Prime
Bodaboda watajwa vinara kwa umbea

Muktasari:
- Wanandoa, wapenzi waathirika wakubwa, wenyewe wataja kiini cha tatizo kwa jamii.
Dar es Salaam. Kwenye vijiwe vya bodaboda mitaani kuna pilikapilika nyingi, baadhi ya abiria wakiwa na watu maalumu wa kuwabeba, huku wengine wakipanda pikipiki yoyote wanayoikuta kijiweni.
Katika vijiwe hivi wapo madereva maarufu, wacheshi na wachangamfu unaoweza kusema ni watu wa watu. Hakuna abiria anayepanda pikipiki zao pasipo kutabasamu.
Safari iwe ndefu au fupi, wanaweza kukusimulia nani katengana na mke wake, nani kapata kazi mpya na nani alikuwa hospitalini. Ni kama redio inayotembea, huna haja ya kuuliza, habari zitakufikia.
Kutokana na silika yao, kama abiria mmoja alimweleza jambo binafsi, basi kesho yake, mtaa mzima utajua, iwapo mteja tajiri alipanda pikipiki yake akanunua kitu cha bei ghali, watu wengine watajua kabla hata hajashuka nyumbani.
Ushuhuda wa abiria
Kwa hali hiyo, bodaboda hao wamekuwa chanzo cha migogoro, kuvunja uhusiano na hata kuleta uhasama miongoni mwa jamii kama anavyosimulia Mariam Chuwa, mkazi wa Kigamboni jijini Dar es Salaam.
Anasema bodaboda ni chanzo cha yeye kugombana na familia yake akieleza: “Sina hamu nao. Kuna kaka mmoja ni bodaboda alikuwa ananichukua ananipeleka maeneo mbalimbali ya kula bata (ya starehe). Baba yangu ni mtu wa misimamo mambo ya kujirusha hataki.
“Yule boda sijui nini kilimtuma akamsimulia dada yangu kuwa huwa ananipeleka viwanja vya sterehe. Dada akamwambia baba, ilikuwa ugomvi mkubwa hadi leo sina hamu.”
Rehema Ally, mama lishe eneo la Tabata Kimanga anasema baadhi ya madereva wa bodaboda wana tabia ya umbea.
“Huwa wanakuja kula kwenye mgahawa wangu, stori zikikolea wanaanza kusema mwanamke yule nilimpeleka gesti Buguruni. Watu wasipende kutoa siri kwa bodaboda maana wataaibika,” amesema.

Odemba Sozi, mkazi wa Tegeta jijini Dar es Salaam amesema ndoa ya dada yake ilivunjika kwa sababu ya dereva wa bodaboda.
“Dada yangu anaishi Mbezi Luis, walikuwa na bodaboda wanayemtumia. Dada alikuwa na rafiki yake wa kiume na alikuwa anamtumia huyo bodaboda kumpeleka kwenda kuonana naye.
“Uvumilivu ulimshinda dereva wa bodaboda akamwambia shemeji yangu, ukaandaliwa mpango. Siku moja akampeleka kisha akampigia simu shemeji wakaenda kumfumania, hadi leo ndoa haipo,” anasema.
Juma Mohamed, mkazi wa Mbagala Mbande jijini Dar es Salaam, anasema madereva wa bodaboda wanatakiwa kutambua siyo kila anayekwenda nyumba ya wageni ni mzinifu.
“Mara nyingi binadamu hufikiria tofauti. Bodaboda wanaweza wakafikiria hawa watu wanakwenda kufanya vitu hivi lakini kumbe siyo. Mfano mtu anakwenda nyumba ya wageni kupumzika ameona nyumbani kuna kelele, lakini yeye anayembeba anachukua na kupeleka kwa mtu tofauti,” anasema.
Kauli za bodaboda
Samsom John (siyo jina halisi), dereva wa bodaboda kwa miaka sita katika kijiwe cha Tabata Relini anasema wapo wambea lakini wengine ni madereva wa teksi na bajaji.
“Madereva wa bodaboda kwa asilimia kubwa tuna siri, nimewahi kuokoa mahusiano ya watu. Unakuta nimempeleka mwanamke sehemu, kumbe mume wake naye kanipigia nimpeleke sehemu hiyohiyo. Kwa hiyo nampigia simu namwambia namleta mume wako mazingira hayo fanya utoke, nakuwa nimeokoa mahusiano ya watu,” amesema.
Said Mohamed (siyo jina halisi), derava wa teksi katika kijiwe cha Ubungo Maziwa anasema umbea ni tabia ya baadhi ya madereva vijiweni.
"Sitaki kukuficha, hapa kijiweni kwetu kuna muda tunaishiwa stori tunaanza kuwajadili wateja. Lakini siyo kwa ubaya ni katika namna ya kuchangamsha genge ili muda uende.
"Nimekumbuka mbali sana kuna dereva sitaki kumtaja jina alipigwa kofi na mume wa mtu kisa umbea. Huyo jamaa alipeleka umbea kwa mke wa mteja kwamba mumewe amekodi teksi akiwa na mchepuko, sasa kumbe yule ni mdogo wa yule kaka,” anasema.
“Mwanamume karudi nyumbani inavyoonekana mwanamke akamwambia aliyoambiwa, jioni hiyo-hiyo hapa kijiweni palichimbika," anasema.
