Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Samia: Hatutawavumilia watakaochezea amani yetu

Muktasari:

  • Asisitiza kuwa Serikali haitavumilia watu watakaotumia dini kuchochea chuki na uhasama, hasa kuelekea uchaguzi mkuu. Awaomba viongozi wa dini kushikilia misimamo ya amani na kuzuia wachochezi.

Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan amesema Serikali haimvumilia mtu yeyote atakayetumia dini kuchochea chuki na uhasama nchini, jambo linalohatarisha uvunjifu wa amani na umoja wa kitaifa katika kipindi hiki kuelekea kwenye uchaguzi mkuu.

Rais Samia ameeleza hayo leo Jumatatu, Machi 31, 2025, wakati wa Baraza la Idd El Fitri, lililofanyika jijini Dar es Salaam, akiwa mgeni rasmi, kwa mwaliko wa Mufti wa Tanzania, Abubakar Zubeir.

Amesema jukumu la kusimamia amani nchini ni la Serikali kupitia vyombo vya ulinzi na usalama, na kwa upande mwingine ni jukumu la wananchi wote wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Ameongeza kuwa kwa kiasi kikubwa, ari na morali za wananchi huchochewa na maelekezo ya viongozi wao wa dini.

"Kwa msingi huo, nimewiwa kulitupa jukumu la ulinzi wa amani na utulivu wetu nchini mikononi mwenu viongozi wa dini. Serikali kwa upande wake, italinda na kusimamia misingi ya Katiba ya kuheshimu uhuru wa raia wa kuabudu na kuhubiri dini.

Viongozi mbalimbali pamoja na waumini wa dini ya Kiislamu wakiwa kwenye Baraza la Eid El Fitr ambalo Kitaifa limefanyika leo Jumanne Machi 31, 2025 katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC), Dar es Salaam.

...ila kamwe, hatutamvumilia yeyote atakayetumia haki hii kuchochea chuki na uhasama. Tumeapa kulinda haki na utu wa kila Mtanzania, hivyo hatutasita kufanya wajibu wetu bila woga. Waswahili husema mchelea mwana kulia hulia yeye,” amesema.

Ameongeza kuwa hawatafanya ajizi kushughulika na wavunjifu wa sheria na wachochezi wa vurugu. Amesema dini ibaki kwenye majukumu yake ya msingi ya kulea waumini wake kiimani na kimaadili, kuendana na misingi ya dini zao.

"Kamwe, viongozi wetu wa dini wasidandie ajenda au vishawishi vya kisiasa na kuvuruga nchi yetu. Badala yake, majukwaa ya ibada yatumike kwa ibada, yasitumike na wanasiasa kufanyia propaganda zao.

“Matarajio yetu ni kwamba majukwaa haya yatafanya kazi ya kutuliza hali na kuleta amani pale wanasiasa watakapotibua utulivu ndani ya nchi yetu,” amesema Rais Samia katika baraza hilo la Idd.

Rais Samia Suluhu Hassan akizungumza na waumini wa dini ya Kiislamu pamoja na wageni mbalimbali kwenye Baraza la Eid El Fitr ambalo Kitaifa limefanyika leo  Machi 31, 2025katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC), Dar es Salaam.

Rais Samia amesema Tanzania inatambulika kwa kuwa na amani na utulivu tangu ilipopata uhuru mwaka 1961. Amesema utulivu huo umewezesha utaratibu mzuri wa kubadilishana uongozi wa nchi kupitia utamaduni wa kisiasa wa uchaguzi kila baada ya miaka mitano.

Amesema nchi imeendelea kuwa na umoja na mshikamano kwa sababu viongozi wa dini wanajiepusha na maneno yenye uchochezi na kuleta mifarakano.

"Mwaka huu tunakabiliwa na uchaguzi mkuu, hivyo nawasihi sana viongozi wetu wa dini, tushikilie msimamo wa imani, udhibiti wa nafsi zetu na wajibu wetu katika kuitunza na kuikuza amani yetu nchini.

“Niwaombe, katika madhehebu na makundi yenu mbalimbali, muweze kuwadhibiti wale wachache miongoni mwenu, walio na mwelekeo wa kuhubiri na kupandikiza chuki kwa wananchi dhidi ya Serikali yao,” amesema.

Rais Samia awakabidhi 'rungu' viongozi wa dini kwa wanaohubiri chuki, uhasama

Amesisitiza kwamba katika mifarakano na hasama, hakuna atakayeibuka mshindi, bali kutatokea hasara na majanga kwa taifa.


Mufti aweka msisitizo

Awali, akizungumza kwenye Baraza la Idd, Mufti Zubeir ametaka kutokuvumiliwa kwa kauli zinazohatarisha amani nchini, huku akiwasisitiza Watanzania kuhakikisha wanaitunza amani iliyopo nchini.

Viongozi mbalimbali pamoja na waumini wa dini ya Kiislamu wakiwa kwenye Baraza la Eid El Fitr ambalo Kitaifa limefanyika leo Jumanne Machi 31, 2025 katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC), Dar es Salaam.

Mufti amesema moto mkubwa asili yake ni cheche, na inapotokea na kupuuzwa, kutatokea mlipuko ambao hauwezi kuzimwa. Amesema si vyema kukubali viashiria vinavyoweza kuharibu amani.

"Tupo kwenye mwaka mbaya ambao wanaweza kutokea watu wakaharibu amani… kwa hiyo ni juu yetu kuitunza amani. Mwaka huu ndiyo tunaelekea kwenye uchaguzi mkuu, tunapaswa kuwa na akili ya kuchagua viongozi watakaotufaa,” amesema Mufti.

