisha sekta tisa zenye fursa za mageuzi ya kuchochea kufikiwa kwa malengo ya Taifa na kuivusha Tanzania miaka 25 ijayo.
Dira 2050 imewasilishwa leo Alhamisi, Juni 26, 2025 bungeni jijini Dodoma na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo, siku moja kabla ya Rais Samia Suluhu Hassan kulivunja kwa Bunge la 12.
Ili kutumia rasilimali za Taifa kwa ufanisi katika kufanikisha malengo ya maendeleo, Dira 2050 inatoa mwongozo wa kuweka vigezo vya kuchagua na kutoa kipaumbele kwa sekta zenye uwezo wa kuchochea mageuzi ya kijamii na kiuchumi.
Sekta zilizobainishwa katika Dira 2050 ni kilimo (uvuvi, mifugo na misitu), utalii, viwanda, ujenzi na mali isiyohamishika, madini, uchumi wa buluu, michezo na ubunifu, huduma za fedha na sekta ya huduma.
Dira 2050 imeainisha vigezo vya kuchagua sekta za mageuzi kuwa ni uwezo wa kuzalisha ajira kwa wingi, uwezo wa kuongeza mauzo ya nje, uwezo wa kukua na kuchochea ukuaji wa sekta nyingine, kuongeza thamani na kukuza Mapato.
Kwa kujibu wa dira hiyo, sekta ya kilimo (uvuvi, mifugo na misitu) bado ni mhimili wa uchumi wa Tanzania, kikichangia asilimia 26.5 ya pato la Taifa, kikiajiri asilimia 65 ya nguvukazi, na kuzalisha asilimia 30 ya mapato ya mauzo ya nje.
Sekta hiyo ina uwezo wa kuzalisha ajira nyingi na kuchochea ongezeko la mapato kupitia mauzo ya bidhaa zilizoongezwa thamani. Uhusiano wake na sekta za viwanda, usafirishaji na biashara unabainisha nafasi yake katika kukuza ajira na uchumi.
“Katika siku zijazo, kilimo bado kitaendelea kuwa nguzo ya uchumi wa Tanzania. Kufikia mwaka 2050, sekta hii inatarajiwa kuwa na mabadiliko makubwa, yenye tija, endelevu na yenye ushindani wa hali ya juu,” inasomeka sehemu ya Dira 2050.
Sekta nyingine ni utalii, unaochangia asilimia 25 ya mapato ya mauzo ya nje ya Tanzania, ni mojawapo ya sekta kuu za uchumi. Sekta hii ina mchango muhimu katika kuimarisha urari wa malipo na kuchochea ukuaji wa pato la Taifa.
Utalii unaendelea kuwa chanzo kikuu cha mapato ya fedha za kigeni, ukichochea sekta muhimu kama vile za ukarimu, usafiri na biashara. Kuongezeka kwa idadi ya watalii wa nje na ndani kunathibitisha taswira chanya kwa uchumi, huku sekta hiyo ikichochea maendeleo jumuishi na endelevu.
“Kufikia mwaka 2050, utalii unatarajiwa kuwa moja ya vyanzo vikuu vya ajira za moja kwa moja na nyinginezo, huku fursa kubwa zikionekana katika sekta za ukarimu, kuongoza watalii, usafirishaji na biashara za ndani,” inaeleza dira hiyo.
Sekta ya viwanda nchini inatajwa kuwa itapanuka na kuwa msingi wa ukuaji wa uchumi ifikapo mwaka 2050. Kwa muda mrefu kilimo kimekuwa uti wa mgongo wa uchumi wa nchi. Hata hivyo, kuitegemea sekta ya kilimo pekee kwa muda mrefu, ni changamoto.
Dira 2050 inafafanua kwamba, mabadiliko ya tabianchi, kuyumba kwa bei na misukosuko ya masoko duniani kunaweza kuiathiri nchi endapo sekta hii pekee inayotegemewa itayumba.
“Tanzania inalenga kuwa kitovu cha viwanda chenye ushindani kimataifa ifikapo mwaka 2050, ikitumia ongezeko la idadi ya watu, maendeleo ya kiteknolojia na msingi wake imara wa kilimo kama nyenzo muhimu,” inaeleza Dira 2050.
Kwa mujibu wa Dira 2050, sekta za ujenzi na mali isiyohamishika zitakuwa kiini cha ukuaji wa miji ya Tanzania, zikikidhi mahitaji yanayoongezeka ya makazi, miundombinu na huduma za umma, huku zikitengeneza fursa kubwa za kiuchumi.
Wakati huohuo, sekta ya madini inatajwa kuwa moja ya sekta muhimu zenye fursa ya kuchangia maendeleo ya nchi. Hii inatokana na utajiri wa rasilimali za madini, zikiwamo dhahabu, almasi, tanzanite na madini ya kimkakati kama grafiti, lithiamu, urani na madini adimu.
Uchumi wa buluu unaozingatia matumizi endelevu ya rasilimali za bahari na maji baridi, utakuwa na mchango mkubwa katika kuleta maendeleo nchini.
Tanzania ambayo ina ukanda mrefu wa pwani, maziwa na mito mikubwa, ina fursa nyingi za kukuza sekta za uvuvi, utalii wa pwani na wa maziwa, usafiri wa majini na matumizi ya nishati mbadala kutoka baharini.
Dira 2050 inaeleza kwamba, sekta ya michezo na ubunifu ina uwezo ambao haujatumiwa kikamilifu katika kuchochea maendeleo ya kijamii na kiuchumi. Inaeleza kwamba, sekta hizo zinatoa fursa muhimu za ajira, kuendeleza ujuzi, kuwa chanzo cha kipato na kuwawezesha vijana, wakati huo huo zikijenga umoja na mshikamano wa jamii.
Sekta ya huduma za kifedha zitakuwa kichocheo cha mageuzi ya kiuchumi Tanzania ifikapo mwaka 2050. Mahitaji ya huduma za kifedha, bima na uwekezaji yatakua kwa kiasi kikubwa kutokana na ongezeko la watu na ukuaji wa miji.
Kwa upande wa sekta ya huduma, inatajwa kuwa itachukua nafasi muhimu katika kuendesha maendeleo ya Tanzania, hususan katika maeneo ya biashara, huduma za ukarimu na huduma nyingine za kijamii na kiuchumi.