Kwa upande wake, dereva wa bodaboda kijiwe cha Kariakoo, Vincent Musa (siyo jina halisi) anasema siri za wateja wao zinawapa manufaa.
“Tuna siri za watu nyingi na zinatupa manufaa, hatuwezi kutoa kwa mtu maana kazi zetu ni kusafirisha abiria. Tunakutana na changamoto nyingi kama hizo, pia huwezi kufikisha taarifa hiyo kwa mtu anayemjua inakuwa siyo vizuri,” anasema.
Amos Tamba, amesema katika miaka 10 ya kazi yake ya udereva wa bodaboda amepeleka watu sehemu mbalimbali, zikiwamo nyumba za kulala wageni na kwa waganga wa kienyeji.
“Mimi ni mstaarabu siwezi kuongea mbele za watu licha ya kuwa najua kule gesti anaenda kufanya nini. Maana kuna wakati unapigiwa simu na mwanamume anakuelekeza mfuate mtu fulani umlete na baada ya muda unaambiwa ukamchukue. Ukimsimulia mume wa mtu kwamba mkeo nimempeleka nyumba ya wageni inakuwa umempa mada akifika nyumbani anageuka mbogo,” anasema.
Shabani Msunde, anasema yeye kikubwa anaangalia pesa.
“Sisi bodaboda tunatoa huduma za kijamii, siwezi kutoa siri za wateja wangu na mpaka mtu amekwambia mambo yako ujue amekuamini. Sasa wewe utangaze ili iweje, ushauri wangu mtu usimpe siri mwingine maana hii dunia hatuaminiani kabisa mambo yako kaa nayo,” anasema.
Mamlaka za mtaa
Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Kimanga Darajani, jijini Dar es Salaam, Marius Alphonce anasema amewahi kupokea malalamiko kuhusu dereva wa bodadoda aliyetishia kutoa siri za abiria wake.
“Kuna binti alikuja hapa baada ya kugombana na dereva, nakumbuka yule bodaboda alisema anajua siri nyingi za yule dada sasa wanapoelekea kama hawaaminiani patakuwa pabaya, atatoa siri zake. Nilisuluhisha yakaisha," anasema.
Mtazamo wa kisaikolojia
Rais wa Chama cha Wanasaikolojia Tanzania (Tapa), Dk Magolanga Shagembe anasema mara nyingi tabia ya umbea hutokana na vitu mtu anavyoviona mara kwa mara kwenye mazingira yake.
"Kuna umbea na kuongea sana, yupo mtu anaongea lakini haongei umbea. Hiyo ni haiba, yaani zile sifa ambazo mtu anakuwa nazo na anazionyesha mara kwa mara, mfano bodaboda wapo ambao wanatuza na wasiotunza siri.
"Wapo watu wengine ambao siyo bodaboda lakini wakifahamu jambo la mtu mwingine hawawezi kukaa nalo. Lazima atafute mtu mwingine wa kumsimulia, wapo bodaboda pia ambao hawana haiba ya kukaa na jambo la watu,” anasema.
Anasema wanaotoa siri siyo kwamba wamepanga, bali ni katika kutaka kujionyesha na kutawala mijadala hutamani kuleta taarifa mpya ambazo watu hawafahamu, hivyo hujikuta wakisimulia hadi mambo ya watu.
"Anajikuta amefilisika kwenye stori, lazima aende kwenye benki ya stori zake. Kwa upande wa bodaboda benki yake inatokana na abiria anaowabeba, wapo wenye uwezo wa kuishiwa wakanyamaza lakini wapo ambao wakiishiwa wanatafuta chochote ili wazungumze.
"Watu wa aina hiyo katika makundi ya binadanu kwa Kiswahili wanaitwa Msondani (sanguine) ni wale ambao wanaongea sana, watu ambao ubongo wao ulivyo hauwezi kufikia utoshelevu wa ndani mpaka uweze kusisimuliwa na mazingira ya nje.
“Hawa wanaongea sana na kupokea maneno, hata sehemu za kelele wanaweza kusoma na wakaelewa kwa sababu ili ubongo uweze kufikia kiwango cha juu unatakiwa kusisimuliwa kutoka nje," anasema.
Msondani ni wazungumzaji na wachangamfu, hupenda kuwashirikisha wengine mambo yao.
Mtaalamu wa saikolojia, Yisambi Mbuwi anasema baadhi ya watu kwa asili hawawezi kutunza vitu kwa muda mrefu.
"Kutokana na haiba anapiga umbea siyo kwa sababu anapenda ni kwa sababu ya kupata nafuu. Kuna baadhi ya watu haiba yao ni usiri, anaweza hata kufanyiwa tukio baya na asiseme.
"Kuna wengine jambo lisifike kwake ni lazima azungumze. Wenye asili hiyo tunasema huwezi kuwaambia kitu, kwa sababu hata siri zao hawawezi kuzitunza. Ili asikie amani lazima azungumze na mara nyingi wanakuwa na marafiki wengi," anasema.
Anasema tabia hiyo inakuwa kama ugonjwa wa kutotunza siri kwa muda mrefu, ni ngumu kubadilika labda kupunguza. Mara nyingi mtu huzaliwa nayo lakini mazingira yanaweza kuiongeza