Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Samia kuhutubia maadhimisho ya uhuru Comoro


Muktasari:

  • Rais Samia atahudhuria sherehe za maadhimisho ya miaka 50 ya uhuru wa Comoro zitakazofanyika katika Uwanja wa Malouzini Omnisport, mjini Moroni.

Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan anatarajia kufanya ziara ya kikazi ya siku moja nchini Comoro kwa mwaliko wa Rais wa Umoja wa Visiwa vya Comoro, Azali Assoumani.

Taarifa iliyotolewa leo Jumamosi Julai 5, 2025 na Naibu Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu, Shaaban Kissu imesema Rais Samia atasafiri kesho Jumapili Julai 6, 2025.

Kissu amesema katika ziara hiyo, Rais Samia atahudhuria sherehe za maadhimisho ya miaka 50 ya uhuru wa Taifa hilo zitakazofanyika katika Uwanja wa Malouzini Omnisport mjini Moroni. Pia anatarajiwa kuhutubia kwenye sherehe hizo.

“Tangu nchi hiyo ipate uhuru mwaka 1975, Tanzania na Comoro zimeendelea kudumisha uhusiano wa kidugu na wa kihistoria uliojengwa juu ya misingi ya ushirikiano katika nyanja za kiuchumi na kijamii, huku Tanzania ikiendelea kuwa mdau muhimu wa maendeleo ya Taifa hilo,” imeeleza sehemu ya taarifa hiyo.

Vilevile, imeeleza kuwa ziara ya Rais Samia Comoro inadhihirisha dhamira ya dhati ya Tanzania ya kuendeleza ushirikiano wa karibu wa kidugu, kihistoria, kidiplomasia na kuunga mkono juhudi za maendeleo na mshikamano wa nchi hiyo katika miaka 50 ya uhuru wake.

Tanzania na Comoro zilitia saini hati nne za makubaliano kwenye kilele cha mkutano wa kwanza wa Tume ya Pamoja ya Ushirikiano (JPC) kati ya mataifa hayo uliofanyika Julai 24, 2024 jijini Dar es Salaam.

Hati zilizosainiwa katika kikao hicho zilijumuisha nyanja za ushirikiano wa kidiplomasia, biashara na viwanda, afya na teknolojia ya habari.

Utiaji saini hati hizo ulishuhudiwa na Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk Stergomena Tax na Waziri wa Mambo ya Nje wa Comoro anayeshughulikia nchi za Kiarabu, nchi zinazozungumza Kifaransa, diaspora na utangamano wa Afrika, Mohamed Mbae.

Akizungumza kwenye ufunguzi wa mkutano huo wa kihistoria, Waziri Tax alieleza umuhimu wa kusainiwa kwa hati hizo ni kuwezesha pande hizo mbili kuwa na ushirikiano ulio katika mpangilio mzuri katika nyanja husika, hivyo kuleta tija zaidi.

"Pamoja na kutia saini hati za makubaliano, pia tumekubaliana kuendelea kushirikiana katika maeneo mengine mengi ikiwamo miundombinu, nishati, ulinzi na usalama, uchumi wa buluu, utalii, utamaduni, sanaa na michezo na maendeleo ya vijana," alisema.

Mbae alielezea kufurahishwa na mkutano wa JPC, akieleza umekuwa kiungo muhimu katika kuendelea kukuza na kuimarisha uhusiano kati ya Tanzania na Comoro.