Prime
Mazito wanayopitia bodaboda ‘popo’

Muktasari:
- Mtaalamu wa afya na mwanasaikolojia waeleza athari za kiafya zinazoweza kuwakabili bodaboda wanaokesha.
Dar/mikoani. Bodaboda wanaokesha kazini ‘popo’ ni sehemu muhimu ya mfumo wa usafiri nchini Tanzania, wakihudumia watu wanaosafiri nyakati mbalimbali ikiwamo usiku kwa sababu mbalimbali.
Usiku bodaboda hupokea abiria wanaotoka kazini, kwenye starehe au wanaohitaji usafiri wa dharura. Lakini kazi hiyo siyo rahisi, ikiwa na hatari nyingi.
Licha ya kipato kinachopatikana, kazi hii ina changamoto lukuki, kutoka kwenye usalama hadi afya na ustawi wa akili, hivyo kuwaweka katika maisha magumu licha ya kuwa ni fursa ya kujenga kesho iliyo bora.
Katika miji na majiji yakiwamo ya Dar es Salaam, Mwanza, Mbeya na Tanga baadhi ya bodaboda hukesha wakitoa huduma kwenye barabara zenye mwanga hafifu, zenye giza, mashimo na kwa nyakati zingine wakipambana na baridi kali.
Wasemavyo bodaboda
Issa Mwakyoma, bodaboda jijini Mbeya anasema baadhi ya maeneo hayana taa za barabarani, hivyo ni rahisi kwa watu wasio waaminifu kuwateka na kuwapora pikipiki baada ya kujifanya abiria.
"Huwa nakesha, kuna mambo mengi. Ni kudra za Mwenyezi Mungu. Kuna wakati namfikisha abiria anakokwenda, akiingia ndani hatoki anatokomea na fedha. Kuna tishio la kuporwa na hata kupata vishawishi kwa wanawake nyakati za usiku," anasema.
Katika hili la vishawishi, bodaboda jijini Tanga anayefanya kazi kwenye kijiwe kilichopo Barabara ya 15 pasipo kutaka kutajwa jina anasema alishawishika kimapenzi mwisho wa siku amezaa na abiria wake, kibaya zaidi ni mke wa mtu.
“Kinachoniuma ni kuona mtoto wangu wa kike amepewa baba mwingine, hili linanitesa kwenye nafsi yangu. Mwenzangu haelewi chochote ni siri yangu na yule mwanamke,” anasema.
Mjini Njombe, Gerald Mwasimba anasema katika kukesha ni rahisi kujikuta ukiishia kwenye mikono ya sheria kwa kupakia abiria wahalifu.
"Mara kadhaa imewahi kutokea unabeba abiria kumbe ni mhalifu anavizia watu wanaoongea na simu ili awapore. Hiyo imewahi kunitokea hapa Njombe nilikodiwa kumbe jamaa anakwenda kupora watu," anasema.
Si hivyo pekee, Mwasimba anasema kuna nyakati maisha yako yanaweka hatarini pasipo kujua baada ya kubeba mzigo kupeleka eneo baadaye unabaini ulibeba dawa za kulevya au hata kiasi kikubwa cha fedha.
Katika hili, Thobias Msigala, bodaboda mjini Njombe anasema wapo walioingia matatani kwa kubeba bangi na mirungi pasipo wao kujua, hadi pale walipokamatwa na polisi.
Julius Mkude (29), mkazi wa Vingunguti Darajani, jijini Dar es Salaam anasema wamekuwa wakikumbana na hatari ya kuporwa pikipiki na wahalifu usiku ambao hujifanya abiria.
“Nilishakutana na wezi walionikodi niwapeleke Gongo la Mboto, eneo walilolitaja sikuwa mgeni nilikubali lakini tukiwa njiani waliniambia nisimame, wakatoa panga na kuamuru niache pikipiki,” anasema.
Anasema aliamua kupambana nao akajeruhiwa na salama yake ilikuwa msaada kutoka kwa watu waliopita wakiwa kwenye gari lenye usajili wa Serikali.
Anasema alipelekwa hospitali, mkewe alimtafuta kwa siku mbili bila mafanikio hadi pale alipopigiwa simu kuwa amelazwa baada ya kupigwa na wahalifu waliotaka kumpora pikipiki.
“Familia yangu waliniambia niache shughuli hii, niliwaambia tutakula nini na ndiyo kazi pekee ambayo naitegemea kwa sasa. Kikubwa ni kuangalia namna ya kujilinda na nachukua tahadhari za kutokwenda safari za nje ya mji, naishia maeneo ambayo nina uhakika kuna watu wengi na kuna pilika nyingi,” anasema.
Juma Abdallah, dreva bodaboda wa jijini Dodoma anasema changamoto ya usiku: “Hata ukipata ajali usiku mara nyingi wenye magari kama wamesababisha hukimbia, lakini hata msaada wa majeruhi huwa mdogo tofauti na mchana anaonekana, Yaani kazi ya bodaboda usiku ni hatari sana.”
Safari kwa waganga
Mjini Morogoro, Oswald Stephano anasema baadhi ya abiria huwapeleka kwa waganga wa jadi na kuna wakati hubeba bidhaa za kutoa kafara na kwenda kuzitupa njiapanda usiku wa manane.
Anatoa mfano wa mteja wake mmoja aliyegombana na mume wake aliyekuwa na uhusiano na mwanamke mwingine, hivyo alimtaka ampeleke kwa mganga akamshughulikie mumewe atulie.
Anasimulia kwa mganga walikaa kwa saa tatu kisha waliondoka na mfuko ambao abiria alimtaka amuhifadhie.
