Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Simulizi ya mvuvi aliyenusurika kifo mara tatu baharini

Mvuvi wa Mwalo wa Deep Sea Jijini Tanga, Ramadhani Adamu akipanga samaki aliyotoka kuwavua kwa ajili ya kusubiria wateja. Picha na Rajabu Athumani

Muktasari:

  • Aliokolewa baada ya boti kuzama mwaka 1998, kuepuka kuliwa na papa mwaka 2000, na kuepuka kifo baada ya boti yake kuzama na viroba vya sukari mwaka 2005.

Tanga. Kufa ni mara moja tu, ndivyo inavyoelezwa na Waswahili, hata hivyo kwa Ramadhani Adamu (58), ambaye ni mvuvi wa Mwalo wa Deep Sea, jijini Tanga na mkazi wa Wilaya ya Mkinga, kifo kwake kimebisha hodi mara tatu na anamshukuru Mungu amenusurika.

Ramadhani anawakilisha zaidi ya wavuvi wadogo waliopo Tanzania wanaovua kwa zana hafifu, lakini wakitegemewa kwa uvuvi wa samaki nchini. 

Akizungumza na Mwananchi leo Jumatatu Agosti 26, 2024 jijini hapa, Ramadhani anasema katika kazi yake ya uvuvi ameshakutana na matukio makubwa matatu yaliyohatarisha uhai wake, likiwemo la chombo alichokuwa akitumia kuzama baharini na kukaa saa 48 bila msaada.

Anasema moja ya matukio hayo lilitokea mwaka 1998 wakiwa wavuvi watatu kwenye chombo, saa 7 mchana wakiwa wameshamaliza kuvua na wakijiandaa kurudi nyumbani.

“Kutoka eneo ambalo tunatoka kuvua mpaka tunapoishi chombo kinachukua saa tatu. Kabla hatujaanza safari kulitokea wingu kubwa lililoambatana na upepo mkali, chombo (boti) ilishindwa safari na kupinduka na kuzama baharini.

"Baada ya kuzama baadaye tulirudi juu na kuokota baadhi ya vitu vilivyokuwa vikielea baharini kutoka kwenye chombo chetu, tulifunga kamba vifaa hivyo pamoja na sisi wenyewe, ili mawimbi yakija tusipotezana kwa kusukumwa na maji, lakini kamba hizo zilikatika na kurushwa tena ndani ya bahari," anasimulia Ramadhani.

Anaeleza kutokana na msukosuko wa kuchafuka bahari, kila mmoja alisukumwa upande wake na mawimbi ya maji, kuanzia wakati huo mpaka usiku ulipoingia walikuwa hawajapata msaada wowote, ila baadaye chombo chao kilirudi juu na yeye na mwenzake mmoja wakalala juu yake.

Mvuvi huyo anasema wakati huo mwenzao mmoja alishapotea na hawakumuona tena. Anasimulia kuwa walikesha juu ya chombo hadi siku ya pili asubuhi, huku chombo kikitembea baharini kufuata upepo unakoelekea, wao wakiwa hawajui wanaelekea wapi.

"Tulilala juu ya chombo asubuhi tunaamka hatujapata msaada, tukashinda tena na kulala, siku ya pili asubuhi kama saa moja au saa mbili, chombo kikapandishwa na maji juu na kutokea eneo linaitwa Vanga nchini Kenya ndio tukaanza kupata msaada," anasema.

Wananchi waliowaona kwenye hali hiyo ndio waliwatoa baharini na kuanza kuwapa misaada, huku wakiwauliza kwamba wao ni raia wa Kenya au Tanga na kuwatengeneza uji mwepesi na kuwapa ili wapate nguvu.

Ramadhani anasema baada ya kupewa uji ule walipata nguvu na kuanza kutoa maelezo, ikiwemo kutoa taarifa ya mwenzao mmoja kufariki dunia kutokana na dhoruba iliyowatokea na hawafahamu walipo mpaka muda huo.

Amesema walipelekwa hospitali na kupatiwa matibabu ya kutolewa chumvi mwili na baada ya hapo, utaratibu wa kurudishwa Tanzania ulianza na wakapelekwa mpaka Horohoro na kukutana na ndugu zao.

Akieleza janga la pili, Ramadhani anasema mwaka 2000 alikutana na samaki aina ya papa, ila hakummeza, bali alimwacha aondoke.

"Nilikutana na kiumbe mmoja ambaye tunamuita papa, ni mkubwa na anaweza kummeza binadamu mara moja tu, angeamua kunimeza siku ile, basi leo nisingekuwepo, lakini Mungu tu alininusuru," anasimulia Ramadhani.

Anaeleza wakati anamwangalia papa huyo akiwa ameshakata tamaa, naye alikuwa anamwangalia, huku akichezesha mkia wake, hivyo wakawa kama wanacheza huku akihema kwa kutumia mtungi wa gesi aliokuwa nao.

Baadaye wakati anarudi nyuma polepole kufuata chombo chao, ili kujinusuru, anasema papa yule aliondoka na kumpa mgongo na hiyo ikawa manusura yake.

Tukio la tatu analokumbuka lilitokea mwaka 2005, ambalo anasema alizama tena baharini na viroba 130 vya sukari akitokea Zanzibar.

Anasema kutokana na changamoto za uvuvi alizokutana nazo, alibadilisha kazi na kuanza kusafirisha mizigo kutoka Tanga kwenda Zanzibar kwa mitumbwi yake.

Anasema katika safari hiyo usiku, chombo kilizama na viroba 130 vya sukari, ila kwa sababu walikuwa na wenzao waliwahi kuokolewa, huku viroba vyote vikizama baharini.

Baada ya kukumbwa na majanga hayo, Ramadhani anasema kwa sasa amerejea tena kazi ya uvuvi katika mwalo wa Deep Sea, akisema ameongeza umakini.