Prime
Sajini wa Jeshi la Polisi atupwa jela maisha kisa mirungi

Babati. Ama kweli sheria ni msumeno, hii ni baada ya askari wa Jeshi la Polisi nchini mwenye cheo cha Sajini, kuhukumiwa kifungo cha maisha jela kwa kuacha wajibu wake wa kulinda raia na mali zake na kusafirisha dawa za kulevya.
Ni tukio ambalo unaweza kuliona kama sinema (movie) kwa jinsi askari huyo, akiwa na Gari Nissan Patrol, alivyopita kwa mwendo wa hatari nje ya kituo cha Polisi Mbulu, jambo lililowashtua Polisi na kuanza kulifuatilia.
Bila kutarajia na katika hali iliyowaacha midomo wazi Polisi, ni kuwa baada ya kulikamata gari hilo ndipo wanagundua waliyekuwa wakimfukuza ni askari mwenzao mwenye cheo cha Sajini, Ismail Katenya mwenye namba F.3544.
Ndani ya gari hilo, kulipatikana mabunda 380 ya dawa za kulevya aina ya mirungi yenye uzito wa kilo 160.9, kosa ambalo linaangukia katika sheria ya usimamizi na udhibiti dawa za kulevya na kosa la uhujumu uchumi.
Tukio hilo lilitokea Januari 22, 2024 baada ya sinema hiyo ya kufukuzana kufika mwisho na Polisi kufanikiwa kumtia mbaroni mwenzao eneo la Silaloda Wilaya ya Mbulu mkoani Manyara, akiwa na dawa hizo za kulevya aina ya mirungi.
Ni kutokana na uzito wa ushahidi uliotolewa na mashahidi saba wa Jamhuri dhidi ya askari huyo wa zamani wa Jeshi la Polisi, Jaji John Kahyoza wa Mahakama Kuu Kanda ya Babati, amemtia hatiani na kumuhukumu kifungo cha maisha jela.
Hukumu hiyo imetolewa Juni 2,2025 na kuwekwa katika mtandao wa Mahakama leo Juni 3,2025, ambapo Jaji alisema kuwa pasipo kusita, mshtakiwa huyo alipatikana na dawa hizo za kulevya zenye uzito wa kilo 160.9.
Ushahidi uliomfunga
Shahidi wa kwanza, Mrakibu Msaidizi wa Polisi, Athuman Mweluvimbo ambaye alikuwa mkuu wa upelelezi wilayani Mbulu, alisema siku ya tukio kuna gari lilipita kwa mwendo kasi katika barabara nje ya kituo cha Polisi.
Aliileza Mahakama kuwa maofisa wa Polisi walilifuatilia huku Mweluvimbo naye akiwa katika kufukuzana huko, lakini akiwa katika gari lingine na kufanikiwa kulikamata gari hilo aina ya Nissan Patrol katika eneo la Silaloda.
Mweluvimbo akitumia tochi, alimulika ndani ya gari hilo na kuona mifuko miwili yenye rangi nyeusi, mifuko minne ya rangi ya udhurungi na mfuko mmoja wa salfeti ikiwa katika kiti cha nyuma, ikitoa harufu inayofanana na ya mirungi.
Baada ya kubaini hivyo, maofisa hao walitafuta shahidi huru ambaye ni mwenyekiti wa kitongoji cha mtaa wa Harka, Zaituni Rajabu aliyekuwa shahidi wa tatu kwa kuwa katika eneo la tukio, waliokuwepo ni maofisa wa Polisi pekee.
Gari hilo lilipelekwa hadi kituo cha Polisi Mbulu ambako upekuzi ulifanyika na kupatikana mabunda 380 ya majani yaliyodhaniwa ni mirungi, ambapo hati ya ukamataji iliandikwa na kusainiwa na vielelezo hivyo kuhifadhiwa stoo.
Gari aina ya Nissan Patrol rangi ya bluu na mifuko iliyokuwa na mirungi ilitolewa mahakamani kama kielelezo.
Mwaluvimbo baada ya kupima uzito wa majani yale walibaini yalikuwa na uzito wa kilo 160.9 ambapo sampuli za dawa hizo zikiwa na uzito wa gramu 10 zilipelekwa na shahidi wa sita, Erasto Laurence kutoka Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali.
Baada ya kufanya vipimo vya maabara, ilithibitika ni dawa za kulevya aina ya mirungi ambapo aliandika ripoti na kumkabidhi shahidi wa tano, Mkaguzi Msaidizi, Msuya aliyepeleka sampuli hiyo ili airudishe Polisi Mbulu.
Ukiacha mashahidi hao, wengine wa Jamhuri ambao ni maofisa wa Polisi walioshiriki katika ukamataji na upelelezi, walieleza namna walivyolifukuza gari lililokuwa limebeba mirungi hiyo na kufanikiwa kulikamata Silaloda.
