Waliohukumiwa miaka 30 kwa kusafirisha mirungi waachiwa huru

Muktasari:
Walioachiwa huru ni aliyekuwa mfanyakazi wa Mfuko wa Pensheni kwa Watumishi wa Umma (PSSSF), Anitha Oswald na dereva teksi, Frank Sifael
Arusha. Mahakama ya Rufaa imewaachia huru watu wawili waliokuwa wamehukumiwa kifungo cha miaka 30 jela kwa kosa la kusafirisha dawa za kulevya aina ya mirungi zenye uzito wa kilo 214.87.
Walioachiwa huru ni aliyekuwa mfanyakazi wa Mfuko wa Pensheni kwa Watumishi wa Umma (PSSSF), Anitha Oswald na dereva teksi, Frank Sifael.
Uamuzi huo umetolewa baada ya Mahakama ya Rufaa kubatilisha hukumu ya awali, ikibaini kuwa ushahidi uliowasilishwa haukuthibitisha pasipo shaka kosa lililokuwa linawakabili.
Mahakama hiyo imefikia uamuzi huo baada ya kujiridhisha na hoja za rufaa zilizotolewa na Anitha na Frank, pamoja na kushindwa kwa upande wa mashtaka kuthibitisha shtaka hilo.
Hukumu ya kuwaachilia huru imetolewa Mei 28, 2025 na jopo la majaji watatu Ferdinand Wambali, Ignas Kitusi na Paul Ngwembe.
Nakala ya hukumu hiyo imewekwa kwenye tovuti rasmi ya Mahakama kwa ajili ya umma.
Upande wa mashtaka ulidai kuwa, tukio hilo lilitokea Desemba 19, 2019 katika eneo la majengo kwa Mtei, Wilaya ya Moshi mkoani Kilimanjaro.
Ilidaiwa kuwa, warufani hao walikutwa wakisafirisha dawa za kulevya aina ya mirungi.
Awali, Mahakama Kuu Divisheni ya Rushwa na Uhujumu Uchumi (Moshi), iliwahukumu kifungo hicho Septemba 8, 2020.
Katika kesi ya msingi upande wa mashtaka ulikuwa na mashahidi saba ambao ni Joyce Njisya (PW1), F 1157/Sajenti Hashim (PW2), E 7853 Evodius (PW3), Adballah Seleman (PW4), F 9950 Isaack(PW5), Ezekiel Midala (PW6) na H 3923 Michael (PW7).
Kwa upande wa utetezi, Anitha alimtumia shahidi mmoja, Monica John, wakati mrufani wa pili aliwasilisha mashahidi wawili, Oliver Mlay na Filomena Antony.
Maelezo ya onyo yaliyotolewa na warufani hao yalikubaliwa na Mahakama kama vielelezo vya upande wa utetezi.
Ushahidi wa upande wa mashtaka ulidai kuwa siku ya tukio, askari wa Moshi walipokea taarifa kuwa gari aina ya Toyota Sienta lilikuwa likisafirisha dawa za kulevya.
Mashahidi PW3 na PW6 walianza kufuatilia gari hilo na kufanikiwa kuliona eneo la Nakumat.
Baadaye, mashahidi hao walipata taarifa kuwa gari hilo limepata ajali eneo la Majengo kwa Mtei, baada ya kugonga uzio wa nyumba inayomilikiwa na shahidi PW4.
Kabla ya tukio hilo, gari hilo liligonga nyumba ya Edwin Makundi lakini lilifanikiwa kuendelea hadi pale lilipopata ajali.
PW3 na PW6 walitoa ushahidi kwamba, kabla hawajafika eneo la ajali, ghafla walimwona dereva(Frank), akishuka kutoka gari na kuanza kukimbia.
Walidai kuwa, walimtambua dereva huyo kwa sababu walikuwa wakipata huduma zake mara kwa mara wakati wa utekelezaji wa majukumu yao ya kiuchunguzi.
PW3 alianza kumfukuza dereva huku akimuita jina, lakini alifanikiwa kutokomea kusikojulikana hadi alipokamatwa Januari 22, 2018 eneo la Panone, Daraja la Maili Sita, Wilaya ya Hai akiwa njiani kuelekea Arusha akitokea Moshi huku akiendesha gari aina ya Toyota RAV4 yenye namba za usajili T 921 CRQ.
Siku ya tukio katika eneo la Majengo, PW6 na PW3 walilisogelea gari hilo lililopata ajali na kufanikiwa kumuona Anitha aliyekuwa amenasa ndani ya ‘air bag’ ambaye alisaidiwa kutoka nje.
PW6 alidai, alikagua gari na kuona baadhi ya mifuko aliyoshuku kuwa na dawa za kulevya na aliamini watu waliofika na kuzingira eneo la tukio wangesababisha fujo.
Alieleza kuwa, aliomba msaada kwa askari polisi wengine wa Kituo cha Polisi Majengo na gari hilo lililokuwa na namba za usajili T 674 DLB, lilikokotwa na gari lingine hadi ofisi ya RCO.
PW6 alisema katika gari hilo kulikuwa na mifuko ya salfeti nane na kati ya hiyo sita ilikuwa mikubwa na mingine midogo yenye rangi nyeupe na ilikabidhiwa kwa PW5 aliyeipeleka kwenye Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali (CGC) iliyopo Arusha na Mwanza na baada ya uchunguzi ilibainika ni dawa za kulevya aina ya mirungi.
Anitha alikiri kuwa ndiye mmiliki wa gari lililokamatwa eneo la tukio baada ya kupata ajali, lakini alikataa kuhusishwa na dawa za kulevya zilizokamatwa katika gari hilo.
