Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mamlaka zidhibiti bodaboda, wafanyabiashara maeneo hatarishi

Usiku wa kuamkia Ijumaa kumetokea ajali eneo la Stop Over, Kimara jijini Dar es Salaam, ambapo tumewapoteza vijana wetu wanne wapambanaji maarufu bodaboda wakiwa katika harakati ya kujitafutia kipato.

Ni tukio lililoacha simanzi, lililotokana na vijana hao kuparamiwa na lori ambalo mashuhuda walieleza kuwa lilipoteza mwelekeo baada ya kugonga nguzo za taa, kisha kuwaparamia madereva wa bodaboda na wachuuzi wengine waliokuwa pembezoni mwa barabara.

Siyo nia yetu kuelezea kwa undani tukio hilo, bali tunaona ipo haja ya kuangaliwa suala la bodaboda na wafanyabiashara wanaofanya shughuli zao kwenye vituo vya daladala na pembezoni kabisa mwa barabara, jambo hilo liwekewe mkakati mpya kulidhibiti.

Imeshazoelewa madereva wa bodaboda jijini Dar es Salaam na mikoa mingine nchini kupaki kwenye vituo vya daladala au pembeni mwa barabara wakitumia kama stendi zao za kusubiria na kupakia abiria.

Sisi tunaliona hili kama ni tatizo ambalo linatakiwa kutatuliwa mapema, kwani likiota mizizi linaweza kuleta madhara makubwa siku za uzoni.

Madereva hawa mara nyingi huweka pikipiki zao katika maeneo yaliyotengwa kwa mabasi na daladala, jambo ambalo husababisha msongamano na usumbufu kwa abiria na watumiaji wengine wa barabara.

Kwa kiasi kikubwa, hali hii inachangiwa na ukosefu wa maeneo rasmi ya kupakia na kushusha abiria kwa waendesha bodaboda, lakini hatudhani kama ni sababu hilo kuachwa liendelee.

Pia, baadhi yao wanakwepa gharama za kutumia stendi rasmi walizotengewa kwa sababu ya kulipa ushuru au wanapendelea kupaki karibu na vituo vya mabasi ili kuwavutia abiria.

Matokeo yake ni kwamba bodaboda hukaa kwa wingi katika maeneo ambayo ni hatari, na mara nyingine huchangia katika kusababisha ajali kwenye vituo hivyo, kwa sababu daladala nazo hushindwa kuingia vituoni, hivyo kushusha na kupakia abiria zikiwa barabarani.

Vilevile, kuna tabia ya wafanyabiashara kufanya biashara kando ya barabara na wengine hata kupika pembezoni mwa biashara zao, ni hatari kwa watumiaji wa barabara. Hii inajumuisha wauzaji wa matunda, mboga, mavazi na hata kupika chakula.

Wafanyabiashara hawa mara nyingi wanachagua maeneo ya barabarani kwa sababu ya wingi wa watu wanaopita, wakitafuta wateja wa haraka bila kulipa kodi au gharama za upangaji wa maduka, huku wakisahau madhara yanayoweza kutokea au usalama wao.

Biashara kando ya barabara huleta athari mbalimbali. Kwanza, inahatarisha usalama wa wafanyabiashara na wateja wao, kwani magari yanayopita kwa kasi yanaweza kusababisha ajali.

Pili, hali hii inachangia uchafuzi wa mazingira kwa sababu taka za plastiki, karatasi na mabaki ya vyakula hutupwa kiholela.

Tatu, inapunguza nafasi ya waenda kwa miguu, hivyo kuwafanya waingiliane na magari, jambo ambalo linazidisha hatari ya ajali za barabarani.

Aidha, wale wanaopika pembezoni mwa barabara hukumbana na changamoto nyingine kama vile uchafuzi wa hewa unaotokana na moshi wa makaa na majiko ya mkaa.

Moshi huu unaweza kuwa na madhara kwa afya, hususan kwa watoto, wazee na watu wenye matatizo ya kupumua. Pia, kuna hatari ya moto kutokea endapo ikitokea ajali kama ilivyotokea juzi usiku.

Kwa kukabiliana na changamoto hizi, Serikali pamoja na mamlaka husika zinapaswa kuchukua hatua madhubuti. Kwa madereva wa bodaboda, wafanyabiashara ni muhimu kuchagua maeneo ya mbali na barabara wakati mamlaka zikiendelea kushughulikia.