Mufti awaka, akemea wanaojaribu kuchokonoa amani

Muktasari:
- Baraza la Idd limefanyika jijini Dar es Salaam, huku Kiongozi wa Waislamu Tanzania akitaka amani itunzwe na wale wanaojaribu kuiharibu waache.
Dar es Salaam. Mufti na Sheikh Mkuu wa Tanzania, Abubakar Zubeir, ametaka kutokuvumiliwa kwa kauli zinazohatarisha amani nchini, huku akiwasisitiza Watanzania kuhakikisha wanaitunza amani iliyopo nchini.
Mufti amesema moto mkubwa asili yake ni cheche, na inapotokea ikapuuzwa, kutatokea mlipuko ambao hauwezi kuzimwa. Amesema si vyema kukubali viashiria vinavyoweza kuharibu amani.
"Tupo kwenye mwaka mbaya ambao wanaweza kutokea watu wakaharibu amani. Mimi sina pa kukimbilia, kwa hiyo ni juu yetu kuitunza amani. Mwaka huu ndiyo tunaelekea uchaguzi mkuu, tunapaswa kuwa na akili ya kuchagua viongozi watakaotufaa," amesema Mufti katika Baraza la Idd El Fitri lililofanyika Dar es Salaam, huku mgeni rasmi akiwa ni Rais Samia Suluhu Hassan.
Mufti amesema hawataacha kulisemea suala la amani kwa sababu ni jambo muhimu na si la kuchezea.
Amesema amani ni kitu kinachohitaji kutunzwa, na kama haitatunzwa, inaweza kuchafuka.
"Amani ni sawa na yai, ukilishika, ulishike kwa uangalifu mkubwa. Ukilishika likakuponyoka, hilo yai litavunjika na huwezi kulizoa. Hivyo ndivyo amani inapoharibika—kurudisha kwake ni tabu sana," amesema.
Katika msingi huo, Sheikh Zubeir amesema nchi zilizochafuka kwa kukosa amani zinahaha kupata amani, na hata zile zilizopata amani baada ya vita bado zinapitia wakati mgumu wa kuishi kwa amani.
"Katika nchi yetu hatuwezi kuachia tu hivi, mtu anajaribu kuleta viashiria vya kuharibu amani halafu sisi wenyewe hatuna neno, tunamuangalia tu kawaida tu kwamba ndiyo sawasawa.
“Analeta maneno yasiyo ya kifikra, mtu anaweza kusema ‘acha kinuke.’ Sasa ikishanuka, maana yake nini? Ikishanuka, utakaa wewe katika nchi hii? Atakaa shangazi yake katika nchi hii?" amesema.
Mufti amesema mtu anapotaka kufanya jambo lolote ni muhimu kufikiria mwisho wa kile atakachokifanya.
"Tumpime huyo mtu anachotuambia. Anatuambia nini? Nini itatokea? Faida yake ni nini? Nini kitatokea baada ya kumfuata mtu huyo?" amehoji.
Kutokana na kauli hiyo, Mufti alitupa dongo gizani akisema, "Kizuri chajiuza, kibaya chajitembeza," akisistiza kuwa mwenye akili huambiwa kidogo na kuelewa sana.
Mbali na hayo, ametoa wosia kwa Waislamu kwamba hawawezi kupata maendeleo katu, abadan, kwa utaratibu walionao wa kuhitilafiana na kuacha kupatana kwenye mambo yanayohusu maendeleo.
Amesema Waislamu wasitarajie kupata maendeleo ya aina yoyote kwa hali hiyo, ndiyo maana kote ulimwenguni masheikh na taasisi kubwa za Kiislamu zinafanya juhudi za mikutano mbalimbali kuzungumzia hitilafu zilizopo ili kuwarudisha watu sehemu moja.
"Wosia wangu kwa Waislamu: ili tupate maendeleo, lazima tuache na tuzipuuze hitilafu zilizopo. Kila mmoja aendelee anavyoona yeye, lakini lengo letu liwe ni Uislamu na maendeleo," amesema.