Mrufani huyo aliieleza Mahakama kuwa, siku hiyo alikodisha gari kwa Frank aliyekuwa amepeleka wasafiri Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA).
Alieleza kuwa saa tisa alimuita Frank eneo la Nakumat ili akachukue baadhi ya vitu alivyokuwa amesahau ndani ya gari hilo ili yeye aende Arusha kumuona mama yake aliyekuwa anaumwa na kudai alipokutana na Frank aligundua gari lilikuwa chafu na kulikuwa na mfuko mmoja wa salfeti nyuma ya kiti cha dereva.
Alieleza kuwa, Frank alimuomba aende naye hadi nyumbani kwake akashushe begi kisha amkabidhi gari na kuwa, wakiwa njiani alianza kuongeza kasi huku akibaini kuwa gari la polisi lilikuwa likiwakimbiza hadi walipopata ajali eneo la Majengo.
Anitha alikana kukutwa na kielelezo cha tano, ambacho ni dawa za kulevya, katika gari lake lililokamatwa eneo la tukio.
Alieleza kuwa, gari hilo lilipelekwa ofisi ya RCO na askari polisi, huku yeye mwenyewe akipelekwa katika nyumba ya Frank kwa ajili ya ukaguzi.
Aidha, hata baada ya upekuzi wa nyumba hiyo, hakukupatikana dawa zozote za kulevya.
Shahidi wa pili (Monica) ambaye ni mfanyakazi kutoka PSSSF aliunga mkono ushahidi wa Anitha kuwa alitoka ofisini siku ya tukio na alikuwa akielekea Arusha kumhudumia mama yake mzazi aliyekuwa mgonjwa.
Hata hivyo, Frank alikana kuhusika na tukio hilo akisema hakuwa dereva wa gari hilo lililoelezwa kukutwa na dawa hizo za kulevya na siku hiyo alikuwa akiendesha gari lingine.
Jaji aliyesikiliza kesi hiyo alieleza kuwa upande wa mashtaka umethibitisha kesi hiyo bila kuacha shaka, kuwatia hatiani na kuwahukumu adhabu ya kifungo cha miaka 30 jela kila mmoja.
Rufaa
Katika rufaa hiyo, Anitha alikuwa na sababu sita ikiwamo Mahakama ilikosea kisheria kuwahukumu kutokana na mlolongo wa ulinzi wa kielelezo cha tano (dawa hizo za kulevya) ukiwa shaka.
Nyingine ni Mahakama kukosea kumtia hatiani kwa kutegemea udhaifu wa utetezi wake na kuhamisha mzigo wa uthibitisho na kuwa kesi hiyo haikuthibitishwa bila kuacha shaka.
Mrufani wa pili alikuwa na sababu nne ikiwamo Mahakama kukosea kumtia hatiani huku mlolongo wa uhifadhi wa kielelezo cha tano na uhalisia wa cheti cha ukamataji ukitia shaka pamoja na ushahidi wa upande wa mashtaka kutofautiana kuhusu kielelezo hicho.
Nyingine ilikuwa ni Mahakama hiyo kukosea kukataa utetezi wake bila sababu za msingi na kuwa kosa dhidi yake halikuthibitishwa bila kuacha shaka.
Anitha aliwakilishwa na mawakili Warehema Kibana na Erick Akaro huku Frank akiwakilishwa na mawakili Majura Magafu na Emanuel Antony na mjibu rufaa (Jamhuri) akiwakilishwa na mawakili Grace Madikenya na Philbert Mashurano, waliopinga rufaa hiyo.
Wakili Magafu aliunga mkono hoja za wakili wa kwanza wa mrufani kuhusu utunzaji wa dawa za kulevya zilizokamatwa kuwa na utata na kuwa hakuna uthibitisho Frank alikuwepo eneo la tukio siku hiyo.
Uamuzi majaji
Majaji hao walianza kwa kueleza kuwa, hiyo ni rufaa ya kwanza wanaagizwa kutathmini ushahidi kwenye rekodi ili kupata ukweli.
Jaji Wambali amesema kwa mujibu wa ushahidi kwenye rekodi, hakuna uhakika juu ya kile kilichoonekana na mashahidi wa upande wa mashtaka kwenye gari la washukiwa katika eneo la uhalifu.
Amesema pia kuna sintofahamu ikiwa kile kilichodaiwa kuonekana kwenye gari linaloshukiwa kilionyeshwa kwa wale waliokuwepo kwenye eneo la uhalifu kama inavyodaiwa na PW3 na PW6.
Hata hivyo, hakuna hata mmoja kati ya hao wawili (PW3 na PW6) aliyetaja jumla ya mifuko iliyokuwa kwenye gari linaloshukiwa katika eneo la tukio.
“Tathmini ya ushahidi inadhihirisha kuwa kutofautiana na kupingana kwa ushahidi wa mashahidi wakuu wa upande wa mashtaka katika kushughulikia madai ya dawa za kulevya eneo la tukio na katika ofisi ya RCO ambako upekuzi ulifanyika, kesi ya mashtaka iliharibiwa sana.
“Tuna maoni haya kwa sababu mlolongo wa matukio unaonesha kuwa ulinzi ulivunjika kwa kiasi kikubwa tangu mrufani wa kwanza na gari linaloshukiwa kukamatwa eneo la uhalifu kwa tuhuma za kusafirisha dawa za kulevya haukuwa sawa,” amesema Jaji Wambali.
Baada ya kupitia hoja zote majaji hao waliruhusu sababu za pili, tatu na tano za mrufani wa kwanza na sababu ya kwanza, tatu na tano za mrufani wa pili na kushikilia kuwa kesi haikuthibitishwa bila shaka na kuamuru waachiliwe huru.