"Tukiwa njiani abiria aliniomba nimuhifadhie mfuko wenye dawa ili usiku aende kutupa njiapanda, kwa kuwa hawezi kwenda nao nyumbani mume wake atauona. Niliufunga mbele ya bodaboda nikamrudisha nyumbani, saa nane usiku alinipigia simu nikamfuata akaenda kutekeleza maagizo ya mganga," amesema.
Bodaboda eneo la Mkuyuni, jijini Mwanza, Fikiri Mwanzo anasema hatasahau siku aliyempakia abiria aliyeshuka makaburini pasipo kujua kile alichokwenda kufanya usiku.
"Aliniambia nimsubiri, nilitetemeka. Kuanzia siku hiyo mwisho wangu wa kufanya kazi ni saa tatu usiku na hubeba abiria ambaye naelewa anaposhukia," anasema.
Hali ya afya
Kutokana na hali ya baridi usiku, baadhi ya bodaboda hawana mavazi maalumu, hivyo kuhatarisha afya zao, huku wengine wakitumia pombe na hata dawa za kulevya kama vile bangi ili kupunguza uchovu au kuondoa hofu wanapokuwa barabarani usiku.
"Tunapokaa kwenye baridi kwa muda mrefu tunajikuta tunakunywa pombe ili kuendelea na kazi. Lakini tunajua si salama, kwa sababu baadhi yetu wamepata matatizo ya kiafya na ajali," anasema Dickson Haule.
Daktari katika Hospitali ya St Anna jijini Dar es Salaam, Salha Salim anasema kazi za usiku huathiri mfumo wa usingizi wa asili.
“Mwili wa binadamu kawaida umezoea kupumzika usiku na kufanya kazi mchana, hivyo kufanya kazi usiku husababisha matatizo ya usingizi, uchovu sugu na ongezeko la hatari ya magonjwa ya akili kama vile msongo wa mawazo,” anasema.
Dk Salha anasema pia wanaofanya kazi usiku wapo kwenye hatari kubwa ya kupata shinikizo la damu na magonjwa ya moyo kutokana na kukosa usingizi wa kutosha na kufanya kazi chini ya msongo wa mawazo.
Anasema wakati mwingine wanakabiliwa na hatari ya matatizo ya mgongo na viungo kutokana na muda mrefu wa kukaa kwenye pikipiki.
“Mwili unapokaa katika mkao uleule kwa muda mrefu, hasa kwenye chombo kinachotikisika kama pikipiki, huongeza mzigo kwenye uti wa mgongo na kusababisha maumivu sugu ya mgongo, shingo na mabega,” anasema Dk Salha.
Asemavyo mwanasaikolojia
Mtaalamu wa saikolojia, Clara Mwambungu anasema watu wanaofanya kazi usiku hukabiliana na changamoto za kisaikolojia zinazohusu hatari wanazokutana nazo kazini na athari hizo si kwao pekee bali pia kwa familia zao.
Kwa waendesha bodaboda anasema wanapokuwa na wasiwasi mkubwa kuhusu usalama wao, mara nyingi hofu huwa mzigo mzito kwa familia zao.
"Waendesha bodaboda hawa wanapoishi kwa hofu ya kushambuliwa au kuingizwa katika ajali, athari hii haishii kwa mtu binafsi, familia zao pia zinahisi athari hizi, kwani inakuwa na hofu kwamba huenda wapendwa wao wasirudi nyumbani salama," anasema Clara.
Anasema wakati mwingine, waendesha bodaboda wanapokuwa katika hali ya wasiwasi au kuishi kwa shinikizo la kiakili, wanakuwa na ugumu wa kushiriki kikamilifu katika maisha ya familia.
Anasema kwa baadhi huwa vigumu kuzungumza na watoto, kushiriki shughuli za familia au kutoa msaada wa kihisia kwa wenza wao kwa kuwa muda wa usiku huwa kazini na anaporejea nyumbani hulala mchana.
“Inapotokea kwamba waendesha bodaboda wanapitia hali ya msongo wa mawazo, wenza wao pia wanajikuta wakikabiliwa na shinikizo la kihisia.
"Mke au mpenzi wa bodaboda wa kazi za usiku anaweza kupata madhara ya mhemko kwa sababu ya kuishi na woga wa kila wakati kuhusu usalama wa mumewe. Hii inaweza kusababisha migogoro ya kifamilia na kupungua kwa mshikamano ndani ya familia,” anasema.
Ushuhuda wa mke
Sikuzani Hamisi, mkazi wa Temeke jijini Dar es Salaam anasema moja ya changamoto anazopitia ni kutokuwa na uhakika iwapo mume wake atarudi nyumbani salama baada ya kazi.
“Kila mara nikisikia sauti ya pikipiki ikirudi, moyo wangu unakuwa na hofu, siwezi kueleza vizuri, lakini kuna aina fulani ya wasiwasi ambayo naipitia. Mume wangu huelekea kazini giza na hurejea nyumbani usiku sana au alfajiri, akiwa mchovu. Mara kadhaa huja na simulizi za ajali au vitisho vya majambazi,” anasema.
Anasema wasiwasi alionao ni iwapo akipoteza maisha, familia itakosa msaada.
“Nikiishi bila yeye, watoto wangu watakuwa na nani? Je, tutapata vipi hela za kuwawezesha katika masomo yao?” anasema akieleza maswali ambayo humpa msongo wa mawazo.
Imeandikwa na Devotha Kihwelo (Dar), Shariff (Morogoro), Bertha Ismail (Arusha), Rajabu Athumani (Tanga), Seif Jumanne (Njombe), Saada Amir, (Mwanza) na Christina Thobias (Iringa)