Mufti amesema hawataacha kulisemea suala la amani kwa sababu ni jambo muhimu na si la kuchezea. Ameongeza kuwa amani ni kitu kinachohitaji kutunzwa na kama haitatunzwa, inaweza kuchafuka.

"Amani ni sawa na yai, ukilishika ulishike kwa uangalifu mkubwa, ukilishika likakuponyoka, hilo yai litavunjika na huwezi kulizoa. Hivyo ndivyo amani inapoharibika kurudisha kwake ni tabu sana,” amesema.

Katika msingi huo, Zubeir amesema nchi zilizochafuka kwa kukosa amani, zinahaha kupata amani, na hata zile zilizopata amani baada ya vita bado zinapitia wakati mgumu kuishi kwa amani.

"Katika nchi yetu hatuwezi kuachia tu hivi, mtu anajaribu kuleta viashiria vya kuharibu amani halafu sisi wenyewe hatuna neno tunamuangalia tu kawaida kwamba ndiyo sawasawa.

“Analeta maneno yasiyo ya kifikra, mtu anaweza kusema ‘acha kinuke.’ Sasa ikishanuka, ndiyo maana yake nini? Ikishanuka, utakaa wewe katika nchi hii? Atakaa shangazi yake katika nchi hii?” amesema.

Mufti amesema mtu anapotaka kufanya jambo lolote ni muhimu kufikiria mwisho wa kile atakachokifanya.

"Tumpime huyo mtu anachotuambia. Anatuambia nini? Nini itatokea? Faida yake ni nini? Nini kitatokea baada ya kumfuata mtu huyo?” amehoji.


Usalama kwa wawekezaji

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, amewahakikisha usalama wawekezaji na wafanyabiashara ndani na nje ya nchi wakati wa uchaguzi mkuu Oktoba mwaka huu.

Viongozi mbalimbali pamoja na waumini wa dini ya Kiislamu wakiwa kwenye Baraza la Eid El Fitr ambalo Kitaifa limefanyika leo Jumanne Machi 31, 2025 katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC), Dar es Salaam.

Amesema mwaka huu wa uchaguzi, wamejipanga kuhakikisha amani inaendelea kutawala kama ilivyo, kwa kuwa hakuna eneo la kukimbilia endapo amani ya Tanzania itaharibika.

"Huu ni mwaka wa uchaguzi na mara nyingi tunapofikia mwaka wa uchaguzi, wawekezaji na wafanyabiashara wakubwa wanapenda kuondoa mitaji yao kwa kuhofia taifa kuingia kwenye machafuko.

“Naomba nitumie nafasi kwa niaba ya wakuu wa mikoa wote, msiogope kuja kuwekeza Tanzania na Dar es Salaam, niwathibitishie katika kipindi ambacho tumejipanga vizuri sana kuhakikisha amani inaendelea kutawala na kubaki hivi ilivyo ni mwaka 2025,” amesema.

Chalamila amesema msingi mkubwa wanaoutumia siyo tu vyombo vya dola, bali wamejipanga kutoa elimu kwa Watanzania kuhusu umuhimu wa amani na kuilinda Tanzania.

Amesema amani ya Tanzania ikiyumba, hakuna baba au mama mwingine wa kukimbilia.

Pia, mkuu huyo wa mkoa amesema katika kuhakikisha amani inatawala nchini, wanatumia viongozi wa dini kuhubiri amani na mambo yote yanayochangia kuwaunganisha Watanzania.


Ombi la Bakwata

Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata) limeiomba Serikali kufanyia kazi dosari zilizojitokeza katika uchaguzi wa Serikali za mitaa mwaka 2024, huku likikemea vitendo vya rushwa na kusisitiza uadilifu kwa wale watakaosimamia Uchaguzi Mkuu 2025.

Katibu Mkuu wa Bakwata, Alhaji Nuhu Mruma, ametoa ombi hilo mbele ya Rais Samia wakati akitoa salamu za Bakwata Taifa katika Baraza la Idd lililofanyika katika Ukumbi wa Mwalimu Nyerere, jijini Dar es Salaam.

"Kupitia jukwaa hili, tunaziomba mamlaka za Serikali kuzifanyia kazi dosari zilizoripotiwa katika uchaguzi wa Serikali za mitaa uliopita na kusisitiza suala la kutenda haki katika kila hatua ya mchakato wa uchaguzi, kwani haki ndiyo msingi mkuu wa amani.

“Tunatoa wito pia kwa vyama vya siasa pamoja na wagombea kuepuka vitendo vya rushwa, kwani rushwa ni adui wa haki,” amesema Alhaji Mruma.

Akijibu ombi hilo, Rais Samia ameahidi kwamba kama Serikali wamejipanga uchaguzi ujao ufanyike kwa haki kwa kusimamia misingi yote ya kanuni, sheria na desturi zote za uchaguzi. Amesisitiza kwamba falsafa ya 4R itaendelea kuwa nyenzo kuu katika uchaguzi ujao.

"Nyote ni mashahidi wa maboresho na mageuzi makubwa tuliyoyafanya kama vile kuruhusu mikutano ya kisiasa kuendelea nchini, Bunge kufanya mabadiliko na kufuta sharti la mgombea kupita bila kupingwa na sasa kila mgombea wa ubunge au udiwani lazima apigiwe kura.

“Vilevile, tumeanzisha Tume Huru ya Uchaguzi iliyokuwa ikidaiwa miaka yote. Tumeweza kufanya haya yote kwa kushirikisha wadau wote wa kisiasa na tulikubaliana hivi,” amesema Rais Samia.