Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Sangara wapungua Ziwa Victoria, Serikali ikitangaza kudhibiti uvuvi haramu

Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Profesa Riziki Shemdoe akizungumza kwenye mkutano wa kuhamasisha wadau wa uvuvi kudhibiti uvuvi haramu na biashara haramu ya mazao ya uvuvi Ziwa Victoria. Picha na Anania Kajuni

Muktasari:

  • Uvunaji wa samaki aina ya sangara umeshuka kutoka tani 91,709 mwaka 2019 mpaka tani 80,265 mwaka 2023, sababu kubwa inatajwa kuwa ni uvuvi haramu.

Mwanza. Wakati uvunaji wa samaki aina ya sangara ukishuka kutoka tani 91,709 mwaka 2019 mpaka tani 80,265 mwaka 2023, sababu ya upungufu huo imetajwa kuwa ni uvuvi haramu.

Kutokana na hali hiyo, tayari Serikali imeweka mikakati kadhaa, ikiwemo kununua boti 10 za doria, kuweka mfumo maalumu wa ufuatiliaji vyombo vya uvuvi (tracking system), ununuzi wa maboya maalumu pamoja na teknolojia ya kubaini vyombo vya uvuvi na wavuvi wanaosogea kuvua sehemu za mazalia ya samaki.

Akizungumza leo Jumatatu Agosti 26, 2024 kwenye mkutano wa wadau wa uvuvi jijini hapa, mkurugenzi wa uvuvi nchini, Mohamed Sheikh ametaja mikakati mingine katika mwaka huu wa fedha kuwa ni kununua droni maalumu kwa ajili ya kufuatilia na kuwabaini wavuvi haramu.

"Uvunaji wa sangara mwaka 2019 ilikuwa  tani 91,709 mwaka 2023 imeshuka mpaka tani 80,265 ikiwa ni upungufu wa tani 11,444. Kwa upande wa uvunaji wa dagaa mwaka 2019 ilikuwa tani 122,000 mwaka 2023 imeongezeka mpaka 154,000 ikiwa ni mafanikio ya juhudi zinaendelea kufanywa na Serikali,” amesema.

Amesema mauzo ya sangara mwaka 2019 yalikuwa tani 32,000 mwaka 2023 na sasa yameshuka hadi tani 20,000.

Kwa mauzo ya minofu ya samaki mwaka 2019 amesema yalikuwa tani 17,000, lakini mpaka sasa ni tani 11,000, wakati mauzo ya mabondo mwaka 2019 yalikuwa ni tani 838 na mwaka 2023 yameshuka hadi tani 433.

Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Profesa Riziki Shemdoe amewaomba wadau wa uvuvi kushirikiana na Serikali kuandaa mkakati wa kulinda ziwa hilo, pia kudhibiti utoroshaji wa mazao ya uvuvi, kulinda mazalia ya samaki pamoja na kutumia nyavu sahihi.

"Kuna wavuvi wanavua bila kuwa na leseni, kwa hiyo vyama vya uvuvi mhakikishe mnavisajili na pia kuna utoroshaji wa mazao ya uvuvi, nasikia kuna biashara ya mabondo ya samaki inafanyika katikati ya ziwa na kupelekwa nje ya nchi, sisi kama nchi hatufaidiki nayo wala kupata fedha ya kigeni," amesema Profesa Shemdoe.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chama cha Wavuvi Tanzania (Tafu) ambaye pia ni Mwenyekiti Kamati ya Ushauri Uvuvi Endelevu Ziwa Victoria, Bakari Kadabi amedai, “ujio wa boti za doria hatuna mashaka zikija zitasaidia lakini kikubwa watakaofanya hizo doria ni hao hao maofisa uvuvi ambao kimsingi mpaka sasa wamefeli kudhibiti uvuvi haramu, kwa hiyo lazima tuangalie njia sahihi ya kukomesha uvuvi haramu na kulilinda ziwa."

Kauli hiyo imeungwa mkono na msemaji wa Chama cha Wavuvi Tanzania (Tafu), Sijaona Kaloli aliyesema mbali na kuwekeza nguvu kubwa kwenye mbinu za udhibiti, pia Serikali iwekeze nguvu ķubwa kwenye uboreshaji wa sera na sheria za kulinda mazao hayo.

"Kwetu sisi tunasema hatua hii imechelewa, lakini kimsingi tunaona mikakati ya kimaandishi si ya kivitendo. Tunasubiri kuona ni kwa namna gani tutasimamia kwa vitendo maelezo yaliyotolewa kwa sababu si mara ya kwanza kuzungumza mikakati kama hii," amesema.

Ziwa Victoria linachangia asilimia 67 katika sekta ya uvuvi kwa mujibu wa takwimu ya mwaka 2023/2024, huku ikikadiriwa kuwa na wavuvi zaidi ya 100,000.