Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mufti, Rais Samia watoa ujumbe wa mshikamano swala ya Idd El Fitri

Muktasari:

  • Asema suala la mapatano umekuwa ugonjwa mbaya hata viongozi wa dini hiyo, hawapatani kutokana na wengine kujiona wanajua zaidi ya wengine, awataka wawe mfano bora.

Dar es Salaam. Mufti na Sheikh Mkuu wa Tanzania, Abubakar Zubeir amewataka viongozi wa dini ya Kiislamu kuwa mfano bora wa mapatano kwenye jamii.

Kiongozi huyo amesema suala la mapatano ni ugonjwa mbaya zaidi kwa viongozi hao kutokana na baadhi kujiona wanajua zaidi ya wengine.

Mufti ametoa ujumbe huo leo Jumatatu Machi 31, 2025 katika swala  ya Idd El Fitri iliyofanyika kitaifa kwenye Msikiti wa Mfalme Mohammed Vi Kinondoni jijini Dar es Salaam.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan  akijumuika na waisalamu wengine  kusali swala ya Eid katika kukamilisha ibada ya Mfungo wa Ramadhan katika Msikiti wa Mohamed VI uliopo katika Makao Makuu ya Baraza Kuu la Waislamu Tanzania  (BAKWATA) Kinondoni Jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kuswali Swala ya Eid El Fitr tarehe 31 Machi, 2025.

Swala hiyo ya Idd El Fitri iliyoanza saa 1:30 asubuhi imehudhuriwa na Rais Samia Suluhu Hassan, Rais mstaafu wa awamu ya nne, Jakaya Kikwete, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Omary Mchengerwa pamoja na waumini wa dini hiyo.

"Hii ni siku ya kushikamana sana na ni siku ya kuondosha vifundo, wale waliogombana leo wapatane, kwa sababu ukifanya hivyo utaingia peponi na milango itafunguka, Mungu hatufundishi tusipatane.

Ugonjwa huu ni mbaya sana na upo kwa mashekh, wengine hawakubaliani, mwingine anajua kuliko mwingine, pataneni mashekh nataka muonyeshe mfano," amesisitiza Mufti.

Kiongozi huyo amesema kutokana na watu kutopatana siku ya mwisho watafika peponi, lakini milango itafunga hadi pale watakapopatana na ndugu zao.

Amesema kufunga kwa milango ya pepo ni kutokana na vifundo ambavyo watu huvibeba na uadui uliopo miongoni mwao.

"Watu siku ya kiama milango itafunga yenyewe kwa sababu ya vifundo na hali ya kutopatana, uadui uliopo baina ya Musilamu na Musilamu, watu wapatane na milango itafunguka," amesema.


Mufti amesema Waislamu ni ndugu kama wa kuzaliwa tumbo moja na wala mtu hapaswi kumdharau ndugu yake au kutomtakia heri.

Awali, Naibu Katibu wa Baraza la Ulamaa, Sheikh Hassan Chizega amewataka Waislamu kuendelea kumtii Mungu hata baada ya mfungo kuisha.

Mbali na hilo amesisitiza Waislamu waendelee kuwa watiifu kwa mamlaka zilizokabidhiwa madaraka.


Ujumbe wa Samia

Katika kurasa zake za kijamii, Rais Samia amewatakiwa heri ya sikukuu hiyo Watanzania:

“Nawatakia nyote kheri ya sikukuu ya Idd al-Fitr. Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema aliyetubariki kuifikia na kuikamilisha Ibada ya Mwezi Mtukufu wa Ramadhani aendelee kutusimamia na kutufanikisha.”


“Tusherehekee kwa amani, umoja, upendo na utulivu. Tuendelee kudumu katika ibada na kumuomba Mwenyezi Mungu aendelee kulijaalia Taifa letu umoja, amani na mshikamano; atuepushe na yote yenye nia ya kutugawa na azidi kutujaalia baraka zake. Idd Mubarak.”


Kuhusu swala ya Idd El Fitri

Idd El Fitri ni sikukuu ya kumaliza mfungo na kutumiwa kuadhimisha mwisho wa mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhan.

Siku hii huwa ni siku rasmi ya mapumziko katika mataifa mengi yenye waumini wengi wa Kiislamu. Hata hivyo idadi ya siku za mapumziko huwa tofauti katika nchi mbalimbali kutegemeana na mwandamo wa mwezi.

Waislamu huanza sherehe hizi kwa kukusanyika kwa maombi ya kila mwaka ambayo hufanyika muda mfupi baada ya machweo.

Alasiri ya leo Jumapili, kutafanyika Baraza la Idd kitaifa katika ukumbi wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam na mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Rais Samia.