Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Samia ataka wanawake kujitathmini kurekebisha maadili

Rais, Samia Suluhu Hassan akizungumza katika Kongamano la Wanawake wa Kiislam kuelekea maadhimisho ya Mwaka Mpya wa Kiislamu 1445 Hijiria.

Muktasari:

  • Rais Samia Suluhu Hassan amewataka wanawake kuwa msingi wa suluhu ya changamoto ya maadili nchini.

Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan amewataka wanawake kujifanyia tathmini ili kuona namna ya kukabiliana na changamoto ya mmomonyoko wa maadili nchini.

Tathmini hiyo, ametaka ianze kwa wanawake kujiangalia uwezo wao wa kulishughulikia hilo, udhaifu wao na vikwazo wanavyotarajia kukutana navyo katika kazi hiyo.

Rais Samia ameyasema hayo leo Julai 16, 2023 alipohutubia katika Kongamano la Wanawake wa Kiislam kuelekea maadhimisho ya Mwaka Mpya wa Kiislamu 1445 Hijiria.

“Katika kurekebisha maadili yaliyomomonyoka, tuangalie fursa zetu ni zipi, tunaweza kufanya nini, fursa ya kwanza walimu wazuri tunao, Serikali inatuunga mkono, wengi wanajitokeza kutoa mihadhara kuwawezesha wengine,” amesema.
Baada ya kuangalia fursa, amesema eneo lingine wanalopaswa kujua ni vikwazo vya kuyafikia hayo wanayoyatarajia.

“Unakuta wifi yako ana kazi nzuri anatoka anakwenda kufanya kazi, unakwenda kwake usipomkuta unasema mwanamke gani hatulii nyumbani, hivi ndivyo vikwazo vyenyewe,” amesema.

Baada ya kuangalia hatua zote, Rais Samia amesema wanapaswa kurudi kwa Serikali kuieleza eneo wanaloweza kufanya ili kurekebisha mmomonyoko wa maadili.

Hata hivyo, mkuu huyo wa nchi amewataka Watanzania kulinda amani, akisema ndiyo msingi wa maendeleo na uchumi wa taifa lolote duniani.

“Juzi nilikuwa namsikiliza Mkurugenzi wa Kituo cha Uwekezaji akawa anaeleza Mei na Juni ndiyo miezi aliyopokea miradi mingi ya uwekezaji, ametaja na gharama zake.
“Lakini hayo yametokea kwa sababu kwa jirani panawaka moto, sisi kwetu kuna amani, mwekezaji hawezi kwenda eneo akiambiwa kuna fujo,” amesema.

Akizungumza katika kongamano hilo, Sheikh Ayzuddin kutoka Kenya amemuomba Rais Samia kutuma Tume maalum kwa ajili ya kukwamua vikwazo vya usafiri katika mpaka wa Horohoro na Lungalunga kutoka Kenya kuingia Tanzania.

“Tunasikia ushirikiano lakini wallahi mtu bora upate safari ya kutoka Mombasa kwenda Canada kuliko upate safari ya kutoka Mombasa kwenda Tanga,” amesema.
Ameeleza safari ya kutoka Kenya kuja Tanzania katika mipaka hiyo kuna unyanyasaji mwingi na vikwazo kwa wasafiri na hata wafanyabiashara.

“Kila ninapopata safari ya kuja nchini Tanzania mara zote naomba dua zote,” amesema. Kuhusu hilo, Rais Samia amejibu atalishughulikia.