Utetezi wa mshtakiwa
Katika utetezi wake, mshtakiwa alikanusha vikali kutenda kosa hilo na kueleza kuwa alikamatwa Januari 22,2024 saa 7:10 usiku katika ajali ya gari iliyohusisha maofisa wa Polisi na hakukamatwa katika tukio la kusafirisha dawa za kulevya.
Alieleza kuwa Polisi walitumia nguvu, kumpiga na kumkamata bila kufuata taratibu na kusisitiza kuwa kesi nzima ilianzia kwenye ajali na madai ya kupatikana na dawa hizo za kulevya aina ya mirungi yalikuwa ni ya kutengeneza.
Alijitetea kuwa Polisi hawakumwambia sababu za kumkamata wala kuonyeshwa mahali ambako dawa hizo zilipatikana na upekuzi haukufanyika eneo la tukio bali kituoni, lakini hati ya ukamataji ilionyesha ilijazwa eneo la tukio.
Kwa mujibu wa mshtakiwa, alilalamika kuwa mnyororo wa utunzaji wa vielelezo (chain of custody) ulikatika kutoka eneo la tukio hadi inatolewa mahakamani, kama kielelezo na wala hakupewa nakala ya risiti ya ukamataji wa dawa hizo.
Hukumu ya jaji
Katika hukumu yake, Jaji Kahyoza alirejea ushahidi wa mashahidi wa Jamhuri ili kujibu swali iwapo mshtakiwa alikamatwa na dawa hizo na hakuna ubishi katika uchunguzi wa awali, alikiri ndiye alikuwa akiendesha gari hilo.
Jaji alisema kuna ushahidi wa Mweluvimbo na Mkaguzi Msaidizi wa Polisi, Clemence Msuya, ambao walieleza bila kutetereka kuwa gari alilokuwa akiendesha mshtakiwa lilipatikana na mizigo iliyodhaniwa ni mirungi.
Kulingana na ushahidi wa Mweluvindo, baada ya kuona hivyo walitafuta shahidi huru kushuhudia na hapo ndipo hati ya ukamataji ilijazwa, lakini upekuzi rasmi na kupima uzito wa mirungi hiyo ulifanyika kituo cha Polisi Mbulu.
Jaji alisema katika utetezi wake mshtakiwa alijitetea kuwa gari hilo lilikaguliwa kwa kusababisha ajali kabla ya kupambazuka na hapakuwepo mkaguzi wa magari wa Polisi (vehicle inspector), jambo alilodai lilikuwa kinyume cha taratibu.
“Ninaona hii simulizi kuwa alihusika katika ajali ilikuja baadaye kama kujinasua. Utetezi wala hawakumuuliza Mweluvindo maswali ya dodoso kwa nini walimkamata mshtakiwa kwa kosa la ajali ya kumbambika kesi ya dawa.”
Jaji aliongeza kusema kuwa:- “Kuhusiana na malalamiko ya jumla ya mshtakiwa kuhusiana na upekuzi kufanywa kabla hakujapambazuka, naona upekuzi huo wa gari Nissan Patrol ulikuwa ni halali kwa vile ulikuwa ni wa dharura”
“Mshtakiwa pia alihoji uhalali wa Mweluvimbo kumkamata mshukiwa wa dawa za kulevya wakati yeye sio Ofisa wa Mamlaka ya Kuzuia dawa za Kulevya. Polisi wana mamlaka kukamata yeyote anayetuhumiwa kwa uhalifu wowote.”
Jaji alitupilia mbali hoja ya mshtakiwa kuwa hakupewa nakala ya risiti ya ukamataji wa mizigo iliyokutwa ndani ya gari lake akisema, alisaini kielelezo hicho namba P3 ambacho ni ushahidi uliojitosheleza kuwa alikamatwa na dawa hizo.
Alisema anashawishika kuamini mshtakiwa alikamatwa akisafirisha majani ambayo awali yalidhaniwa ni dawa za kulevya, lakini baadaye kupitia kwa Mkemia Mkuu wa Serikali ilithibitishwa ni dawa aina ya mirungi.
Jaji alisema Mahakama inaridhika kuwa mizigo iliyopatikana katika gari alilokuwa akiendesha mshtakiwa ni mirungi na mshtakiwa hakupinga kielelezo namba P6 ambayo ni ripoti ya uchunguzi kutoka Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali.
“Utetezi wa mshtakiwa kuwa alikamatwa kimakosa kutokana na ajali kati yake na polisi hauungwi mkono na ushahidi. Utetezi haukuibua mashaka kutikisa ushahidi wa Jamhuri hivyo waliweza kuthibitisha shitaka pasipo kuacha mashaka”alisema.
Katika hitimisho, Jaji alimtia hatiani polisi huyo na kumuhukumu kifungo cha maisha jela ambayo ni sheria inayotajwa na sheria ya kusimamia na kuzuia usafirishaji wa dawa za kulevya, ikisomwa pamoja na sheria ya uhujumu uchumi.