Askari Magereza wawili mbaroni wakituhumiwa kusababisha kifo

Muktasari:
- Askari Magereza wawili wanadaiwa kusababisha kifo cha Emmanuel Chacha wakati wakijihami baada ya vijana zaidi ya 20 kuwavamia wakitaka mifugo iliyokamatwa iachiwe.
Mwanza. Polisi Mkoa wa Mara linawashikilia askari wawili wa Jeshi la Magereza kwa tuhuma za kusababisha kifo cha Emmanuel Chacha (18), mkazi wa Kijiji cha Kisangura.
Taarifa ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mara, Pius Lutumo iliyotolewa leo Aprili Mosi, 2025 imesema askari hao wanashikiliwa katika Gereza la Tabora B, wilayani Serengeti.
Amewataja askari hao kuwa, Sijali Hence na Ilinus Mushumbusi wanaodaiwa kusababisha mauaji hayo Machi 31, 2025 saa nne asubuhi.
Inadaiwa tukio hilo lilitokea ndani ya kambi ya mradi wa ufugaji gerezani hapo baada ya askari Magereza watatu waliokuwa zamu kukamata ngo'mbe 98, mbuzi watano na kondoo sita waliokuwa wameingizwa ndani ya eneo la mradi.
"Wakati zinafanyika jitihada za kupeleka mifugo hiyo kuhifadhiwa ndani ya kambi, ghafla walitokea vijana zaidi ya 20 wakiwa na silaha za jadi (mapanga na mishale) na kuwavamia askari hao kwa kuwashambulia, huku wakiwataka kuachia ng'ombe wasipelekwe kambini," imesema taarifa.
Kamanda amesema katika jitihada za kujiokoa kutoka kundi la vijana hao, askari walifyatua risasi kadhaa hewani kwa lengo la kuwatawanya na kati ya risasi hizo moja ilimjeruhi Emmanuel Chacha aliyefariki dunia akiwa njiani akipelekwa hospitalini.
Taarifa imesema Polisi inaendelea na uchunguzi wa kina kuhusu tukio hilo ili kubaini mazingira halisi ya mauaji hayo.
Kamanda Lutumo amewataka wananchi kuzingatia mipaka ya malisho kwa mifugo yao ili kuepusha migogoro isiyo ya lazima.